Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hapa amezungumza kwa kiasi kikubwa sana na amejaribu kueleza kwamba Tanzania ni nchi ya nne Afrika kwa upatikanaji wa maji ambayo yapo chini ya ardhi ikitanguliwa na nchi ya Zambia, Mozambique, Sudan ya Kusini na ya nne ni Tanzania. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu ametujalia maji mengi sana Tanzania, suala lililopo ni Wizara husika kuhakikisha kwamba wanaweka mikakati ambayo inatekelezeka, mikakati ambayo mwisho wa siku itakuja kuzalisha maji na wananchi waweze kuyapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota amezungmza mradi ambao amezungumza zaidi ya miaka mitatu hivi sasa pale Mtwara, mradi ambao unatoka katika Jimbo la Nanyamba kule eneo la Mayembe Chini unakuja mpaka Mtwara Mjini. Huu mradi hivi sasa ni zaidi ya miaka minne haujakamilika na kila mwaka tunavyokuja ndani ya Bunge tukija kuhoji tunaambiwa watu wa Benki ya Exim ya China hawajatoa pesa na Serikali ipo kwenye majadiliano, tumefikisha suala hili katika Wizara ya Fedha, kwa muda mrefu na huu ni mwaka wangu wa tatu nazungumza ndani ya Bunge hili kwamba ule mradi vijiji vimechukuliwa zaidi ya vijiji 26, wananchi wamechukuliwa maeneo kutoka Jimbo la Nanyamba, Mtwara Vijijini mpaka baadhi ya mitaa ya Mtwara Mjini wamechukuliwa maeneo zaidi ya miaka mitatu hivi sasa, hawajapewa fidia kwa kigezo kwamba Exim Bank ya watu wa China haijatoa pesa za mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Wizara ya Fedha, inavyopanga mikakati yake kwa sababu hili ni jambo la pili kwa Mtwara, liko jambo la ardhi pia Wizara ya Fedha iliahidi itatoa pesa kwa ajili kulipa fidia kupitia UTT lakini hawatoa pesa, mwisho wa siku wananchi wamechukuliwa maeneo yao. Kwa hiyo, hata hapa pia kwamba pamechukuliwa zaidi ya miaka mitatu wananchi hawa wanapaswa kulipwa fidia ili sasa na wao waweze kufanya shughuli zingine kwa sababu mashamba yao yamesitishwa kupisha mradi huu. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ihakikishe Wizara ya Fedha inapeleka fedha kwenye miradi ya maji ili kuondoa matatizo ambayo tumezungumza kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilizungumza hapa mwaka jana na mwaka juzi kwamba Mtwara Mjini hatuna tatizo la maji pale chini, kuna mradi ambao Serikali ilitenga bilioni tano ambapo mkandarasi alikuwa site, mkandarasi tayari ameshatafuta maji, maji yamepatikana, tumefanya pump test na maji yalikuwa ni mengi sana. Maji mengine ile clip niliichukua nikamrushia Mheshimiwa Waziri kumjulisha kwamba maji yamepatikana Mtwara Mjini katika eneo la Lwelu tunachohitaji sasa ni Wizara kutoa pesa ziweze kujenga visima, ziweze kujenga mtaro, ziweze kusambaza maji kuna maeneo zaidi ya kata tano Mtwara Mjini tuna tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwamba hawa wakandarasi tunaowapa miradi hii kuweza kutekeleza kwa sababu yule mkandarasi alishasema kwamba tayari amesha-raise certificate ameshapeleka Wizarani suala lililobaki ni yeye kulipwa zile pesa ili aweze kuchimba visima aweze kusambaza maji katika kata za Mtwara Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nimtajie Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo Mtwara Mjini tunashida ya maji ziko kata zaidi ya nne hapa, katika Kata ya Mitengo pekee eneo la Mitengo Juu hatuna maji, wananchi hawana maji, eneo la Mji Mwema, Vitengo hakuna maji, Kilima Hewa hatuna maji, maji hayapo kabisa Kata ya Ufukoni, Kihole hakuna maji, Comoro ambako hata mimi mwenyewe ndiyo naishi huko hakuna maji, yaani anapoishi Mbunge maji hakuna. Lakini Soko Jinga hakuna maji, Kwa Selemu hakuna maji, Mbaye Juu hatuna majina, Mtwara Mjini na maji chini yako mengi na mkandarasi yuko site, pesa hapewi kwa ajili ya kusambaza maji. Kwa hiyo, naomba sana huyo mkandarasi certificate ameshatoa, kazi ya Wizara ni kutoa pesa ili huyu jamaa aweze kuchimba visima na aweze kusambaza mabomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ni pamoja na eneo la Chipuputa nalo pia liko Mtwara Mjini maji hatuna, tuna eneo la upande wa Magereza hakuna maji, kuna Mbawala Chini ile mitaa ambayo inatoka nje ya mji kidogo ambayo mwanzo ilikuwa vijiji kote hakuna maji Mbawala Chini, Naulongo, Dimbuzi, Mkunja Nguo, Mwenge, Naliendele Mikoroshoni kote hatuna maji wakati maji Mtwara yapo kedekede, suala lililobaki ni Wizara kutoa pesa kumpa mkandarasi ili aweze kusambaza haya maji na wananchi wa Mtwara Mjini waweze kupata maji kwa sababu tuna maji baridi kweli pale chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba sana Wizara ihakikishe mwaka huu huyu mkandarasi anapewa fedha ili aweze kusambaza haya maji wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini wanahitaji maji kwa kiasi kikubwa sana. Pale ambapo kuna miradi hii ya visima ambavyo vimejengwa kuna wakati fulani tulitembelea maeneo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini kupitia Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, utakuta vyanzo vimejengwa vizuri sana pesa zimetumika nyingi sana kujenga hii miradi, lakini vile visima havijafunikwa yaani siku moja anaweza akatoa mtu tu huko chizi chizi akaja akaingia pale akamwaga uchafu akamwaga nini wananchi wanaweza kupoteza maisha, kwa sababu ya ulinzi wa visima vya maji Tanzania miradi hii mikubwa ya maji lazima ifunikwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa za nchi zingine maeneo mengi visima vya maji vimefunika, Tanzania visima vya maji viko naked na ulinzi wenyewe ukiangalia hakuna ulinzi wa kutosha, wakati maji ndiyo maisha ya Watanzania. Naomba sana hii miradi inavyotekelezwa kutengewe pesa maalumu, bajeti ya kufunika visima Ruvu Chini, Ruvu Juu visima vifunikwe Mtwara Mjini pale Mangamba visima vifunikwe (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati fulani taarifa zinasema wakati wa kampeni mgombea mmoja alienda akawatumia wale watumishi wa pale, akamwaga uchafu ndani ya maji, wananchi wa Mtwara tukanywa kwa sababu ulinzi wenyewe hautoshi. Sasa hii siyo Mtwara ni Tanzania nzima. Kwa hiyo, naomba sana kwamba Wizara itenge bajeti ya kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji hivi visima hivi vya maji, mabirika haya ya maji yanafunikwa kunakuwa na ulinzi kwa ajili kuwafanya Watanzania waweze kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni mtu wa Mtwara, lakini nilikuwa naishi Lindi kama mwalimu, kuna Mradi wa Ng’apa ambao umeanza kujengwa zaidi ya miaka saba hivi sasa pale Lindi, mradi ambao ulitakiwa uende kuwanufaisha wananchi wa Lindi Mjini, wananchi wa Mitwelo pale lakini huu mradi unasuasua sana zaidi ya miaka saba sasa, mkandarasi aliyepo pale yupo taratibu sana, tunashangaa tatizo ni nini? Kwa nini maeneo mengine ya nchi hii wakandarasi wanakuwa wanakimbia kimbia hivi lakini ukija maeneo ya Kusini wakandarasi wapo taratibu na hawachukuliwi hatua yoyote. Tuna mradi huu wa Ng’apa ni wa muda mrefu wananchi wa Lindi wana matatizo kuliko maeneo yote ya Kusini mwa Tanzania hawana maji ya kutosha, maji pale Ng’apa yapo na ule mradi utatoa maji mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu kila mwaka tunaambiwa hapa mkandarasi atamaliza mwaka huu naomba usimamizi uwe wa kina yule mkandarasi amalize mradi wa Lindi Mjini ili wananchi wa Lindi Mjini waweze kupata maji na wananchi wa Mitwelo kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la bill za maji, kumekuwa na malalamiko makubwa sana Tanzania, kumekuwa na malalamiko Mtwara Mjini kumekuwa na malalamiko Mikoa ya Kusini Lindi kumekuwa na malalamiko mpaka Dar es Salaam, kwamba watu wanakadiria tu bill za maji yaani wale wanaokuja kuchukua bill za maji kusoma mita hawasomi mita wanakadiria tu unaambiwa mwezi huu unalipa shilingi 40,000 mwezi huu unalipa shilingi 50,000 wakati hawajasoma exactly ni cubic meter ngapi zimeweza kutumika kwa mwezi husika, kwa hiyo, naomba Wizara iangalie hili suala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 nilizungumza kuhusiana na Mtwara Mjini lakini hili suala haliko Mtwara Mjini ni Tanzania mzima, wasomaji wa mita hawasomi mita wanakadiria na kuwabambikiza wananchi bill za maji kubwa ambazo ni kinyume kabisa na uhalisia wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la upotevu wa maji ni jambo ambalo limekuwa ni chronic hivi sasa, sisi tunaishi Dodoma hapa, ukipita mitaani huko maji mabomba yanapasuka sana, mabomba yanavuja sana kuna sehemu zingine barabarani kumetengeneza mpaka mabwawa, ukienda hapa Dodoma hapa njini tu eneo la Chadulu ukifika pale kila siku maji yanavuja na unatoa taarifa kwa watu wa maji hawaji kurekebisha. Tanzania nzima iko hivyo Dar es Salaam napo hivyo, leo mbona likipasuka unaweza ukatoa taarifa kwa watu wa Idara ya Maji wanachukua muda mrefu sana kuja kurekebisha. Tunaomba sana maji yanapotea kwa sababu haya maji yanatumia gharama sana kuyachimba kupatikana kwake na kuyasambaza yasiachwe yanamwagiga yanapotea.