Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia siku zote tatu tangu tarehe 7 hadi leo tarehe 9 Mei, 2018 ametujalia afya njema na kuendelea kujadili bajeti yetu ya maji na umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kulishukuru Bunge lako tukufu kwa kujadili hoja ya hotuba ya Wizara yangu niliyoiwasilisha hapa Bungeni tarehe 7 mwezi Mei, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hizi zimechangiwa na Wabunge 145, ninawashukuru sana. Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa Wizara yangu imechukua na itafanyia kazi ushauri na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji ili kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi wote wa nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kutokana na muda mfupi nilionao ninaahidi hoja zote tutazijibu kwa wananchi na kuwasilisha kwenu kupitia kwenye Hansard, na ninawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla hatujamaliza Bunge tarehe 29 Juni, 2018 Mwenyezi Mungu akitujaalia salama, basi majibu ya hoja zote mtakuwa mmeshayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Wakati na mimi naanza ubunge, naingia kwenye Bunge lako tukufu nilikutana na hoja ya dola milioni mia tano kutoka Serikali ya India lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwamba nikiwa sasa kama Waziri wa Maji na Umwagiliaji hoja hii sasa imekamilika. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama ulivyoona wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote watakaoguswa na mradi huu wamefurahi. Kwa maana ya fedha hizi kwenda kugusa kwenye hii miji 17, basi zile fedha ambazo ilikuwa tuzipeleke tumege kwenye fungu hili tulilotenga kwa fedha za ndani kupeleka maeneo yale zitakuwa zimeokolewa na zinaweza zikapelekwa maeneo mengine. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisome tu maeneo yatakayofaidika na hizi dola milioni 500 ambazo mkataba wetu wa kifedha utasainiwa kesho, ni pamoja na Muheza, Wanging’ombe, Makambako, Kayanga, Songea, Zanzibar, Korogwe, Njombe, Mugumu, Kilwa Masoko, Geita, Chunya, Makonde, Manyoni, Sikonge, Kasulu na Rujewa. Kwa hiyo, utaona fedha hizi itakapokuwa tumeanza kazi zitanufaisha wananchi wengi sana wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe taarifa tu kwamba hiyo Kamati iliyoko India, pia ilichukua watumishi watatu wa Wizara yangu ya Maji na Umwagiliaji. Wakitoka huko watakuwa wameshakamilisha na mpango wote wa manunuzi. Kama unavyofahamu Wizara yangu na jinsi ninavyoipeleka, wakishasaini mkataba huo basi mimi mara moja kazi inaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya majibu ya hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji; Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo ilianza mwaka wa fedha 2006/2007 na itakamilika ifikapo mwaka 2025. Utekelezaji wa programu hii unahusisha programu ndogo tano ambazo ni usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, huduma ya maji vijijini, huduma ya maji mijini, usafi wa mazingira mijini, kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira na kujenga uwezo wa kitaasisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya programu hii ililenga kujenga miradi 1,810 na hadi sasa tumeshatekeleza miradi 1,469 ambayo imekamilika. Miundombinu ya maji iliyojengwa ina vituo vya kuchotea maji 102,586 ambavyo vina uwezo wa kuhudumia jumla ya wananchi 30,972,000 sawa na asilimia 85.2 iwapo kama vituo vyote vilivyojengwa vingekuwa vinatoa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vituo 86,877 tu ndivyo vinatoa maji, vituo vilivyobaki havitoi maji. Hivi ndivyo ambavyo vimeshusha asilimia ambayo tungetarajia kuipata sasa hivi. Tungetarajia kuwa na asilimia 85.2; lakini tuna asilimia 58 hadi 59.76. Sababu mbalimbali zipo ambazo zimefanya hivi vituo ambavyo vimeshajengwa kwa fedha hizi ambazo tulichangiwa na wahisani mbalimbai pamoja na fedha za ndani zimekuwa hazitoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa michango yenu Waheshimiwa Wabunge nimewasikiliza kwa umakini sana, ni kweli kwa Mheshimiwa Mbunge ambaye tumeenda kutekeleza mradi kwenye eneo lake na aliwaambia wananchi sasa mmeona nimeleta fedha, halafu leo hii yale maji hayatoki, kuna uwezekano mkubwa lile Jimbo ukaanza kulikimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikiliza kwa makini sana Waheshimiwa Wabunge, na hasa kwa kuzingatia na mimi kwa sababu nasafiri kila eneo, sababu zote ambazo mmezitoa, mmetoa sababu nyingi kwamba hela inaliwa, uadilifu hakuna, hela inagawanywa, inapelekwa kule kwenye Halmashauri halafu inarudishwa Wizarani, siwezi kuwakatalia hilo kwa sababu hapa ushahidi upo kwamba tumetekeleza miradi, lakini kuna miradi mingine ambayo haitoi maji. Waheshimiwa Wabunge, niwape taarifa tu kwamba suala hili nilishaanza kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Rais huyu mimi huwa nawaambia watumishi kwamba ukitaka kutekeleza kazi vizuri tekeleza kwa Rais huyu, kwa sababu Mheshimiwa Rais yeye anapenda kazi, hana majungu, hana maneno na mimi kwa sababu ninamfahamu nilikuwa nimeshajiandaa. Mheshimiwa Naibu Waziri Kakunda amezungumza kwamba utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya maji, Wizara yangu kazi yake ni kupanga bajeti, kutoa miongozo na maelekezo lakini utekelezaji unafanyw ana Wizara kutoa miongozo na maelekezo, lakini utekelezaji unafanywa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nimeshaifanyia kazi Ntomoko muda wote, kwa hiyo, pale Mheshimiwa Rais alivyosema Mheshimiwa Waziri najua unanisikia hawa watu wa watomokoe, saa 24 nilikuwa nimeshawatomokoa tayari kwa sababu nilielekezwa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda Mara katika ziara yake akaniagiza kwamba fanya uchunguzi miradi yote ya Mkoa wa Mara na hata katika michango hii Waheshimiwa Wabunge wamelalamikia miradi iliyotekelezwa Mara. Natarajia ripoti ile imerudi na Mheshimiwa Waziri Mkuu nitamkabidhi ripoti hii Ijumaa. Waheshimiwa Wabunge lakini niseme tu kwamba yale maeneo yote tuliyotarajiwa kwamba tumepigwa wakandarasi wame-surrender wao wenyewe kwa barua kwamba, miradi hii wanaachana nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana nasema jamani tuna kiongozi mzuri, Mheshimiwa Rais kwa sababu anatenda haki. Hata yule ambaye alizowea tabia fulani sasa anaanza kukimbia mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwa ufanyakazi wangu a ndani ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji nasema hili ni somo, kama yule ambaye ulikuwa unashirikiananae yeye mwenyewe ameanza kushtuka hivi wewe bado unabaki kuwa na akili hiyo? Itakuwa ni kitu cha ajabu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge tumekwenda mpaka kwenye Mradi wa Mugumu tumeufanyia kazi. Tumegundua matatizo yote yaliyojitokeza, lakini ule hatuwezi kuusimamisha, tunatoa kibali mkandarasi aendelee na kazi ili mradi ule ukamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sababu mbalimbali ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, lakini pia, na Wizara yangu kuna sababu mbalimbali ambazo wameniambia. Hivi vituo vilivyojengwa vikatumia hela nyingi vimeshindwa kutoa maji, moja ya sababu ni kukauka kwa vyanzo vya maji. Hata hivyo kama Wizara tunajiandaa kuhakikisha tunatunza rasilimali zote za maji, tunazuwia kuvamiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nikushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri katika hotuba yako umezungumza kwamba, hata pale Songea sasa tunakwenda kulipa fidia. Tumeshajiandaa na tumetenga bajeti, Waheshimiwa Wabunge tunahitaji shilingi bilioni 18 ili tuweze kulipa yale maeneo yote makubwa, maeneo oevu ili yasiweze kuingiliwa na shughuli za kibinadamu. Tunayawekea sheria na tutawekea utaratibu na wale watakaokuwa wanayalinda, ili tuhakikishe kwamba, tunatunza rasilimali za maji, maana vinginevyo kila wakati tutakuwa tunatekeleza miradi halafu miradi ile inakuwa haileti tija inakauka, kwa hiyo itakuwa tumetumia fedha miradi inakuwa haitoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, uchaguzi wa teknolojia. Umetekeleza mradi kijijini bila kupima uchumi wa eneo lile, unapeleka generator ya kutumia dizeli, wananchi wanafika mahali hawawezi. Vyombo vya watumiaji maji tunavyoviunda hivi bado hatujaviimarisha, lakini tunaendelea kuwafundisha ili wawe na uwezo wa kusimamia hii miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru sana TAMISEMI wanaendelea kuvisajili na kuvifundisha, na mimi kazi yangu ni kutoa fedha ili waendelee kutoa elimu kwa