Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Josephine Tabitha Chagulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kuniwezesha kuwa hapa Bungeni leo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Nimpongeze Waziri na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama lakini bado kunahitajika jitihada za ziada katika suala hili la maji. Naishauri Serikali ili suala hili la maji liende vizuri iweke ukomo kama ilivyoweka TANESCO kwamba ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote vitapata umeme. Kwa hiyo, Wizara ya Maji nayo itamke muda rasmi wa kumaliza tatizo la maji kwa vijiji vyote nchini, hii itasaidia miradi kukamilika kwa wakati.

Kuna mradi wa maji katika Wilaya ya Nyang’hwale leo ni mwaka wa sita tangu uanzishwe, wananchi wanateseka na haijulikani lini watapata maji. Niiombe sana Serikali iweze kumaliza mradi huu wa maji ili wananchi wa Nyang’hwale wapate maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya maji katika Mji wa Geita na vitongoji vyake ni makubwa sana ukilinganisha na maji tunayoyapata, mahitaji halisi ni lita 15,000,000 kwa siku lakini tunayopata ni lita 4,000,000. Kwa hiyo, kuna upungufu wa lita 11,000,000 kwa siku sawa na asilimia 29 ya maji tunayopata. Niiombe sana Serikali iongeze uwezo wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Viktoria ili tuweze kupata maji ya kutosha kulingana na mahitaji yetu ya maji kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa uchimbaji visima virefu 16 katika Halmashauri ya Mji katika vijiji 16 tofauti tofauti ambapo mpaka sasa mkandarasi amechimba visima vyote 16 na visima saba tu ndiyo vimefanikiwa kupata maji. Pamoja na vyanzo hivyo kuchangia kiwango hicho cha maji lakini bado huduma ya maji ni changamoto. Hivyo tunaiomba Wizara kuchukua hatua za makusudi katika kuhakikisha upanuzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria unafanyika ili kukidhi mahitaji ya maji kwa siku katika Mji wa Geita na vitongoji vyake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa katika Idara ya Maji Geita nayo ni kukosa usafiri kwa ajili ya kufuatilia miradi ya maji iliyopo pembezoni mwa halmashauri. Tunaomba tupatiwe gari kwa ajili ya watendaji wetu ili waweze kumudu vizuri shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.