Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kuna kitu kimoja bado sijakielewa vizuri. Serikali hii wanatuambia kwamba wanakusanya makusanyo yanapita mpaka lengo kwa mwezi, lakini cha kushangaza kwenye bajeti ya maji inaenda asilimia 22, sasa hizo hela zinazokusanywa zinakwenda wapi? Mtakapokuja kuhitimisha Waziri wa Fedha atueleze, wanatudanganya hawakusanyi ama wanakusanya lakini pesa zinatumika nje ya bajeti tunazopitisha hapa Bungeni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tupate ufafanuzi huo, asilimia 22 kwenye utekelezaji wa mambo ya msingi, mambo ya maji ni jambo la aibu, la kusikitisha na linalokatisha tamaa wananchi wa Tanzania. Ukiangalia kwenye Ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017 ukurasa wa 99 hadi 100 inaonekana kuna pesa shilingi bilioni 410 zilikusanywa na TRA ikiwepo pesa kwa ajili ya usambazaji wa maji, lakini kuna pesa haikutolewa kwenda kule inakotakiwa kwa ajili ya kusambaza maji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Mkoa wa Mtwara, tuna tatizo kubwa la maji katika sehemu mbalimbali. Ukienda maeneo ya Newala Mjini, Newala Vijijini, Nanyamba ukiingia huko ndani Mtwara Vijijini, Mtwara Mjini kwenye kata za pembezoni kuna tatizo kubwa la maji; wale watu wanafikia wananunua mpaka dumu moja la lita 20 shilingi 1,000, shilingi 800, shilingi 500; lakini wale watu wa Mtwara kila siku nasema wanachangia pato kubwa la nchi hii kupitia kilimo cha korosho ingawa nako pia kuwalipa hawalipwi kwa wakati lakini wanachangia. Kwa nini hatukai tukaangalia suala la maji likawa ni suala la kipaumbele? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nipate ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha kuhusu ule mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kuja Mtwara Mjini ambao tunaamini ungefanyiwa utekelezaji wake ungesaidia kwa kiasi kikubwa pale bomba lilipotaka kupita. Mwaka jana tumeona pesa zimetengwa tunaambiwa kuna processes zinaendelea, hizo processes zitaisha lini? Sisi tunachotamani tuone maji safi ya baridi yanapatikana ambayo hayo maji pia yangeenda kusaidia katika uwekezaji wa viwanda ambao mnausisitiza lakini tuna tatizo kubwa la maji katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji ni suala mtambuka. Tukikosa maji ya uhakika maana yake magonjwa yatakuwa mengi, hata kama Serikali itakuwa inatoa fedha nyingi kwa ajili ya dawa lakini tukumbuke bajeti ya dawa itakuwa kubwa kwa sababu ya matumizi ya maji ambayo siyo safi na salama. Nasema pia ni suala mtambuka kwa sababu mama anapoamka asubuhi kwenda kutafuta maji kule anakumbana na vikwazo vingi, anaweza akabakwa, akibakwa kesho mnamuita tupime DNA, mnapimaje DNA wakati ninyi ndio mliosababisha hayo yote yanayotokea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusifanye vitu kwa ajili ya kutaka kujionesha, twendeni tutoe hela. Kama hela zinakusanywa kupita kiwango hizo hela zinakwenda wapi? Watu wakihoji hapa kwamba kuna hela shilingi 1.5 trillion zimepotea watu mnakasirika, lakini mnasema mnakusanya, kwenye maji haziendi, kuziona hatuzioni. Tunataka tupate majibu ya uhakika ili tujue mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ungeniuliza mimi kipaumbele ningekwambia maji ni kipaumbele kwa sababu ni mtambuka. Kama huna maji kiwanda hakifanyi kazi, kama huna maji hata hiyo ndege hauwezi kupanda kwa sababu hautakuwa na afya nzuri, unaumwa na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina mengi ya kuyasema lakini tunaomba tupate kueleweshwa, nakushukuru.