hivi vyombo vya watumiaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakiri, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, miradi mingi haikusanifiwa vizuri na ndio maana imetupeleka huko ilikotupeleka; tumepoteza fedha. Hata hivyo tayari mwaka huu nimeshaunda timu ya wahandisi ndani ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na wanaanza kufanya kazi. Wahandisi hao watapitia usanifu wote wa kwenye halmashauri hata wataalam washauri watakaonunuliwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maji, wakishakamilisha wataalam hawa waandisi tutahakikisha kwamba, wanapitia zile nyaraka, ili tuweze kuokoa fedha, value for money lazima ipatikane.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kumekuwa na muingiliano ambao unatusumbua kama Serikali. Hapa panasimamiwa na taasisi hii, pengine TAMISEMI, huku wanasimamia Wizara, huku anasimamia Mhandisi Mshauri ambaye ameajiriwa na analipwa pesa, hawa watu wanatuchanganya, tunataka kutengeneza mfumo ambao utasimamiwa na mtu mmoja ili kama tunamlaumu tunamlaumu mtu mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata hoja nyingi za ubadhirifu wa fedha kwenye miradi ya maji, katika huu muda wa siku tatu ilikuwa tukitoka hapa tunakwenda kukaa na Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, namshukuru sana na tarehe saba tulivyomaliza hotuba hapa nilikwenda kukaa na wafadhili, kumbe na wafadhili nao lilikuwa linawauma, wameafiki kwamba kuna haja ya kuunda timu ya wataalam watakaopitia miradi yote iliyotekelezwa, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mnapendekeza. Mlipendekeza kwamba iingie Kamati ya Bunge, lakini kabla hamjafika hapo sisi tayari tumeshaunda kamati na kamati hii itasimiwa na Profesa Mbwete wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kujaza wataalam ili tuhakikishe kwamba miradi yote iliyotekelezwa katika programu hii iliyoanza mwaka 2006/2007 inapitiwa, na Waheshimiwa Wabunge tutatumia sheria, tutatumia nyenzo zote ambazo zimewekwa na Serikali. Mheshimiwa Rais
amesema jamani hela ya maji awamu hii ni sumu, kama kuna mtu alihujumu basi wakati wake umefika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ndugu zangu na kwa umri nilio nao kwa kweli sina huruma na mtu ambaye ni mwizi na niko hivyo hata huko nilikotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yetu kwamba Kamati hii itafanya kazi kwa uadilifu, na nitaisimamia, na tunaendelea kuchagua watu ninawajua, waadilifu ninawajua wako wengi tu ambao tutawaweka pale. Kwa hiyo, ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge, naomba sana watakapokuja kwenye Halmashauri zenu, kwenye maeneo yenu muwape support kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, sisi ni Madiwani. Baada ya bajeti hii kupita wanapokwenda kutenegeneza mipango kazi kwenye halmashauri na sisi tuwepo, ni muhimu sana hili. Kwa sababu, wakati mwingine napata shida nakwenda kwenye halmashauri nakwenda na Mheshimiwa Mbunge, tunafika kule wakati wanapanga mpango kazi kumbe hata sisi madiwani hatukuwepo, wote tunakuwa wageni, naomba tushirikiane.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikija kwenye jimbo lako nataka nipate taarifa kutoka kwa wewe Mbunge, kwamba hapa kuna hili, ili niweze kufanyia kazi kwa sababu na mimi ni mtaalam. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka kwenye bajeti ya mwaka jana niliwaambia Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana tunawapa hivi vitabu vya bajeti. Tukishakamilisha hii bajeti Waheshimiwa Wabunge na ninawaomba sana, muipitishe, ili tutekeleze miradi ya maji baada ya hapo mwambie Mkurugenzi wako wa Halmashauri una shilingi kambi katika mwaka ujao wa fedha ili aanze kujipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wameonesha kwamba, fedha hazijatengwa, akiwemo mama yangu Mheshimiwa Magdalena Sakaya, nitakuonesha hela yako iko wapi kwenye kitabu bila wasiwasi wowote. Una fedha ya kutosha imetengwa, hatuwezi kuacha Halmashauri ya Kaliua. Nchi hii Rais ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ndio Rais wa Watanzania. Ni Rais ambaye ametokana na chama tawala, Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo, wananchi wote hawana mtu mwingine atakayewahudumia