Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu Kitila na watendaji wake. Mnyonge nyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Waziri na timu yake inafanya kazi kubwa sana kuhakikisha wanamtua mwanamke ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa walilokumbana nalo Wizara hii ni ukosefu wa fedha za kutekeleza bajeti za Wizara tunazopitisha. Natambua kuna fedha tulitakiwa kupokea mkopo wa dola za Kimarekani bilioni 500 toka Exim Bank ya India ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini. Tatizo kubwa ni Wizara ya Fedha kuwataka walipie VAT mkopo huo. Tuombe sheria iletwe ili kumpa mamlaka Waziri wa Fedha kutoa msamaha wa kodi ili tupokee mkopo huo kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji. Sambamba na hili tuongeze tozo ya shilingi 50 ili ifike shilingi 100 kuwezesha miradi mbalimbali ya maji kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie upande wa miradi ya maji Jimboni kwangu, moja ni Mradi wa Kalya. Naishukuru sana tena sana Serikali kwa kuuwezesha mradi wa maji wa Kalya kukamilika kwa asilimia 95 na tayari maji yanatoka. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kuongezewa pesa ili maji haya yanayotoka katika Vijiji vya Tambisho na Kalya yaende hadi Kijiji cha Kashaguru. Pia nimuombe Waziri yeye binafsi tuambatane hadi Kalya kuona jitihada kubwa sana za Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mradi wa Rukoma, nitoe masikitiko yangu kwenye mradi huu kwani tenki limejengwa lakini takribani miaka minne sasa hakuna chochote kinachoendelea. Tumeomba zaidi ya mara 20 mradi huu na wa Kandaga kuhamishiwa utekelezaji wake kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, lakini hadi leo Halmashauri ya Kigoma Vijijini wamegoma kuileta miradi hii Halmashauri ya Uvinza. Tatizo kubwa ni Mhandisi wa Maji Mkoa kwani anatambua fika hii miradi iko kwenye Hamashauri ya Wilaya ya Uvinza. Pamoja na barua za Wizara kuelekeza miradi hii irudi Uvinza lakini yeye amekuwa ni sehemu ya kukwamisha Halmashauri ya Kigoma Vijijini kutoukabidhi Halmashauri ya Uvinza. Nimuombe Waziri wakati akija Kalya tupite na kukagua miradi hii miwili ya Rukoma na Kandaga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ilagala; kutokana na ukaribu wa kutoka Ilagala kwenda Mwakizega naomba Wizara itufikirie kuongeza mtandao wa maji kuelekea Vijiji vya Kabeba na Mwakizega.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Uvinza unaenda vizuri. Tunaiomba Serikali kuleta fedha kwa wakati ili mradi huu ukamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Nguruka ulikuwa ukamilike tangu Desemba, 2017 lakini bado haujakamilika. Najua kuwa tuliomba Mheshimiwa Waziri utuongezee mtandao wa maji toka Nguruka hadi Miyabibi. Tunaishukuru Serikali kwa kukubali ombi letu la kupatiwa maji Kijiji cha Miyabibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni vijiji vya Bweru na Itabula. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa vijiji hivi viwili vya Bweru na Itabula vipate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri atuangalie kwenye visima hali ni mbaya sana Halmashauri yetu ya Uvinza. Sambamba na hili tuombe suala la bomba la Maragalasi kuwa ni kitovu cha kilimo cha umwagiliaji. Nataka kujua kwa nini huu Mradi wa Kitaifa wa Ziwa Tanganyika usiwanufaishe na wananchi wa Vijiji vya Kalilani, Lufubu, Mgambo, Katumbi, Sigunga, Herembe, Igalula, Kaparamsenga, Kanawena, Kahama, Mkonkwa, Lyabusanda, Msiezi, Sunuka, Karago na kadhalika ili wananchi wanaoishi kando ya Ziwa Tanganyika wanufaike na mradi huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya niendelee kuwapa pongezi Wizara hii kwa utendaji wao mzuri. Ili utendaji huu mzuri uendelee lazima Serikali iwe inapeleka fedha za miradi ya maendeleo tunazopitisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja.