Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kwa moyo wa dhati kabisa kutokana na changamoto za maji nchini, Taarifa ya Kamati imeelezea changamoto kwa kina na Waheshimiwa Wabunge humu ndani wote tunajua umuhimu wa maji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 174. Kwanza tu naomba nimwambie ukweli kwa sababu Mradi wa Bunda maji ni kama mtoto wangu niliyemlea tangu nikiwa Mbunge wa Viti Maalum, naujua vizuri sana na kwa sababu nataka kulisaidia Taifa hili, nitasema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, hivyo vituo ambavyo vinasemwa hapa vilivyojengwa ni Nyasura, Balili Msikitini, Balili Stoo na Kunzugu. Makubaliano katika ujenzi wa mradi huu wa maji, vituo vilikuwa vianzie kwenye chanzo cha maji Nyabehu. Hilo halijafanyika na kilichotokea Mamlaka yetu ya Maji Bunda ikaamua kujenga kituo kimoja Nyabehu. Vituo vingine vilivyokuwepo kama Tairo ni kituo ambacho chanzo chake ni ile miundombinu ya zamani, siyo mradi huu mpya, hilo Mheshimiwa Waziri naomba ulizingatie kweli kweli. Mradi huu wa maji Bunda kilikuwa kichaka cha watu kula fedha za Serikali ambazo ni kodi za wananchi kushirikiana na watoto wa vigogo na wewe unajua. Lazima tuseme haya, tunahitaji hii miradi ya maji ikamilike mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani miaka nane tunazungumzia chujio. Kuna habari nimezipata huko Wizarani kwako, aidha mmepigwa au mlikuwa mnataka kupigwa. Chujio la shilingi bilioni tatu mlikuwa mnaambiwa lijengwe kwa shilingi bilioni 12. Tunaipeleka wapi nchi hii? Kweli dhamira ya kumtua ndoo mwanamke kichwani itakamilika kwa ufisadi wa namna hii wakishirikiana na baadhi ya watendaji, ambao wengine mnawatoa Mtwara mnawaleta Bunda, mnawatoa Bunda mnawaleta Wizarani. Wizarani ambapo ndiyo kunasimamia miradi lukuki ya maji, hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mradi wa Maji tu Bunda unachukua miaka kumi na bado haujakamilika ina maana mnahitaji miaka 100 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji katika majimbo kumi, hilo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, huu mradi wa Bunda ni wa muda mrefu sana. Akisimama Mheshimiwa Boniphace atakwambia hivyo hivyo, akisimama Mheshimiwa Kangi atakwambia hivyo hivyo. Hatuhitaji Bunda Mkoa wa Mara kuwa kichaka cha wezi, tumechoka na hili tutaendelea kusema na tunaomba wachukuliwe hatua. Kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi walisema na Ofisi yangu ilitoa ushirikiano na bado baadhi ya wakandarasi na watumishi wengine wanapeta. Wanakula na nani? Please, huu wizi sisi hatuhitaji, tunahitaji miradi ikamilike wananchi wapate huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwako kunahitaji maji, Waheshimiwa Wabunge wote wanahitaji maji katika maeneo yao na hili nasema kwa dhamira ya dhati. Itokee sisi Wabunge na Mawaziri tukatiwe maji miezi mitatu, tu-feel pinch ambayo wananchi wetu wanaipata ya kukosa maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia kumsaidia mwanamke kutua ndoo ya maji kichwani. Waheshimiwa Wabunge kwa miaka mitatu mfululizo mwaka 2015/2016 fedha zilizotengwa zikapitishwa na Bunge hili ni zaidi ya shilingi bilioni 485, zilizotoka ni shilingi bilioni 136 sawa na asilimia 28. Mwaka 2016/2017 fedha zilizotengwa shilingi bilioni 913, zilizotoka shilingi bilioni 250 sawa na asilimia 25. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Aprili mwaka huu fedha zilizotengwa za maendeleo ni shilingi bilioni 673, zilizotolewa ni shilingi bilioni 135. Tunaenda mbele, tunarudi nyuma. Ile dhamira ya kuhakikisha mwanamke hatembei umbali mrefu kutafuta maji iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mitatu mfululizo! Yaani badala ya kupanda, tunashuka. Asilimia 28, 25, 22, why? Halafu tunakuja hapa tunasema kweli tuna dhamira ya dhati ya kuhakikisha tunamaliza tatizo la maji katika Taifa hili. Kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwenye Majimbo ya Vijijini kwenye mahospitali yetu kuna operesheni hazifanyiki kwa sababu maji hakuna hospitali. Naomba hili jambo mliangalie kwa umuhimu wake. Wanawake wanateseka.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani sasa hivi bora umpelekee mgonjwa ndoo ya maji hospitalini kuliko chakula. Kama wawakilishi wa wananchi hali hii hatutaikubali. Hii figure nimetoa za miaka mitatu mfululizo, nikiwatajia hiyo ya miaka nane ni aibu tupu! Halafu bado tunakuja tunasema tuna dhamira ya dhati, kweli! Hata asilimia 40 tu tumeshindwa kufikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza sekta ya umwagiliaji; tunawahamasisha vijana graduate kwenda kulima kilimo cha umwagiliaji. Mwaka 2015/2016 mahitaji ni shilingi bilioni 400. Bunge hili tulipitisha shilingi bilioni 53 kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji. Fedha zilizotoka ni shilingi bilioni tano; asilimia 10, shame! Shilingi bilioni tano! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wangu wa Nyatwali wana project kubwa sana ya kilimo cha umwagiliaji; kwa pesa hii inawezekanaje? Wale wa kwa Karukekere kwa Mheshimiwa Kangi, Mgeta kwa Mheshimiwa Boniphace na maeneo mengine! Lazima tuseme haya mambo, hatuwezi kuyafumbia macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zimekosekana, vijana wamehamasika kwenda kuwekeza kwenye kilimo. Kwa pesa hizi! Haya mwaka huu Bunge tulipitisha shilingi bilioni 24, zimetoka shilingi bilioni nne tu kwenye kilimo cha umwagiliaji. Four billion, halafu tunakuja hapa kwa mbwembwe nyingi kwamba tunataka kuboresha kilimo cha umwagiliaji. Kweli tuko serious? Tunaguswa na maisha ya Watanzania? Tunaguswa na tatizo la ajira la vijana wa nchi hii ambao wameona Serikali haiwezi kuajiri, wameenda kujiajiri kwenye kilimo cha umwagiliaji, kwa pesa hizi tutazigawaje? Hata kama sungura mdogo kiasi hiki, hata mkia hauwezi ukatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine miaka yangu yote nane ya Ubunge nimesikia upotevu wa maji DAWASCO ni ule ule asilimia 47. Ukienda kwenye ripoti ya CAG wamesema walishauriwa kununua chombo ambacho kitasaidia kudhibiti tatizo la upotevu wa maji. Mpaka leo kimya. Wizara yako inasemaje? Au kuna mradi wa watu hapa? Tunataka tujue.