Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Waziri kwa hotuba na kwa bajeti yake ambayo ameweza kutuwasilishia. Niombe kumshukuru kwa Bwawa la Dongo ambalo limewekwa kwenye mpango ambapo hili bwawa sasa kwa pesa zilizotengwa japo ni kidogo, lakini naomba hizo pesa zitoke na usanifu uendelee ili wale wananchi wa vijiji vya Dondo na Laiseri viweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kiteto ina tatizo kubwa sana la maji kwa kipindi kirefu na kwa maeneo mengi ambayo tumekuwa na tatizo na maji ni kwamba tuliahidiwa kupata mabwawa kwa sababu yale maeneo ni kame. Ninaomba Waziri na Wizara yake waweze kutusaida kukarabati mabwawa yetu upande wa Makame, bwawa ambalo lilichimbwa na wananchi lakini halijakamilika katikati ya Lukiushi na Makame.
Ninaomba pia kukarabatiwa Bwawa la Matui ambalo Mheshimiwa Waziri uliliona, ulilikagua na ukaona kwamba linastahili kukarabatiwa na ni bwawa kubwa ambalo linastahili kukarabatiwa na lipate pesa kwa ajili ya maji ya binadamu, pia umwagiliaji kwa ile kanda ambayo kuna wananchi zaidi ya 20,000 ulijionea mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna bwawa la umwagiliaji la Enguselo, hili bwawa limefanyiwa upembuzi yakinifu wananchi walishaachia yale maeneo yao kwa hiari yao na maeneo mengi yameshaachwa kwa muda mrefu na mashamba wameyaacha. Sasa ni lini Wizara itatenga pesa muda wa kufanya uhuishaji kwa kukarabati lile bwawa na kulijenga tayari kwa wanachi kuweza kulitumia kwa ajili ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mabwawa mengi kwa sababu Kiteto ni eneo kame, na jambo la kutusaidia ni mabwawa, kwa mazingira yetu ya wafugaji na wakulima ni lini Serikali itatusadia kupata mabwawa upande wa Makame, Ndido, Rorela, maeneo ambayo ni kame lakini wafugaji wengi hawana mabwawa na mifugo inalazimika kwenda upande wa Simanjiro, upande wa Kilindi na kwenda upande ambako mifugo yetu inalazimika kutafuta maji ikihangaika huku na kule na wafugaji wanapata shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo miradi mingi ya vijiji ambayo haijakamilika, tunaomba Serikali itusaide ni namna gani tunaweza kupata pesa ili hii miradi ya vijiji vya Dosidosi, Ndughu, Nguselo, Lergu, Ndido, Songambele na vijiji vyetu vingi ambavyo sasa vipo kwenye mpango vingine nimevitaja kwenye maandishi baada ya kuwa nimekuandikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kwa mpango wetu bajeti tuliyotengewa ni ndogo, karibu shilingi bilioni 1.329, sasa Mheshimiwa Waziri kwa pesa hii umepunguza bajeti yetu kwa bajeti ya mwaka jana, kwa bajeti hii miradi yetu ya maji na shida tulizonazo hebu niambie Waziri tunakwenda wapi? Nikuombe Waziri review bajeti yako, fika mahali sasa Kiteto uionee huruma, kwa jinsi ambavyo tuna shida ya maji muda mrefu, katika ilani yetu ya utekelezaji 2015 - 2020 ni mikoa mitano ambayo ipo kwenye plan na ni mikoa kame ambayo ilikuwa na priority. Mkoa wa kwanza ni Simiyu, Mkoa wa pili ni Dodoma, Mkoa wa tatu ni Singida, Mkoa wa nne Shinyanga na Mkoa wa tano ni Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Manyara leo kwenye bajeti ukiangalia mkoa mzima sisi ni karibu bilioni
7.9 ambayo ni pesa tuliyotengewa. Ukilinganisha na mikoa ambayo bado ina maji na vyanzo vingi vya maji, sasa Mheshimiwa Waziri nikuombe hili nenda nalo, angalia ni namna gani ya kufanya uweze ku-rescue mkoa mzima wa Manyara kwa sababu ya hali nzima kubwa ya upungufu wa maji tulionao kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nmshuruku Mheshimiwa Waziri kwa kututengea pesa kwa ajili ya Mji wa Kibaya, Mji huu ulikuwa ni kame kwa muda mrefu, lakini tuna visima vingi ambavyo vimechimbwa kwa msaada wa jitihada zetu za pesa na ndani kwa maana ya Halmashauri yetu na Mkurugenzi na Baraza letu la Madiwani tumekaa tukapanga tukachimba visima, sasa tunaomba pesa kwa ajli ya ukamilishaji, tunamalizia ili yale maji na zile tenki tulizojenga pale ulipokagua wewe mwenyewe ulivyofika site tuweze kupata namna pesa zinaweza kutusaidia kuhakikisha kwamba zile tanki zinakamlilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, visima vinafungwa pampu maji yanapandishwa pale ulipoona kwenye tanki ili Mji wote wa Kibaya uweze kusambaa maji kwa ajli ya matumizi ya watu wetu kulingana na jinsi ambavyo unaona yale maeneo yetu watu wanaongezeka, ujenzi unaongezeka, lakini na matumizi ya maji yanatakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo shida kubwa muda mrefu sana ambayo imetukabili kwa mazingira yetu ya maji, lakini kumekuwa na miradi mingi ambayo imekuwa inahujumiwa na miradi mingi unakuta tunao mradi wa Matui ambo ulijengwa pale Chapakazi zaidi ya milioni 600 zimetumika lakini wananchi hawapati maji, mradi upo nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapopata nafasi baada ya maswali na majibu tuongozane, twende Chapakazi uone mradi uliogharimu shilingi milioni 600, kodi za Watanzania na wananchi hawapati maji ili uweze kujiridhisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba kwamba lile eneo la Matuhi unalifahamu, kuna zaidi ya watu 20,000 tumekubaliana kwamba kisima cha Nchimila kifungwe pump, kifungwe umeme ili kiweze kusambaza maji. Tumeshakuletea ile plan na feasibility design nzima imeshakuja, Wizarani tunaomba approval ile design iweze kwenda na tupate pesa ili kuhakikisha kwamba tunatandika mabomba wale wananchi zaidi ya 20,000, ikiwemo vituo vya afya makanisa, misikiti na maeneo yote ya makazi na vituo vidogo zaidi ya 40 zimeshakuwa designed waweze kupata maji kwa sababu kunaweza kutokea mlipuko wa magonjwa kipindi kijacho kwa sababu ya upungufu wa maji na shida kubwa ya maji ya watu ambayo wanapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsanta sana.