Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaingia Bungeni hapa nilijifunza kupitia Wizara tatu ambazo zilikuwa pressure kubwa sana kwa Wabunge wote ambazo ni Wizara ya Maji, Wizara ya Afya na Wizara ya Ujenzi. Sasa najiuliza mara mbili mbili sielewi ndiyo maana sasa hivi wanawake wana kamsemo wanasema wanawake wanaweza. Hivi kwa nini pressure ya Wizara ya Afya imeisha kabisa yaani hata nilikuwa nasikiliza Wapinzani wanashauri lakini Wizara hii kila mwaka humu ndani lazima tulumbane, kuna tatizo gani Wizara ya Maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona hata Rais akienda kwenye ziara huko mikoani kwetu anapata pressure na maswali mengi na mabango ya maji. Ndugu yangu, rafiki yangu Kamwelwe kwani wewe huwezi kumaliza matatizo yako ukawa mbunifu kama Mheshimiwa Ummy alivyofanya kwenye Wizara sumbufu kabisa ya Afya? Gari mpya umepewa, mafuta yapo, ukija mikoani tatizo dakika mbili huyo kwenye ziara kwa Mkuu wa Mkoa, hukai na walengwa/ wawakilishi wakakuambia matatizo? Huwezi kuyamaliza haya matatizo kwa kuja unajifungia kwenye air condition kwa Mkuu wa Mkoa unaenda kuonyeshwa miradi tu iliyofanya vizuri, miradi mibovu hauonyeshwi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongee kidogo na Mheshimiwa Waziri. Tunaona kuna zoezi linaendelea kwamba wakandarasi wengi wamelipwa asilimia 80 lakini kazi hazifanyiki. Nataka nikwambie Waziri mtawafunga wakandarasi wote. Hii miradi ya maji ya Benki ya Dunia asilimia 90 ya wakandarasi waliofanya hizo kazi wengi wameuziwa nyumba na wengine wame-paralyze kwa sababu mnawasainisha mikataba ya mabilioni ya hela halafu hela haziendi. Mtu anafanya kazi, amekopa benki bilioni aki- rise certificate ya 500 inakuja baada ya miezi tisa nyingine miaka mitatu, nyumba imeuzwa na pressure anayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Waziri asiunde Tume ikachunguza hizi hela zinarudi Wizarani kwako. Nataka nikwambie usiposikia ushauri wetu utapambana na maswali bajeti ijayo. Kule Wizarani kwako kuna watu wanacheza na watu wa huko Halmashauri hela zikija zinarudi kwako huko huko. Mimi nimekuwa Meya nafahamu, nimekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri nafahamu, makampuni ya ushauri ambayo yanatutia hasara kwenye Halmashauri zetu yako ndani, ni ya watumishi wa Wizara yako na unao. Sasa ni bora ukasikiliza mawazo ya Wabunge ukaunda Tume ikaenda kuchunguza, kama hauwezi umuombe Spika aunde Tume ya Wabunge ikachunguze hili suala tukija bajeti ijayo mzee tusikuulize haya maswali mengi mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuuliza rafiki yangu Mheshimiwa Waziri na ulipita jimboni kwangu, hivi kweli kitabu kizima cha kurasa 200 na kitu hata shilingi milioni tano hamna kwenye jimbo langu au ni style gani tuitumie kuomba? Jimbo langu mimi asilimia 85 ni ziwa, lakini hatuna maji, kweli Waziri hata kisima kimoja? Labda wengine humu tumekuja kwa bahati mbaya au mtufundishe style ya kuomba ili tuweze kupata angalau hata visima viwili. Mbunge unajadili bajeti nzima ya mabilioni unatoka humu unasifia tu wenzio hata kisima kimoja hamna, kweli Mheshimiwa Waziri? Nisikitike sana lakini nina imani wewe mzee ni msikivu na ni mtani wangu utatekeleza, nadhani utaangalia hata kwenye ukokoukoko huo utupie hata visima vitatu kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na suala la kuongeza shilingi 50 kwenye mafuta. Nashauri kabisa kama walivyoshauri Wabunge wengine, Wabunge wote tuazimie na wewe ufanye kazi ya kubanana na sisi ile shilingi 50 iongezwe. Sisi wengine huku vijijini bado tuna uhitaji mkubwa sana wa maji. Mheshimiwa Waziri nilishawahi kukwambia kwamba kwangu kuna mradi umeshapitwa na Wabunge watatu walionitangulia wa shilingi bilioni 1.2 skimu ya umwagiliaji, mashamba ya watu mmechukua, kutengeneza hamtengenezi, mmeleta shilingi milioni 200 zimeisha kugawana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri Wizara yako hii Wahandisi wa Maji wengi walioko kule Wilayani kwetu siyo Wahandisi wa Maji ni Environmental Engineer ndiyo wanaokuangusha. Jaribu kufanya paranja, ma-engineer wa maji wapo wengi vyuo vikuu vinatoa acheni kufanya upendeleo kuweka watu wasiohusika. Mtu wa mazingira na visima wapi na wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu namheshimu sana nilitaka nichangie tu hapo lakini nikwambie Mheshimiwa Waziri kama alivyosema Mbunge mwenzangu wa Geita unavyosema asilimia za maji zilizoko Geita watu wanatushangaa sisi humu Wabunge ndani. Hebu jaribu uje hata ziara ya kushtukiza uone hizo asilimia unazozitaja kwenye kitabu haziko Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi mingi imekwama, Chankorongo na Mharamba kwenye jimbo langu haitekelezeki. Mtu anamaliza mradi wa shilingi bilioni tano anakabidhi wiki moja hautoi maji, lakini ukija wanakuchukua unakaa kwa Mkuu wa Mkoa unateleza na air condition.

Mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri sihitaji kubishana na wewe mzee wangu, baada ya Bunge hebu njoo mkoani kwangu ufanye ziara, hasa Jimbo la Geita Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.