Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba nitoe pongezi zangu za dhati kwa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya ya kutatua tatizo la maji hapa nchini. Natambua na sote tunatambua kwamba wakati tumepata uhuru na baadae, nchi yetu ilikuwa na watu wachache, sasa hivi watu ni wengi sana na kila mwananchi ana mahitaji makubwa ya maji. Kwa jinsi hiyo, bado maji ni tatizo kwa wananchi wengi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo Serikali imefanya juhudi kubwa na ya dhati kabisa kuweza kutatua matatizo ya maji katika maeneo kadhaa ya Taifa letu. Hakuna mtu ambaye anaweza kutatua tatizo hili kwa wakati mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, alianza Baba wa Taifa akafanya kazi yake, akaja Mzee Mwinyi akafanya kazi yake, akaja Mzee Mkapa akafanya kazi hiyo, akaja Mheshimiwa Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, mume wangu akafanya kazi yake na sasa hivi yuko Dkt. John Pombe Magufuli anafanya kazi yake na ataiacha hii na bado kazi itaendelea. Tunaamini Serikali ina dhamira ya dhati kabisa kuondoa tatizo la maji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo sasa naomba nielekee kwenye eneo langu ambalo nalifanyia kazi kule Lindi. Naipongeza na kuishukuru sana Serikali kwa mradi mkubwa kwa mabilioni ya pesa ambao walitupatia na hatimaye leo hii wananchi wa Wilaya ya Lindi Mjini wanapata maji. Tatizo kubwa lililopo hapa pamoja na kupata yale maji, kuna tatizo dogo siyo kubwa sana, naamini wataalam wakikaa, aidha, Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Nishati wanaweza kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa la kukatikakatika kwa umeme ndiyo linasababisha pump zisiweze kupeleka maji kwenye matenki hatimaye maji yale yakapelekwa kwenye maeneo husika. Naomba Wizara hizi mbili zikae kwa pamoja ili waweze kutatua tatizo hili ambalo linawakabili wananchi wa Wilaya ya Lindi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Serikali kwa dhati kabisa kwa kutupa fedha kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi mikubwa miwili; ujenzi wa miundombinu ya maji safi katika eneo la Ng’apa na Mitwero. Fedha hizi au miradi hii itasaidia kuondoa changamoto ya maji kwenye maeneo hayo niliyoyataja. Unaweza ukaangalia ukurasa wa 188 jinsi ambavyo Serikali imeweza kutuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka niende kwenye eneo la umwagiliaji. Tunajua na tunatambua kwamba kupanga ni kuchagua, na eneo hili ni muhimu sana kwa usalama wa chakula hapa nchini. Mwananchi yoyote pamoja na kuhitaji maji anahitaji kula. Tukiangalia eneo la umwagiliaji ni eneo ambalo lina uhakika wa kutupatia chakula hapa nchini. Kwa mfano takwimu zinaonesha kwamba hekta 475,520 sawa na asilimia 24. Asilimia 24 hii inachangia chakula kinachopatikana hapa nchini. Sasa kama tukiongeza mara mbili yake ina maana kwamba tutakuwa na asilimia 48 na asilimia hizi 48 zitatuongezea kiasi kikubwa cha upatikanaji wa chakula hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Upotevu wa Maji. Tunaamini na tunajua kwamba maji mengi yanapotea. Sasa katika hili ni lazima Serikali ichukue hatua makini zaidi kuweza kuthibiti hayo maji. Lakini hasa kule majumbani, maji mengi yanapotea; tuwe makini kuwaambia vijana wetu maji haya yasipotee. Wakati mwingine kikombe moja kinatumia maji zaidi ya lita tatu au lita nne kusafishia. Hii haikubaliki na hili haliwezekani ni lazima tuwe makini katika udhibiti wa maji yetu haya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naona muda umenitupa mkono, lakini naomba kuunga hoja hii kwa asilimia 100, ahsante sana.