Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nichangie Wizara ya Maji. Kwanza kabisa napenda kumpa pongezi Waziri wa Maji, Mheshimiwa Isack Kamwelwe kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwenye Wizara hii. Pia napenda nimpongeze Naibu wake, Mheshimiwa Aweso, wote kwa pamoja mnajitahidi kufanya kazi ya kutatua matatizo ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda niungane na Wabunge wenzangu waliochangia kuhusu kuongeza shilingi 50 kwenye petroli na dizeli ili iweze kusaidia bajeti ya maji kwa kupata chanzo kikubwa cha kuendeleza miradi ya maji. Naungana na Wabunge wenzangu waliounga mkono hoja ya kuongeza shilingi 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali iongeze bajeti ya Wizara ya Maji. Bajeti ya Wizara ya hii ni ndogo ukilinganisha na mahitaji ya maji nchini Tanzania na mikoani kote. Kila mahali unapoenda iwe ni vijijini, wilayani na city center ni kilio cha maji. Niiombe Serikali iongeze bajeti ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naenda moja kwa moja kwenye Mkoa wangu wa Katavi. Mkoani kwangu Katavi, Wilaya ya Mpanda tunalo Bwawa linaloitwa Milala. Bwawa hili limechimbwa miaka mingi tangu enzi za ukoloni, enzi za Mpeluki kwa wale wanaotoka Katavi wanafahamu lilikuwepo toka kabla ya uhuru. Bwawa hili lilikuwa linatumika ku-supply maji pale Mpanda Mjini kwa matumizi ya wananchi wote wa Manispaa ya Mpanda. Sasa hivi bwawa hilo haliwezi kutumika tena kwa sababu lina viboko wengi wamezaliana pale, wanakula mazao ya wananchi, mipunga, mahindi, wanachafua maji kiasi kwamba yale maji ya bwawa hilo hayawezi kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara ya Maji na Umwagiliaji ishirikiane na Wizara ya Maliasili na Utalii iwatoe hawa viboko ili yale maji yaweze kutumika. Manispaa ya Mpanda, kata nyingi hazina maji, Kata za Mpanda Hoteli, Ilembo, Magamba na Shanwe, zote hizo hazina maji. Kwa kusafisha haya maji yaliyoko kwenye Bwawa la Milala litafanya kata hizi ziweze kupata maji. Nimeshawahi kupeleka hili swali ili lije hapa Bungeni niliulize, lakini nashangaa limechukua miaka miwili halijaletwa hapa kuhusu kuhamishwa viboko hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukichukulia kwamba hilo bwawa liko mjini pale Mpanda, zamani lilikuwa ni nje ya mji lakini sasa hivi limezungukwa. Kwa hiyo, kuwa na viboko ni hatari na kuna shule ya sekondari ya Mwangaza iko karibu na hilo bwawa, watoto wa shule wanakwenda pale kuchota maji na viboko wenyewe huwa wanatembea kutoka kwenye bwawa hilo wanakuja mpaka Mpanda Mjini. Niiombe sana Serikali na Waziri Mheshimiwa Kamwelwe iweze kututatulia hilo tatizo la viboko Mpanda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala la viboko, niende moja kwa moja kwenye suala la maji ya visima. Kwanza Mpanda tunashukuru kwa visima vya maji lakini niombe sana vile visima ambavyo vinatumia mkono muangalie uwezekano wa kuweka solar ili wale akina mama wa vijijini na hasa wazee waweze kuchota maji yale. Muweke pump inayotumia umeme na tape ili akina mama wale waweze kuchota maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, visima vingi vimechimbwa kule lakini havijakwisha na vingi ni vya ku-pump na akina mama vijijini ambao hawana nguvu wanashindwa ku-pump yale maji. Mnaweza mkatumia umeme wa solar kwa sababu umeme wa REA haujapita kwenye vijiji vyote vya Mpanda na ukizingatia kwamba Mkoani kwetu Katavi hakuna umeme wa gridi. Niombe basi uweze kutumia umeme wa solar ili akina mama wa Mkoa wa Katavi waweze kufaidika na maji haya ya visima ambavyo vinaendelea kuchimbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napende kuzungumzia miradi iliyoko Mkoani Katavi; tunao mradi wa Ikorongo II ambao utaleta maji kwenye vijiji vya Magamba. Nafahamu Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba lipo tank la Mwanamsenga kule Ilembo ambalo halifanyi kazi limechoka. Niombe likarabatiwe ili vijiji vile vya Magamba viweze kufaidika na maji hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba vile visima vinajengwa kule Mkoani kwetu Katavi ni temporary. Nimwombe Mheshimiwa aharakishe kuleta mradi mkubwa Mkoani Katavi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika ili yaweze kusambazwa Mkoa mzima wa Katavi. Maji ya visima ni temporary measure, utakapoletwa mradi mkubwa wa kutoka Ziwa Tanganyika utaweza ku-supply vijiji vingi vya Mkoa wa Katavi na Waziri anafahamu miundombinu ya mkoa wetu si rafiki. Kwa kupata maji haya inaweza ikawarahisishia akina mama shughuli nyingine za biashara ambazo wanaweza wakafanya kutokana na haya maji yatakayotoka Ziwa Tanganyika. Maji haya pia yataweza kusaidia mikoa ya jirani kama Mkoa wa Rukwa, mkoa wetu wa zamani ambao tulikuwa pamoja, haya maji yanaweza yakafika pale kwa kupitia Jimbo la Kavuu mpaka Sumbawanga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la umwagiliaji. Kule mkoani kwetu Katavi miradi ya umwagiliaji iko nyuma sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri miradi ambayo ilikuwa imeanzishwa Mkoani kwetu Katavi ifuatiliwe ili iweze kuendelea. Miradi ilianzishwa lakini mimi kama mimi sijaiona ile miradi kwamba imekwisha na hatuelewi ilifikia wapi na taarifa kama vile Wabunge wengine wamekuwa wanazungumza inatakiwa ieleweke ile miradi huwa inakuwa chini ya nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa umwagiliaji Kata ya Ugala lakini jinsi ulivyoisha sielewi uliishaje na sielewi ulikuwa chini ya usimamizi wa nani na maelezo yake hayaeleweki. Niiombe Wizara ya Maji ijaribu sana kuwa inafuatilia kwa ukaribu miradi yote ya maji ambayo inaanzishwa humu nchini ili kuona kwamba mradi huu umegharimu shilingi ngapi na zimebakia shilingi ngapi na wamelipwa shilingi ngapi. Kama mradi umetolewa pesa na haujakamilika basi wale watu wanaohusika na hiyo miradi waweze kuwajibika. Tunaona tu kwenye makaratasi kwamba kuna mradi huu wa maji lakini miradi inakuwa haijaisha na pesa hazijulikani zimekwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie suala hili la maji. Napenda sana kumshukuru Rais kwa hatua aliyoichukua jana pale Morogoro kumpigia simu Katibu Mkuu wa Maji lakini nafikiri hili suala lilikuwa ndani ya Waziri mwenyewe wa Maji na Naibu wake kufuatilia ile miradi ya maji. Basi niombe wawe wanaifuatilia kwa karibu ili suala la maji lisilete tatizo sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu maji taka kwenye Mkoa wetu wa Katavi. Miundombinu ya maji taka ya Mkoa wa Katavi bado, nimwombe Wazir Kitengo cha Majitaka kiweze kufuatiliwa kwa sababu ule mkoa ni mpya lakini suala la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.