Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hoja hii ya maji na umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miundombinu mibovu ya maji katika Halmashauri zetu. Katika Halmashauri zetu, miundombinu ya maji ni mibovu sana ndiyo maana kuna upotevu wa maji. Kwa mfano, katika Ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017 inaonesha upotevu wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 huko Babati peke yake. Tuone ni namna gani tunapata hasara ya upotevu wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hapa Dodoma peke yake, karibu kila siku mabomba yanapasuka. Hii inatokana na kuweka mabomba yenye kiwango cha chini. Namwomba Mheshimiwa Waziri kufuatilia suala hili na kuhakikisha upotevu huu wa maji unadhibitiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije suala la bili za maji. Kuna watu wanaletewa bili za maji mpaka shilingi milioni mbili kwa mwezi, kwa kweli ni janga. Tumekuwa tukilalamika kila siku tukaambiwa hizo bili zitarekebishwa, lakini tatizo linaendelea. (Makofi)

Naomba kuuliza kwa Mheshimiwa Waziri, ni tatizo gani linalosababisha hizi bili ziendelee kupanda siku hadi siku. naiomba Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri, suala hili la bili za maji lishughulikiwe haraka iwezekanavyo kwa sababu wananchi wetu wanaumia. Hata sisi Waheshimiwa Wabunge wengi kati yetu tunapata bili hizo kubwa na ukienda kuwaonesha wanasema tunarekebisha, lakini hawarekebishi. Sasa kama inatokea hivi kwetu sisi Wabunge, je, wananchi wa kawaida inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la mikataba mibovu ya maji. Karibu nchi nzima kuna tatizo la mikataba mibovu na kusuasua kwa miradi ya maji. Nitoe mfano wa mikataba mibovu ya maji ambayo baada ya muda mfupi inavunjwa. Mfano, Mkoa wangu wa Njombe kuna mradi wa Lugenge, Utalingolo na Ihalula. Mradi huu ni wa mwaka 2013. Yule mkandarasi aliyewekwa kukamilisha mradi huu, mkataba ule ulivunjwa baada ya miezi mitatu na baada ya kuvunja ule mkataba yule mkandarasi alishitaki na baada ya kushitaki alishinda kesi yake. Hata baada ya kushinda hadi leo hii hajalipwa pesa zake, alitakiwa alipwe shilingi milioni hamsini hajalipwa na mradi huu hadi leo hakuna kinachoendelea na mabomba yamelala tu hapo. Naomba suala hili Mheshimiwa Waziri alifuatilie haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine vilevile wa Lwangu umetekelezwa na mkandarasi na hela zile za mwanzo zimepotea. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri afuatilie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ukosefu wa maji. Ukosefu wa maji ni janga la nchi hii. Ukiangalia maeneo mengi yana vyanzo vya maji, yana maji ya kutosha, lakini bado kunakuwa na tatizo la maji. Kwa mfano, Njombe inazungukwa na mito ya maji, lakini nenda pale Njombe Mjini unakuta watu wanapata maji mara moja kwa wiki.

Mheshimiwa Waziri ni tatizo gani? Ninaomba tafadhali fuatilia suala hili kuhakikisha hiyo miradi ambayo mmeahidi, basi itekelezwe kwa wakati. Tumekuwa tukiahidiwa sasa muda mrefu lakini hakuna utekelezaji. Siyo hiyo tu, kuna Wilaya ya Ludewa, vijiji vya Mkomang’ombe wananchi wale kwa kweli wanatia huruma. Wamekuwa wakiahidiwa kupatiwa maji… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)