Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu sana kwa ajili ya wananchi pamoja na akina mama. Naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na sasa hivi tupo muda huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji pamoja na Naibu wake, Kaka yangu Mheshimiwa Kamwelwe kwa kazi kubwa nzuri anaoyoifanya, anafanya kazi nzuri sana lakini Wizara yenyewe ndiyo ngumu, wananchi wanatakiwa watuliwe ndoo ya maji kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nizungumzie Mkoa wangu wa Katavi hususan Wilaya ya Mpanda, Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi. Naomba niipongeze Serikali ilileta miradi; Mradi wa Ikorongo I na Ikorongo II, lakini siku hadi siku watu wanaongezeka. Tulivyotegemea kuwa labda Ikorongo I katika vyanzo vile vya maji, yale maji yanaweza kututosheleza wananchi wa Wilaya ya Mpanda, imekuwa tofauti. Naishukuru Serikali haikuchoka, ikaongeza mradi mwingine tena wa Ikorongo II, lakini bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa sana ndani ya Wilaya ya Mpanda hususani pale mjini. Serikali ilijitahidi kutuletea maji, mabomba yale makubwa, lakini bado ndani ya maeneo yetu, miundombinu ya maeneo husika ambayo yanatakiwa yapelekwe maji hatukuweza kubadilisha ile miundombinu, ipo vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya zamani, ilikuwa ni yale mabomba ya zamani ya chuma. Mabomba ya chuma yanaota kutu. Sasa kama yanaota kutu, sidhani kama yanaweza kuchukua au kubeba mzigo mzito ambao unakuja kutoka katika matenki yetu. Maana yake maji kwenye matenki yanajaa, lakini sasa kwenye kupita njiani kule, lazima kuna mfumuko yale maji yanaweza kuvuja na mabomba yanapasuka. Sasa imekuwa shida sana pale Wilaya ya Mpanda maji ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua Serikali bado ina jitihada kubwa na sasa hivi kwenye bajeti ya Wilaya ya Mpanda nimeona shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya marekebisho mbalimbali kwa ajili ya matengenezo pale mjini. Bado kunatakiwa kazi kubwa sana kwa sababu wananchi wa Mpanda hawana maji kabisa sasa hivi, hususani Makanyagio, Majengo na Kashaulili ambapo ndiyo katikati ya Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi pale Wilaya ya Mpanda. Hawana maji kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia huu mradi wa Ikorongo, tulijenga magati Ilembo na Airtel. Magati haya katika Kata ya Ilembo, sasa hivi hayatoi maji kabisa. Airtel nako kwenye yale magati hayatoi maji. Katika huu Mradi wa Ikorongo nao vilevile haujaweza kutimiliza kwa sababu wataalam wamesema yanaweza kufika asilimia 50 tu wananchi wa Mpanda wakapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mwenyezi Mungu ametupa bahati kubwa sana. Ninashukuru Serikali kwa Mkoa wa Mwanza na Shinyanga wametoa maji kutoka Ziwa Victoria, Mungu ametupa neema yake, tumepata maziwa na mito. Sasa naomba nasi ndani ya Mkoa wetu wa Katavi, Mungu ametupa neema, tuna Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakitupa maji ya Ziwa Tanganyika, shida ya maji itakwisha kabisa katika Mkoa wa Katavi kwa sababu maji ya Ziwa Tanganyika yatatumika ndani ya Wilaya yetu mpya ya Tanganyika; Wilaya nzima itapata maji ya Ziwa Tanganyika, tutakuja sisi Wilaya ya Mpanda na Halmashauri ya Nsimbo wote watapata maji ya Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu sikivu na kaka yangu Mheshimiwa Kamwelwe, sasa hivi afanye mipango ya kuleta maji kutoka Ziwa Tanganyika ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupumua kwa sababu maji vijijini hakuna na ukiangalia Makao Makuu ya Mkoa hatuna maji. Naomba sana hilo liweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi, katika Mkoa lazima sasa tuanze system ya majitaka. Ndani ya Mkoa wetu wa Katavi hatuna system ya majitaka kabisa wala gari na matokeo yake mvua zikinyesha ni adha kubwa sana ndani ya Mji wa Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu sikivu, iweke mipango mikakati, nimemsikia Mheshimiwa Waziri kuna sehemu ambayo tayari miundombinu ya majitaka kwa mikoa kadhaa basi sasa na sisi Mkoa wetu wa Katavi ni mkoa, Wilaya ya Mpanda ni Makao Makuu ya Mkoa, tuanze sasa hivi mpango wa kujenga majitaka au basi tutafutiwe gari la kuweza kunyonya majitaka kwa sababu hatuna gari, hatuna kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye umwagiliaji; ninaishukuru Serikali, mipango ni mizuri sana ya umwagiliaji, lakini sisi tulijengewa miradi ya umwagiliaji Urwila, Ugala, Halmashauri ya Nsimbo, Kamsisi na Kata ya Mbede, lakini ile miradi sijaona kama imefanya kitu chochote. Naomba niulize swali moja, Mheshimiwa Waziri, hii miradi ya umwagiliaji hivi kwa nini tunatumia gharama kubwa sana lakini wananchi hawanufaiki kabisa. Leo hii ukiniambia Urwila wamenufaikaje kwa umwagiliaji, hakuna wananchi wa Urwila waliofaidika kwa ajili ya umwagiliaji na pesa nyingi sana zimetumika pale. Vilevile Kamsisi na Ugala pesa nyingi sana zimetumika, halafu tukija Mbede pesa nyingi zimetumika lakini miradi ya umwagiliaji bado hatujafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninaomba Serikali ijipange upya, miradi ya umwagiliaji bado hatujafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaendelea kufanyika, lakini ninaomba kuunga mkono hoja Mamlaka ya Maji Vijijini. Mamlaka hii itatusaidia sana kwa sababu wananchi wa Vijijini wengi wao ndani ya vijiji vyetu hatuna maji, lakini mamlaka hii ikiundwa itatusaidia sana kwa sababu itafanya kazi vizuri. Tulianzisha TARURA, tumeona jitihada za TARURA, nafikiri tukianzisha Mamlaka ya Maji Vijijini nayo inaweza kutusaidia sana akina mama, tutawatua ndoo kichwani. Naomba niunge mkono hoja hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba katika ile shilingi 50 tuongeze iwe shilingi 100 ili sasa mamlaka hii iweze kuwa na nguvu... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana naomba nipongeze.