Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nikupongeze sana kwa Tulia Marathon.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri wanayoiendelea kuifanya kwenye Wizara yao ya Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue hii kuwashukuru kwenye taarifa yake ya kwenye kitabu hiki Singida Mjini walau tumeonekana, ninamshukuru sana. Eneo langu la Irau pale Kisaki limetengewa fedha kama shilingi milioni 900 na kama haitoshi kuna fedha zingine za upanuzi wa miundombinu ya maji kama shilingi bilioni moja, kwa ujumla yake tumepata kama shilingi bilioni tatu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuieleza hofu yangu ya upatikanaji wa fedha hizi, inanitia mashaka kidogo kama fedha hizi zitakuja, kwa sababu bajeti ya mwaka 2016/2017 nilitengewa shilingi bilioni 2.4 fedha hizi hazikuwahi kuonekana mpaka leo. Mheshimiwa Waziri alifika Singida akasema tumetengewa fedha, lakini akiwa bado anachangia Mpango wa Maendeleo hapa Bungeni alitolea mfano wa Singida kwamba tulitengewa fedha na hatukuziomba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kulisema hili kwa sababu katika mazingira ambayo ninayaona Wizara inatenga fedha zinazokwenda Halmashauri na mimi nakwenda kuongea na wananchi wangu kuwaambia tumetengewa fedha za maji zinakuja, lakini fedha haziji na Mkurugenzi anaulizwa anasema hana taarifa ya fedha zinazoletwa na Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii imekuwa kubwa sana ndiyo maana hofu hii naileleza wazi. Lakini nimeendelea kuifuatilia na katika kufuatilia kwangu nimegundua uzembe mkubwa sana unaofanywa na Halmashauri zetu hizi, ukiangalia malalamiko makubwa ya miradi ambayo haitekelezwi kwenye Halmashauri ni miradi ambayo inasimamiwa na TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tuliweke jambo hili wazi, Wizara ya Maji inatenga fedha, lakini fedha zinazokwenda Halmashauri zinasimamiwa na TAMISEMI na TAMISEMI tumekwishamaliza bajeti yao hapa, sasa niiombe Serikali iangalie jambo hili na ninaiomba Idara ya Maji kwenye Halmashauri isibaki kwenye Halmashauri, isimamiwe na Wizara ya Maji na Umwagilaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kutofautisha leo Wizara ya Afya, hospitali za Rufaa za Mikoa zinasimamiwa na Wizara ya Afya, kwa nini Idara za Maji za Halmashauri zisisimamiwe na Wizara ya Maji ili kuweka utaratibu mzuri wa kuweza kulisimamia jambo hili. Eneo hili linatupa mkanganyiko mkubwa sana na TAMISEMI imeshakuwa kubwa, hebu tuipunguzie mzigo yenyewe ibaki kufanya monitoring, suala la maji libaki kwenye eneo la Wizara ya Maji, nimuombe Mheshimiwa Waziri akija alione eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naungana na wenzangu kuomba kuundwe tume ili kuweza kufatilia miradi ya maji ambayo imeshindwa kutekelezeka na mikataba mibovu iliyotengenezwa huko nyuma imefanya wananchi wetu wasipate maji, niombe sana Bunge lako liweze kuliangalia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo fidia ya maji kwenye maeneo yetu, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri alitupatia fedha kwenye Kata yangu ya Mwankoko shilingi 1,500,000,000 lakini bado kuna fedha zingine wananchi wanadai nimuombe ili aweze kutupa hizo fedha. Lakini tunalo eneo la Irao ambalo lipo Kisaki wananchi wanadai fedha ya fidia shilingi bilioni 2.1, bado kule Misaki Mandeo wanadai shilingi milioni 200, jumla ni takribaki shilingi bilioni 2.5 nimuombe Mheshimiwa Waziri hili nalo aliangalie wananchi hao wanahitaji kulipwa fidia ya maji ili iweze kuwasaidia kwa sababu wananchi walikuwa waungwana kupisha vyanzo vya maji tuweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida unakua kwa kasi sana, tunataka tuendane na kasi ya ujenzi wa viwanda. Viwanda haviwezi kujengwa kama hatuna maji ya kutosha, kuendelea kutegemea visima maji yanayochimbwa maana yake hatutafikia malengo. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, ule mkakati wa maji ya kutoka Ziwa Victoria unaokwenda mpaka Simiyu usiishie Simiyu, utoke Simiyu uingie Mkalama, utoke Mkalama uende Kiomboi, uingie Singida DC, uje Singida Mjini, Ikungi, Manyoni na Itigi, Mkoa mzima utakuwa umeweza kuingia kwenye mtandao wa maji wa Ziwa Victoria. Ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri eneo hili ni muhimu mno hatuwezi kuendelea kutegemea visima peke yake tukawa na viwanda vya kutosha, watusaidie wasiishie Simiyu waje moja kwa moja mpaka Mkoa wa Singida na wote tutaweza kuendana na kasi hi ya ujenzi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Manispaa ya Singida inakua kwa kasi mnoo, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu lakini kama haitoshi watu wanajenga kwa kasi kubwa lakini miundombinu ya maji taka haiwezi kutosheleza mazingira tuliyonayo. Wameshafanya feasibility study kwenye eneo la Manispaa, tunahitaji fedha ili kuweza kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya maji taka. Eneo hili litatusadia sana, tukiacha hivi ilivyo tutakuwa na mazingira magumu sana ya kesho kuendelea ku-solve tatizo hili kwa kutumia magari ya maji taka. Pale Singida hatuhitaji magari ya maji taka, tunahitaji kuhakikisha kwamba kuna miundombinu rafiki kwa ajili ya kuondoa majitaka yale na kwenda kwenye Maziwa yetu tunayo mabwawa mawili pale ya Singidani na Kindai. Ni lazima Serikali ije na mkakati wa uvunaji wa maji, hatuwezi kuendelea kutegemea visima kama nilivyosema awali na Singida tunalo eneo ambao tulikwisha lipanga kwenye master plan yetu, eneo hili linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kushirikiana na Wizara hii, lile eneo tulilolitenga maalum eneo lile tuweze kupewa kwa ajili ya kuchimba bwawa ili tuweze kuyavuna maji haya. Itatusaidiasana kupunguza tatizo la maji katika Jimbo la Singida Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wenzangu kwamba lazima kuwe na Wakala wa Maji Mijini na Vijijini, lakini walio wengi wanazungumza Wakala wa Maji Vijijini, hapana! Tuzungumze Wakala wa Maji Mijini na Vijijini. Tumefanya kosa kwenye REA, tumezungumza Wakala wa Umeme Vijijini peke yake na leo wa Mjini tunahangaika na suala la umeme. Sasa tuzungumzie Wakala wa Maji Mjini na Vijijini, tukiliweka hivi maana yake tutaondoa shaka tunaoishi Mjini. Ninamuombe Mheshimiwa Waziri aliweke kwenye mazingira hayo, litatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza wenzangu kuhusu nyongeza ya shilingi 50 kwenye lita ya mafuta ya petroli na dizeli nami nataka niwaunge mkono, ukifanya hesabu ya haraka unaongeza kwenye bajeti hiyo isiyopungua bilioni 160, siyo fedha ndogo. Niwaombe sana Wabunge wenzangu na niiombe Serikali ione umuhimu huu wa kuweza kuweka nyongeza hii. Tutaondokana na tatizo la maji kwenye mazingira haya ambayo yanatukabili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nichukue fursa hii kuunga mkono bajeti na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, ama hakika kitabu hiki walimu tuliozoea kusoma kitabu hiki kina mikakati ya kutosha na kitabu hiki kinajitosheleza. Tukiweza kukisoma vizuri nadhani tutatumia muda wetu mzuri kuweza kutatua matatizo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.