Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumpongeza Waziri wa Maji, Mheshimiwa Engineer Isack Kamwelwe; Naibu Waziri, Mheshimiwa Aweso na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri ya kuwasilisha bajeti hapa Bungeni. Wizara hii ni muhimu sana, lakini bado Serikali haijaweza kuleta pesa ya kutosha katika miradi ya maji nchini. Kuna mtiririko wa fedha za miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge hazipelekwi kwa wakati katika miradi yake. Nikiwa mmoja wa Mjumbe wa Kamati hii, naomba Serikali izingatie sana maoni ya Kamati na ifanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Kamati ya Bunge na Wabunge wote waliopendekeza kuwa kuwepo na ongezeko la tozo ya shilingi 50 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli ili kutunisha Mfuko wa Maji kama ilivyo kwa miradi ya barabara na umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa Serikali ikaanzisha Wakala wa Maji Vijijini kama ilivyo Wakala wa Umeme na TARURA. Hii inasaidia kwa haraka miradi iliyopo vijijini, sababu ndiko kwenye matatizo makubwa sana ya maji kuliko mijini. Pia tumeona jinsi hizo Wakala nyingine zilivyoweza kutekeleza kwa haraka na eneo kubwa, toka kuanzishwa kwake, ndiyo maana tunapendekeza kiundwe chombo hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya umwagiliaji ndiyo mkombozi wa maendeleo ya nchi nyingi duniani. Tunatambua kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inahimiza umuhimu wa kuendeleza eneo kubwa lililopo nchini linalofaa kwa umwagiliaji kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo, kwenye maeneo ya chakula, biashara, malisho na kilimo cha majani. Halmashauri nyingi sana zikiwemo Halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Iringa, zinajenga miradi ya umwagiliaji kwa kuanza na kutumia pesa za Halmashauri. Miradi mingi sana inachelewa kukamilika kutokana na ucheleweshwaji wa pesa za miradi hiyo toka Serikalini (Wizarani).

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wingi wa miradi hiyo, nilikuwa napenda kujua, je, Serikali huwa inatumia vigezo gani kupeleka pesa hiyo katika miradi ya umwagiliaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Meneja wa IRUWASA katika Mkoa wetu wa Iringa, amekuwa akisimamia miradi vizuri sana na kusababisha upatikanaji wa maji katika Manispaa ni asilimia 96. Tatizo lililopo ni mji kupanuliwa kwa haraka sana na Mkoa unahitaji sasa kupata mabomba makubwa ya kusambaza maji katika maeneo yote kwa wakati, kwa sababu yaliyopo sasa hivi hayatoshelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri alipotembelea katika Mkoa wetu, kwani alitoa semina ambayo alitujengea uwezo mzuri sana wa kufuatilia pesa za miradi ya umwagiliaji. Pia uamuzi wa IRUWASA kusimamia miradi ya Mkoa wa Iringa ni la busara sana. Pia naipongeze Serikali kwa kusaini pesa za mradi mdogo wa maji Ilula, Jimbo la Kilolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na changamoto kubwa sana ya usambazaji maji safi na salama na hasa kulikuwa na yale mabomba ya Mchina ambayo yalikuwa ni tatizo. Nawapongeza angalau kwa sasa wameweza kujitahidi kwa kiasi kikubwa sana kuweza kusambaza maji hata maeneo mengi. Pia nampongeza sana Meneja wa DAWASCO lakini naomba kasi iongezeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana katika shule zetu za msingi na sekondari hasa kuhusiana na elimu bure. Hakuna michango yoyote inayotolewa shuleni kwa ajili ya tozo za maji na umeme. Hivyo kufanya shule nyingi kukatiwa maji na kusababisha mlipuko wa magonjwa na watoto wetu kusoma katika mazingira magumu sana. Hivyo, naiomba Serikali jambo hili ilipime na ichukue maamuzi kama ilivyo kutoa elimu bure na tozo za maji ziondolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wananchi juu ya uvunaji wa maji? Kwa sababu kumekuwa na kipindi kirefu cha mvua na kusababisha mafuriko na uharibifu wa mazingira; ni kwa nini Serikali isitumie mvua, hivyo kutoa elimu ili wananchi wavune maji na yatumike wakati wa kiangazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.