Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara, hakika wanatenda kazi, hatuna shaka nao katika utendaji wao wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ya Wizara hii tunafahamu kwamba ni pesa, lakini mimi naiomba sana Serikali, hapa naiambia moja kwa moja Serikali, hizi pesa ambazo tumezitenga kwa ajili ya Wizara hii naiomba Serikali ihakikishe kwamba inazipeleka kadri zinavyopatikana na ikiwezekana zipatikane kwa asilimia mia moja, kwa sababu kama wanavyosema watu maji ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa sababu katika bajeti hii, kabla ya hapo nilikaa na Mheshimiwa Waziri nikamueleza tatizo kubwa la bwawa letu kule katika Kijiji cha Namasogo na tatizo la mfumo wa maji taka pale Mangaka mjini. Nashukuru katika bajeti hii nimetengewa shilingi milioni 400 katika Bwawa la Namasogo, lakini pia shilingi milioni 500 kwa ajili ya mfumo wa maji taka pale mjini Mangaka kwa kweli nawashukuru sana kwa hiki, kidogo ambacho tumeanza nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Katika bajeti hii pia tumetengewa pesa zaidi ya shilingi milioni 1300 kwa ajili ya maji vijijini. Basi hizi pesa nalihakikishia Bunge lako tukufu tutakwenda kuzisimamia, mimi pamoja na Madiwani wenzangu kule tukiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri kuhakikisha kwamba lengo la Serikali linatimia. Kwa sababu kama Diwani nina jukumu la kusimamia pesa hizi ili zifanye kazi tarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa Wilaya ambazo zinashida kubwa sana ya maji katika nchi hii ni pamoja na Nanyumbu. Kwa hiyo, ninaomba sana Serikali katika bajeti zingine iangalie wilaya gani zina tatizo kubwa katika mgawanyo wa hizi pesa ili tuweze kufanana katika kutatua tatizo kubwa la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma mpaka Mjini Mangaka. Serikali ilikuwa imeshandaa utaratibu wa kuyatoa maji kutoka Mto Ruvuma na kufikisha katika makao makuu ya Wilaya pale mjini Mangaka. Hatua tuliyokuwa nayo ni ya usanifu wa kina na kuandaa makabrasha kwa ajili ya kutangaza zabuni. Sasa niiombe Serikali, kwanza speed ya upembuzi yakinifu iwe kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda hautusubiri lakini wananchi wanatusubiri. Kwa hiyo nashauri sana hawa watu tuliowapa hili jukumu wafanye kazi kwa speed ili wananchi waone matokeo ya sisi kuwa viongozi wao katika awamu hii ya tano.

Kwa hiyo nashauri sana Wizara isituangushe katika utendaji wa kazi ili maji kutoka Mto Ruvuma yafike pale mjini Mangaka. Lakini nilishaomba na tena naomba yale maji upembuzi yakinifu uelekee hadi Lumesule kupitia Michiga na Likokona. Vilevile tufike pia Nagomba, Mikangaula, na Mpakani mwa Wilaya yetu na Masasi pale Namatumbusi. Tukifikisha maeneo hayo nia uhakika kwamba tumesaidia eneo kubwa la Wilaya ya Nanyumbu kupambana na shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya kwa sababu muda wangu ni mdogo sana, basi naunga mkono hoja, nashukuru, ahsante sana.