Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa afya njema Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Engineer Isack Aloyce Kamwelwe (Mbunge), pamoja na Naibu Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mbunge). Pia nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii.

Kutokana na upatikanaji wa visima virefu maeneo ya Kimbiji, Dar es Salaam hivyo naishauri Serikali katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 itenge fedha kwa ajili ya kusambaza maji hayo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam. Wakulima wengi wa mboga mboga Mkoani Dar es Salaam wanatumia maji ambayo si safi na si salama kwa umwagiliaji. Hivyo naishauri Serikali iwawezeshe wakulima hao wachimbe visima virefu kwa ajili ya kupata maji safi na salama ya kumwagilia mboga zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali isimamie vya kutosha malalamiko ya wananchi wanaobambikiziwa bili hewa za maji ili haki iweze kutendeka. Naishauri Serikali iboreshe miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam katika maji taka. Kwa kuwa wakati wa mvua septic tanks zinafumuka na kumwaga maji machafu yenye vinyesi ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, mfano katika Milima ya Uluguru, Morogoro. Naishauri Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu jinsi ya kuvuna maji ya mvua na jinsi ya kuyahifadhi kwa sababu wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iweke chujio la maji madhubuti katika Bwawa la Mindu lililopo Mkoani Morogoro kwa kuwa wakati mwingine maji huwa na uchafu wa rangi ya kijani. Pia yawekewe dawa ya kusafisha maji kwa sababu wakati mwingine yanakuwa na harufu ya samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji zipelekwe kwa wakati katika eneo husika ili kuweza kuondoa matatizo ya upatikanaji wa maji katika nchi yetu. Naishauri Serikali wakandarasi ambao wameonesha kiwango cha chini cha utekelezaji wa miradi ya maji wachukuliwe hatua za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nawatakia afya njema na umri mrefu ili kuyatekeleza majukumu yenu ya kila siku.