Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini kabla sijachangia naomba ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais mwaka 2015 wakati anazindua Bunge hili aliposema maneno haya; “Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi na ukosefu wa maji vijijini. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanza miradi mipya na tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na maji salama.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili bajeti ya Wizara ya Maji ambapo hata wewe pamoja na kuwa uko kwenye Kiti umeshindwa kuvumilia maana hupati nafasi ya kuchangia, umezungumza habari ya uhitaji wa maji katika eneo lako. Uhitaji wa maji katika Taifa hili imekuwa ni janga kubwa sana na Bunge hili ni lazima lifanye uamuzi ambao utaisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia vitabu vilivyopita, nimeangalia Wizara ya Afya ina page 47; nimeangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ina page 45, nimeangalia vitabu kama vitatu, vinne hivi. Kitabu hiki cha Maji kuonesha kwamba Serikali imeshindwa kutekeleza iliyoahidi inapage zaidi ya 280. Hii ni kuonesha kwamba maneno mengi ni kutafuta kujitetea badala ya kutekeleza kile ambacho tumeahidi. Kama Serikali ingetekeleza asilimia hata kumi ya kilichoandikwa humu, Taifa hili lingefika mahali pazuri na tungeondokana na tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya REPOA ya mwaka 2018, asilimia 42 ya Watanzania wanakiri kwamba tatizo la maji limekuwa kero zaidi ya asilimia 34 ya mwaka 2014. Kadri siku zinavyokwenda, population ya Watanzania inaongezeka. Kwa hiyo, hata kama tungekuwa na maji kidogo miaka ya nyuma, kadri siku zinavyoenda lazima uhitaji wa maji uwe mkubwa. Mipango ya Serikali katika kutafiti, hebu tusaidieni mnataka Watanzania waishije ili akina mama waache kupoteza usiku na mchana kutafuta maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya CCM ambayo imeahidi kwenye Ilani ya CCM ya 2015, imesema itasaidia upatikanaji wa maji kutoka 67% mpaka 85%. Leo mnapeleka bajeti kwa asilimia 22, leo mnapeleka bajeti kwa asilimia 15, mnataka sisi tuamini nini mnachotuahidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda mbele, katika Kamati wanasema asilimia ya bajeti iliyopelekwa ni 22%, lakini Mheshimiwa Waziri anasema 56%. Kwa mujibu wa kanuni, taarifa zote zinazokuja Bungeni lazima zipitishie kwenye Kamati, Kamati i-verify. Nataka Mheshimiwa Waziri atuambie, tuamini taarifa ipi kati ya Kamati inayosema mmepeleka 22% na wewe unayesema tumepeleka 56%? Tunamdanganya nani hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili linahitaji maji. Mwaka 2017 tulisema tunataka angalau tuweke shilingi 50 kwa ajili ya maji vijijini, mkakataa. Mkatuambia mna fedha kutoka India dola milioni 500. Kwenye kitabu hakuna hata nusu page, hata nusu maneno uliyoahidi kwamba hizo fedha ziko wapi? Kwa hiyo, mnakuja mnadanganya Bunge ili tupitishe bajeti, lakini ukienda kwenye utekelezaji mnasahau hata maneno yenu ambayo mliyasema mwaka 2017. Fedha zile za India hiyo dola milioni 500 ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnashindwa kutekeleza bajeti hii kwa sababu tunawashauri wekeni fedha kwenye mafuta, hamtaki. Mnatafuta fedha hampati; lakini mnakuja hapa Mheshimiwa Waziri unatuambia mmepeleka hela ya maji kwa asilimia 26, halafu usiliombe Taifa radhi kwa kuacha Watanzania wateseke, halafu mnasema mnawasaidia akina mama. Badala ya kuwasaidia kuwaondoa ndoo kichwani, mnawatwisha ndoo kichwani, yaani mnaweka juu ya ndoo. Hata Naibu Waziri amejiridhisha, anasukuma kila siku toroli ya madumu ya wanaotafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza ahadi hizi ni lazima Serikali ioneshe commitment nzuri ya kupeleka fedha. Naomba kama Bunge tukubaliane tuweke shilingi 50 ili tupate fedha ya kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya vijijini. Bila hivyo hili tatizo litakuwa kubwa na maneno mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ni mazuri sana na ni mengi mno, lakini utekelezaji wake kama hauna fedha huwezi kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kuhusu Mamlaka ya Maji katika maeneo ya Halmashauri ambapo Serikali iliahidi kutekeleza kwa kusaidia fedha za ruzuku kwa ajili ya kujiendesha. Mheshimiwa Waziri atusaidie, kama Serikali iliahidi kutekeleza na kusaidia, kwa nini fedha haziendi na mpaka mwisho TANESCO inawakatia wananchi umeme na sisi tunakosa maji kwa kosa ambalo siyo la wananchi. Maana wananchi wanalipa bills zao lakini Serikali haipeleki. Kwa nini Serikali isiadhibiwe mnaadhibu raia ambao hawana makosa wala hawahusiki katika hili jambo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnashindwa kuchangia jambo hili, mseme hamuwezi kuliko kutudanganya na kuwaumiza wananchi wetu. Tukimpigia Mheshimiwa Waziri wa Nishati anasema sihusiki, tukimpigia mtu wa Hazina anasema hahusiki. Nani anahusika katika madeni haya ambayo mnawanyanyasa na kuwatesa Watanzania? Mnakata umeme kwenye maji ambayo akina mama wako hospitalini! Akina mama wanajifungua ninyi mnakata maji, hamjali. Sense of human iko wapi katika jambo hili na kosa siyo la kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme machache katika Jimbo langu, naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie, ahadi ya Serikali ya kukarabati mabwawa katika Kijiji cha Esilalei ambao Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa ziara yake ya kuomba kura, inatekelezwa lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa maji wa Monalo na Mheshimiwa Waziri anakuja, maana alikuja Monduli. Tangu 2011 mpaka leo wananchi wanaendelea kulalamika hawapati maji na ule mradi umegharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili. Huo mradi unakamilika lini na Serikali inapata ukakasi gani kuwashughulikia wote wanaokwamisha mradi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miradi ya umwagiliaji; katika miradi ya umwagiliaji Mheshimiwa Waziri anafahamu, alikuja na nilimtembeza pamoja na umri wake lakini alitembea. Tulienda Selela akaahidi, tulienda Mto wa Mbu akaahidi, tulienda Engaruka akaahidi kwamba watatupatia fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde hayo. Kwenye bajeti hii sijaona hata mahali ametaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anatutakia nini? Mbona tulimpokea vizuri naye alituahidi mengi? Mbona sioni hata nusu ya alichotuahidi kutusaidia? Alituahidi kutengeneza kile chanzo cha maji Ngaramtoni Mheshimiwa Waziri alifika mwenyewe, Monduli ilikosa maji akatuahidi. Mheshimiwa Waziri tumemkosea nini au tulimpokea vibaya? Wananchi wa Monduli wamekukosea nini? Alituahidi! Hakuna kwenye kitabu chake hata mahali ametaja hata ahadi moja aliyoahidi, kosa letu nini? (Makofi)

Mheshimiwa Waziri ulikuwa unatudanganya uondoke au ulikuwa unamaanisha kutusaidia kutatua matatizo ya maji? Ninaomba uniambie, wananchi wa Monduli wanakuamini na uliwaahidi, katika ahadi zako zote, mwaka huu unatutekelezea nini? Hakuna hata moja umetaja. Mheshimiwa Waziri kwa nini? Tumekutembeza Jimbo zima, tumeweka mafuta zaidi ya magari 20 tumekusindikiza, tumeenda na wataalamu, tumekuletea maandiko Mheshimiwa Waziri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mapendekezo matatu; moja, kwa kuwa miradi hii ya vijiji kumi na miradi mingi inaonekana haitoi maji kwenye nchi hii, naomba Serikali ifanye special auditing kwenye miradi yote ya maji ya nchi hii ili tujue ni miradi mingapi inafanya kazi na miradi mingapi haifanyi kazi mtuletee Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani nilishawishi Bunge tuweke azimio kwamba hatutapitisha bajeti ya Wizara hii mwakani mpaka mmetuletea special auditing ya miradi yote ya maji, maana mnatengea fedha miradi lakini ukienda kwenye mradi, hakuna maji. Tunataka kufanyike special auditing kwenye miradi yote ya maji nchi hii. Tufahamu ni miradi mingapi inatoa maji na mingapi haitoi maji. Tuna value for money. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumwambia Mheshimiwa Waziri kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli waliwahi kuleta fedha za consultant aliyekuwa anasimamia ile miradi hakufanya kazi, lakini Wizara ilituma fedha tulipe, nikasema hailipwi. Wizara inaniambia kwa nini unazuia, kwani ni hela zako? Nikasema huyu mtu hakufanya kazi, hakustahili kulipwa. Imekuwa ni uchochoro wa kupitisha fedha za Serikali. Wale wanaoitwa consultant wanawaambia walete engineer wanaleta hawa ma-technician wao mimi siwajui majina yao, lakini hakuna wanachofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ni muhimu Serikali ifanye tathmini ya miradi ambayo imetekelezwa na imekamilika na ambayo haijakamilika na iseme kwamba ni lini miradi hii itakamilika. Tumechoka na ahadi ya kwamba miradi itatekelezwa, miaka 10, miaka 15 mnatekeleza tu. Tutaanza lini mpya? Maana hakuna hata mradi mmoja mmeanza upya mnatekeleza ile ya zamani tu. Hata ule wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Nzega ni ya zamani mnatekeleza. Mnamaliza lini mwanze hii mipya? Ni muhimu mkatuambia kila mradi unaanza lini na unakamilika lini ili wananchi wawe na imani ya kwamba Serikali inafanya kazi na wao kuna siku watapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.