ni Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge katika Bunge la mwaka jana walimuelekeza Waziri wa Maji na Umwagiliaji aangalie uwezekano wa kuunda Wakala wa Maji Vijijini. Ninaomba kutoa taarifa kwamba tumefanya kazi hiyo mliyotuelekeza, tumeshirikiana kati ya Wizara yangu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Rais, Utumishi na Wizara ya Fedha na Mipango, tayari tuliunda kamati imeanza kuangalia uwezekano wa kuunda taasisi hii muhimu sana ya Wakala wa Maji Vijijini. Tumeshafika hatua ya mbali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, strategic plan tayari, business plan tayari imeshaandaliwa, framework document tayari imeshaandaliwa, establishment order nayo imeshaandaliwa tayari. Kwa hiyo, taratibu za kisheria zinaendelea, lakini pia sasa tunaingia kupata maoni ya wadau kwa mujibu wa taratibu na tunatumia sheria ya uanzishwaji wa wakala Executive Agency Act, Cap. 245. Tutafika stage ambayo tutaomba ridhaa ya mamlaka husika, ili uweze kuanzisha huu wakala. Kwa hiyo, yale mliyoelekeza Waheshimiwa Wabunge tayari tumeshaanza kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waheshimiwa Wabunge walipochangia sana hotuba hii, na nishukuru kwa kweli Waheshimiwa Wabunge wamechangia na mimi nimefuatilia sana. Kulikuwa na tofauti kubwa za kitakwimu kati ya kitabu kilichoandikwa na Wizara ya Maji, lakini pia na kitabu kilichotolewa na Hoja za Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna tofauti ya kitakwimu kuhusu fedha za maendeleo zilizopokelewa na Wizara kati ya Taarifa ya kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa iliyopo katika Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019. Tofauti hiyo imetokana na muda wa kuwasilisha Taarifa hizo. Nirudie tena, tofauti hiyo imetokana na muda wa kuwasilisha taarifa hizo, hadi tunakutana na Kamati mwezi Machi, fedha zilizopokelewa kwa Fungu 49 zilikuwa sawa na asilimia 22 kama Taarifa ya Kamati ambavyo ilikuwa imeelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunakamilisha maandalizi ya hotuba ya bajeti hadi tunakutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti mwezi Mei, 2018 Wizara ilishapokea fedha zaidi, hivyo tuliona ni muhimu kutoa taarifa hadi kipindi hicho kwa sababu Hazina tayari walishatuletea fedha nyingine. Taarifa iliyowasilishwa katika Kamati mwezi Machi ilijumuisha fedha za nje zilizopokelewa kutoka hazina kwa njia ya exchequer pekee. Aidha, kuna fedha za wafadhili ambazo hupelekwa moja kwa moja katika miradi ya maendeleo kabla ya kuingizwa kwenye exchequer.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zinapelekwa kwenye miradi mbalimbali baada ya utekelezaji ambapo badaye baada ya mwaka Hazina huwa wanaziingiza kwenye exchequer. Lakini kwa sababu tulikuwa tunaendelea kukusanya taarifa baada ya kupata taarifa hizo tulilazimika kuingiza hizo fedha na baadae kuwasilisha kwenye Kamati ya Bajeti. Baada ya kuziingiza sasa tukawa tumepata, sasa fedha ambazo tulikuwa tumezipata hadi mwezi Mei ni shilingi bilioni 359.9 ambayo inafanya sasa fedha ambazo zimetolewa na Serikali hadi kufikia mwezi Mei ni asilimia 56. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hiyo ndio tofauti ambayo tumeiona kati ya Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na taarifa ambayo tumeitoa mwishoni kwa sababu ilibidi tukiri fedha ambazo tayari tumeshapewa na Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishukuru sana Kamati yangu ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Tumefanya ushirikiano kwa muda mfupi, lakini tumefanya mengi. Tangu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iundwe au iteuliwe mwezi Machi, 2018 Wizara yangu imeshakutananayo mara tatu, tarehe na ajenda tulizojadili tulipokutana ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya tarehe 26 na tarehe 27 Machi, tulikutana na Kamati ili kupokea na kujadili na kupitisha bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2018/2019; tarehe 7 Aprili tulikutana na Kamati kupokea taarifa kuhusu utendaji wa Tume ya Umwagiliaji, lakini tarehe 20 Aprili, 2018 tulikutana na Kamati kwa ajili ya kupokea Taarifa Kuhusu Utendaji wa DAWASA na DAWASCO na mchakato wa kuunganishwa kwa taasisi hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kikao