Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha kufika mahali hapa na mimi niweze kuchangia hoja hii muhimu iliyopo mbele yetu. Bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2018/2019 inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kutimiza yale yote iliyoyaanisha katika Ilani hasa kukamilisha miradi yote iliyopo katika sekta ya maji na umwagiliaji. Naipongeza Wizara kwa kuandaa bajeti nzuri inayokwenda kuleta mapinduzi makubwa kwa kutatua kero zinazowakumba wananchi wetu hasa katika sekta ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya maji nchini imekuwa kubwa sana, Wabunge wote humu Bungeni tunakabiliana na changamoto hiyo nchi nzima ingawa Serikali imeendelea kuweka nguvu kubwa katika sekta ya maji, lakini bado suala la upatikanaji wa maji sehemu mbalimbali za nchi hasa vijijini imekuwa changamoto kubwa sana, kujenga na kupanua miradi mbalimbali ya maji vijijini itasaidia sana kukabiliana na changamoto hiyo, miradi 71 iliyokamilika bado ni idadi ndogo sana ukilinganisha na miradi inayoendelea kutekelezwa takribani miradi 366.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuiweka sekta ya maji katika vipaumbele vyake kwani inawagusa watu wetu wa hali duni hasa vijijini ndiyo wanaohangaika kukesha kusaka maji usiku kucha na kuacha kufanya shughuli za kiuchumi na kimaendeleo. Naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazoendelea nazo katika mipango yake ya kuhakikisha kwa mwaka huu 2018/2019 kukamilisha miradi yake ya maji ipatayo 387 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na pia kuanza miradi mipya ya maji vijijini, ni jambo jema na lazima tulisemee kwa namna ya kupongeza na kuipa moyo Serikali kwa kuonyesha inatambua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi sana katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu kwa kasi ya hali ya juu, lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali katika safari hiyo ya maendeleo. Changamoto hizo zimenigusa mimi pamoja na wananchi wangu wa Kibaha Vijijini, kwa muda mrefu sasa tunaendelea kukabiliana na changamoto hiyo kwa muda mrefu sasa. Miradi ya maji ambayo ndiyo ingewakamua wananchi hawa kwa kupata maji safi nayo haikukamilika kwa wakati na ikizingatiwa chanzo cha maji kipo katika eneo lao na wao wamekuwa walinzi wazuri wa chanzo hicho ili kuepuka uharibifu wa aina yoyote unaoweza kutokea na kuleta athari kwa watumiaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wamekuwa wakishuhudia maji yakipita na kwenda maeneo ambayo yamekuwa sugu kwa changamoto ya maji ni Magindu, Gwata, Kipangege, Mwanabwito na Kisabi. Naomba katika bajeti hii kupewa kipaumbele katika sekta ya maji hasa katika miradi ya maji maeneo husika ili iweze kukamilika kwa wakati, na kwenye baadhi ya miradi ambayo ina changamoto ya kusimama kufanya kazi kutokana na kuharibika miundombinu yake basi nayo ipewe kipaumbele kwa kufanyiwa ukarabati wa haraka ili huduma iweze kurejea kwa wananchi, hii itasaidia kwa utekelezaji wa miradi ya maji ili wananchi waondokane na kadhia hiyo ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuja na mkakati kabambe ikishirikiana na Wizara ya Kilimo ambao utakwenda kuanzisha utaratibu maalum wa kutoa elimu kwa wananchi hasa wakulima ili kuondokana na kilimo kilichopitwa na wakati na kuja na kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ili kuwawezesha wananchi kuweza kufanya kilimo cha umwagiliaji nchini. Ushirikiano huo wa hizi Wizara mbili utaleta mabadiliko makubwa hasa katika sekta hizi husika. Naunga mkono hoja.