Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia leo kupata fursa hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Maji, sote tunafahamu umuhimu wa Wizara hii kwamba maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu, naomba nimshukuru sana Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Ukiangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 126 na 127, wameeleza miradi mbalimbali ambayo itatekelezwa katika Mkoa wetu wa Ruvuma. Naomba niipongeze sana Serikali wametutengea shilingi 15,393,653,000, ni mkoa wa kwanza katika kutengewa pesa. Naomba sana niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niseme kutenga pesa ni hatua moja lakini kupeleka pesa katika miradi ni hatua nyingine. Niombe wakati utakapofika tupeleke hizi pesa ili kuhakikisha miradi ambayo tumekusudia kuitekeleza inatekelezwa. Miradi ambayo imepangwa kutekelezwa katika Mkoa wangu wa Ruvuma ni katika Wilaya za Madaba DC, Mbinga, Mbinga Mji, Namtumbo, Nyasa, Songea, Songea Manispaa na Tunduru. Kwa hiyo, naishukuru Serikali na niombe sana kwamba wakati utakapofika Mheshimiwa Waziri kama vile ambavyo umetuweka namba moja katika kututengea pesa nyingi basi ni vizuri katika utekelezaji vilevile tuwe namba moja katika kupeleka pesa.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spka, naomba pia nizungumzie Miradi ya Benki ya Dunia ambayo ilitakiwa itekelezwe katika Vijiji vya Mchoteka, Nakapanya, Majimaji na Muwesi. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri anakumbuka hicho kitu kwamba miongoni mwa vijiji ambavyo viliwekwa kwenye mpango wa utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Benki ya Dunia ni pamoja na hivyo vijiji ambavyo nimevisema. Niliwahi kusimama katika Bunge hili kuvizungumzia vijiji hivyo na Waziri alitoa majibu kwamba vijiji vile vimekosa vyanzo. Niombe, tafadhali Mheshimiwa Waziri naomba niseme kwamba vyanzo kule bado vipo. Ni vizuri sasa twende tukatekeleze katika kuona tunatafuta vile vyanzo vya maji kata hizi ambazo tunazifikiria kupata maji zipatiwe maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie tena suala la fidia Bonde la Mto Luhila - Songea. Mheshimiwa Waziri ninapozungumzia Bonde la Mto Luhila - Songea naamini utakuwa unakumbuka kwamba wananchi walipisha pale mradi mkubwa wa maji na hivi ninavyozungumza kiasi cha pesa karibu shilingi bilioni 1.9 wananchi wale wanadai. Imekuwa kero kwa sababu wananchi wale walikuwa wasikivu, walipisha huu mradi mkubwa, lakini mpaka hivi navyozungumza wananchi karibu 803 hawajapatiwa pesa zao. Nikuombe Mheshimiwa Waziri wakati utakapofika uhakikishe tunalipa fidia kwa wananchi wale ambao walijitolea kupisha mradi huu mkubwa wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie upatikanaji wa maji katika Miji Midogo ukiweno Miji ya Namtumbo na Lusewa. Naomba nizungumzie sana Lusewa hata ukija katika Kata ile ya Lusewa kuna kituo cha afya ambacho hakina maji. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, naamini bado mwanya upo, utufikirie katika kituo chetu cha Lusewa kutupatia maji. Tunapozungumza maji kama walivyosema Wabunge wenzangu sisi akina mama, watoto ndiyo hasa tunaathirika katika suala hili la maji. Tunapokuwa na kituo cha afya ambacho hakina huduma ya maji ni mtihani mkubwa sana. Nikuombe tufikirie sisi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na hususani wale wananchi waliopo katika Kata ile ya Lusewa wakati utakapofika ili tupate mradi wa maji katika Kijiji kile cha Lusewa. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.