Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha kuchangia Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai wa binadamu, wanyama na kilimo na kila kilichoumbwa. Bajeti ya Wizara hii ni ndogo mno kwa sababu maji katika nchi hii ni tatizo kubwa na ndoa zinakatika kwa ajili ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wakati wa kampeni yake na baada ya kushika madaraka alisema atahakikisha kuwa anamtua mama ndoo kichwani, lakini bado tatizo liko pale pale, bado ndoo iko kichwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatenga fedha za miradi, lakini inachelewesha kuzifikisha fedha katika Halmashauri na utakuta utekelezaji wa mradi unakwama na kuchukua muda mrefu.Vilevile wakandarasi ni lazima wasimamiwe kikamilifu kwa sababu wananunua mabomba yaliyokuwa hayana viwango. Utakuta muda mdogo yanapasuka na kusababisha maji kupotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wako wakandarasi ambao hawana utalaam wa kutosha, wanachimba visima virefu lakini maji hayapatikani na baadae kufeli na kusababisha kuitia hasara Serikali na mradi kusimama, hili ni tatizo. Tunaomba watendaji waache kukaa ofisini, wafike kwenye miradi kuisimamia ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile fedha zitengwe kwa ajili ya kujengwa mabwawa ya kuhifadhia maji ya mvua ili kupunguzia wananchi tatizo la mifugo yao hasa wakati wa kiangazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasomaji wa mita wana matatizo, hawasomi mita vizuri na wanawabambikia madeni makubwa wananchi ambao wanashindwa kulipa baadae wanawakatia maji na kupata usumbufu mkubwa.
Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha shule zote nchini zimepata maji ili kuwaondoshea usumbufu watoto wetu hawa wasichana pale wanapokuwa kwenye siku zao waendelee na masomo yao waondokane na kubakia nyumbani?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu naomba kuwasilisha na kabla sijawasilisha, nauliza; ikiwa hatuna maji ya kutosha hivyo viwanda vitafanyakazi vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasiliaha.