Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa uhai wa afya mpaka leo nipo humu Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitakuwa na uchoyo wa fadhili pasipo kuwapongeza watendaji wa Wizara ya Maji wakiongozwa na Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Naibu Waziri Juma Aweso, Katibu wa Wizara - Kitila Mkumbo na wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichukue fursa hii ya kuchangia kwa maandishi katika hotuba ya Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kuwa maji ni muhimu kwa binadamu, wanyama na mimea, lakini pia maji ni chanzo cha uchumi kwa nchi yetu kwani bila maji umeme haupatikani, bila maji barabara hazitengenezwi, bila maji mitambo haifanyi kazi, bila maji vyakula havipikwi, bila maji operation hazifanyiki katika hospitali. Hivyo naomba maji yapewe kipaumbele cha hali ya juu na kupelekewa fedha zinazotosheleza na zifike kwa wakati kwani ripoti ya Wizara na ya Kamati zinaonesha ni asilimia 22 tu ya fedha zinazoidhinishwa ndiyo zinakwenda kwenye maji. Naomba sana pesa zinazoidhinishwa ziwe zinakwenda kama zilivyoombwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa miradi ya maji; Mkoa wa Tabora umebahatika kuwemo kwenye mikoa itakayopata maji toka Ziwa Victoria, lakini mradi huu utachukua muda mrefu mpaka kukamilika, hivyo tunaiomba Serikali ituwezeshe wananchi wa Tabora tupate vyanzo mbadala vya maji hususani Manispaa ya Tabora ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikipata vyanzo vya maji toka Bwawa la Igombe na Kazima ambapo mabwawa hayo kwa mujibu wa taarifa ya engineer wa maji ni kwamba yame- expire hivyo inapofika wakati wa kiangazi hukauka na kufikia kutoa tope badala ya maji na kuwasababishia adha kubwa wakazi wa Tabora Manispaa kukosa maji kwa muda mrefu na pia kulipuka kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na watumiaji wengi kutumia maji yasiyo safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Manispaa ya Tabora wamekuwa wakikumbwa na adha kubwa ya bili ya maji ambapo inawapasa walipe bili kubwa kinyume na matumizi ya maji wanayotumia. Hivyo tunaiomba Serikali kuwa na mita nzuri na wasoma mita wenye weledi kwani wamekuwa wakiwabambikia bili kubwa tofauti na maji wanayotumia. Lakini pia tunaiomba Serikali iwatolee wateja wa maji service charge kwani wanalipa bili kama kawaida, kufanya hivyo kutawasaidia wananchi hususani kina mama kuingiza maji kwenye majumba yao na hivyo kuiongezea Serikali mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, kumekuwa na tabia ya wakazi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji kufanya shughuli mbalimbali za uchumi kama vile kilimo cha bustani hali inayosababisha vyanzo hivyo kuwa katika hatari ya kukauka. Hivyo niombe Serikali iweke sheria kali na kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wale wote watakobainika kuharibu vyanzo vya maji ili viweze kutumika kwa muda mrefu. Pia naomba vyanzo hivyo vitunzwe kwani pasipofanyika hivyo, kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani haitafainikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upoteaji hovyo wa maji, maji yamekuwa yakipotea hovyo hivyo kwenye vyanzo vya maji au kwenye mabomba baada ya kukatika na hivyo maji kupotea au kusambaa njiani kabla ya kuwafikia watumiaji wa mwisho na hivyo kuwafanya wakose maji mara kwa mara.
Hivyo naomba Serikali iweke mikakati ya kuzuia upoteaji wa maji na pia kuwawajibisha wale wote wanaokata mabomba makusudi ili wajinufaishe au wapate maji bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha.