Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia na naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu hii ukiitazama ina matatizo makubwa mawili; la kwanza ni tatizo la fedha ambalo limesemwa na kila Mbunge; lakini la pili kama walivyosema baadhi ya Wabunge ni tatizo la uwezo wa matumizi ya pesa zenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni mwa mwaka huu Mheshimiwa Waziri alifanya ziara na alikuja Geita na yeye mwenyewe akawa anashangaa kuona maji hakuna, anashangaa kuona malalamiko ya maji yako nchi nzima lakini anasema ana takriban shilingi bilioni 50 kwenye akaunti na tatizo ni kwamba hakuna mtu analeta certificate kuonesha kwamba kuna kazi zinaendelea.

Kwa hiyo, ina maana tuna matatizo mawili, la kwanza inawezekana tuna tatizo la pesa ambalo ni dogo lakini tuna tatizo la uwezo wa kutumia pesa kutoka kwenye Wizara yenyewe na pengine inawezekana ni uwezo wa watu walioko chini kwenye Wizara wanaoweza kusababisha pesa zitumike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kuimarisha sana uwezo wa watu wake huku chini. Kuna lugha mbili zinazungumzwa hapa, Mheshimiwa Waziri anasema msiangalie sana ring fence ya bajeti yenu kwenye Halmashauri, anzisheni miradi, tengenezeni certificate mlete tulipe, lakini walioko kule chini wanaangalia kile ambacho wamepewa na Serikali ndiyo wanatangaza na pengine hawatangazi mpaka waambiwe pesa zipo. Kwa hiyo, inawezekana kuna tatizo la mawasiliano kati ya ofisi ya Mheshimiwa Waziri na watu wake ndiyo maana malalamiko ni mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali, kwa miaka yote miwili mfululizo tumekuwa na tatizo kubwa sana la maji katika Mji wa Geita. Katika taarifa yake ukurasa wa 53 amekadiria kwamba hivi sasa upatikanaji wa maji katika Mji wa Geita ni kama takribani asilimia 37. Inawezekana takwimu hizi Waziri ameletewa lakini siyo kweli, Geita takwimu hizi ambazo nazipinga upatikanaji wa maji uko chini ya asilimia 15 na sababu ni kwamba maji yaliyoko Geita ambayo yanasukumwa na mgodi wa GGM, makubaliano ya uanzishwaji wa mradi ule ilikuwa Serikali ichangie asilimia 50 na mgodi asilimia 50, mgodi ukatumia shilingi bilioni 12; lakini Serikali ikatoa shilingi 400,000 peke yake. Kwa hiyo, matokeo yake ule mradi umekamilika lakini uwezo wake wa kufanya kazi unafikia kaya 1,700 peke yake. Mara nyingi Mji wa Geita hauna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hivi karibuni GGM wamesema wanajiondoa kwenye uendeshaji wa mradi ule na sasa hivi GEUWASA walikuwa wanakusanya mapato bila kuingia gharama ya kupeleka umeme wala kusukuma umeme kutoka kwenye chanzo cha maji. Maana yake ni kwamba muda mfupi ujao GGM wakijiondoa, GEUWASA wanatakiwa waanze kujilipia mwenyewe gharama ya uendeshaji na mradi ule uko category C.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ya namna gani tunamaliza tatizo la maji katika Mji wa Geita. GGM watakapoacha kusukuma maji kwa sababu wanasema gharama ni kubwa na walikuwa wanatumia pesa za CSR ambazo Serikali kupitia sheria tuliyorekebisha hapa Bungeni tumewanyang’anya sasa tumezipeleka halmashauri, kwa hiyo, hawana tena uwezo wa kutumia zile pesa na wao hawana fungu lingine kwa maelezo yao na kwa mwezi mmoja wanatumia milioni 70 maana yake ni kwamba GEUWASA hawana uwezo tena wa kusukuma maji, hata hii asilimia 15 tunayoipata sasa hivi haitakuwepo. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri aje na majibu ni namna gani ataondoa tatizo hili kwa sababu tumesubiri pesa za India leo mwaka wa tatu hazionekani na muda unakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi pale wa LV- WATSAN na kwa nini nimesema tunalo tatizo la matumizi ya pesa na usimamizi, huu mradi una pesa tayari shilingi bilioni sita, Waziri ametaja kwenye taarifa yake lakini mradi ambao ungekabidhiwa mwezi Novemba, 2016; leo Mei, 2018 mradi huu haujakamilika na mkandarasi hayuko site, maana yake ni nini? Amesema mradi huu utakabidhiwa Mei, namhakikishia Mheshimiwa Waziri sio kweli kwa sababu sisi tunatoka kule site tangu alivyoondoka matenki na mabomba yako vilevile na mkandarasi haonekani na kama anaonekana atakuwa anafanya kazi nje ya mkataba kwa sababu alishasimamishwa na Wizara na watu wanaomsimamia. Sasa kama pesa zilikuwepo shilingi bilioni sita na hakuna tatizo la pesa hapa lakini mradi hauendi leo mwaka wa tatu maana yake ni kwamba liko tatizo pia la uwezo wa kumsimamia huyu mkandarasi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri pengine leo atakuja na majibu sahihi kwamba huu mradi wa LV-WATSAN utakamilika lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita tunashangaa kuona tunapokuja na bajeti ya visima, sisi tuko kilometa nane tu kutoka ziwani. Watu wa Shinyanga, Tabora na sehemu nyingine wangezungumzia visima nisingeshangaa, sisi tunataka maji ya ziwa. Pale kama Serikali itawekeza maji kutoka ziwani ukapandisha kwenye ule mlima ulioko pale Geita, maji yatashuka yenyewe kwa gravity kwenda mpaka Kahama, kwa nini tunahangaika na visima katikati ya Mji wa Geita ambavyo kiangazi vyote vinakauka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini moja ya miji inayokuwa haraka sana kutokana na shughuli za madini na mwingiliano wa watu ni Mji wa Geita. Nimeona humu kwenye ripoti ya Waziri wamekadiria wanapeleka maji kwa watu 130,000, sisi Geita pale tunaamini kuna zaidi ya watu 300,000 sasa hivi na tunahitaji maji mengi sana ili tuweze kuendelea na shughuli zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii ametupatia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji. Mwaka jana walitupatia tena shilingi bilioni mbili ambazo zilitupa kama kilometa 80 za mtandao wa maji. Tatizo kubwa tulilonalo ni maji machache ambayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)