cha kujadili taarifa ya utendaji wa DAWASA na DAWASCO Wizara iliwasilisha kwa kina taarifa ya uamuzi wa Serikali wa kuunganisha taasisi za DAWASA na DAWASCO na hatua iliyofikiwa katika mchakato huu. Ilielezwa kuwa kuanzia tarehe 01 Julai, mwaka 2018 Shirika la DAWASCO litakoma na kutabaki na Shirika moja la DAWASA lililofanyiwa maboresho ya kimuundo na majukumu. Hatua iliyofikiwa hadi sasa ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuandaliwa kwa kuundo na majukumu mapya ya DAWASA; mbili kuandaliwa kwa muundo na utumishi wa DAWASA; lakini tatu ni kuandaliwa kwa muundo na mishahara ya DAWASA na nne ni kuandaliwa kwa orodha ya kazi, maelezo ya kazi na kanuni za utumishi za DAWASA. Pia namba moja hadi nne tayari zimeshawasilishwa kwa Msajili wa Hazina na Utumishi kwa ajili ya idhini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kufanya tathmini ya madeni na mali za DAWASA na DAWASCO; Kamati maalum iliundwa kufanya kazi hii na imemaliza kazi yake na imewasilisha taarifa yake jana kwa Katibu Mkuu, jana tarehe 8 Mei, 2018. Kwa sababu hizi taasisi mbili zinaungana kwa hiyo, lazima kubainisha madeni ambayo taasisi zinadaiwa na madeni ambayo taasisi zinadai.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kukamilisha mchakato wa kuunganisha DAWASA na DAWASCO ni pamoja na; kuandaa De- Establishment Order ya DAWASCO kwa sababu tarehe 01 DAWASCO itakoma; kuunda Bodi ya DAWASA, kufanya marekebisho ya Sheria ya DAWASA ya mwaka 2001 na ile ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009 kwa sababu hatuwezi kuwa na sheria mbili wakati taasisi hizi zinafanya kazi moja. Hatua zote hizi zinakwenda vizuri kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mchakato wote huu wafanyakazi wa DAWASA na DAWASCO kupitia vyama vyao vya wafanyakazi pamoja na wafanyakazi wote kwa ujumla wao wameshirikishwa kikamilifu. Hakuna taharuki yoyote inayotokana na mchakato huu katika Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo taarifa ya Kamati imekiri kwa kuishukuru Wizara katika taarifa yake ukurasa wa 52 kwa ushirikiano mkubwa ambao imekuwa ikiupatia Kamati yangu tangu Kamati ilipoteuliwa mwezi Machi, 2018. Wizara yangu itaendelea kuipa Kamati ushirikiano mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na changamoto pia ambazo zilikuwa zimeainishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, lakini hoja hizi ambazo ziliibuliwa wakati tunapitia kutafuta majibu tumekuja kukuta kwamba ni hoja ambazo pia zilikuwa zimeibuliwa na CAG. Sasa kwa sababu zimeshaibuliwa na CAG, na kwa mujibu wa taratibu hoja zimeibuliwa na CAG na zikaletwa katika Bunge, ninamuagiza Katibu Mkuu na nifurahi tu kwamba, majibu tayari wameshajibu sasa wanasubiri taratibu za kiserikali kwa ajili ya kuitwa na kupeleka PAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuagize Katibu Mkuu ahakikishe kwamba hoja hizi zipelekwe, ili kwa mujibu wa sheria iliyopo hoja zikishaibuliwa upo utaratibu maalum ambao unatumiwa, ili kuweza kuzifikisha kwenye Kamati ya PAC na baadae sasa ndio zitatolewa majibu kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji pia ina tume ya umwagiliaji, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA imekamilisha kuandaa upya mpango kabambe wa umwagiliaji. Mpango huu umeweka dira, malengo na mikakati ya kuendeleza sekta ya umwagiliaji kati ya mwaka 2018 hadi mwaka 2035. Mpango huu umeandaliwa kwa kuzingatia hali ya upatikanaji wa rasilimali maji katika mabonde tisa na umeainisha kwa karibu na malengo ya Programu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo. Tunaamini utekelezaji wa mpango huo utahusisha na kuinua sekta ya umwagiliaji hapa nchini. Tukishakuwa na umwagiliaji maana yake ni kwamba kilimo chetu kitakua, kilimo kitakuwa na uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa na timu hii ya Wajapan imebainisha mambo mengi sana. Tumekuwa na scheme za umwagiliaji ambazo zinafanya kazi mara moja kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesema ni kweli, zinafanya kazi mara moja kwa sababu zilijengwa bila kujengewa chanzo cha maji. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge nina imani taarifa hii inakabidhiwa mwezi Mei na baada ya hapo sasa tutatoa taarifa rasmi kwa Kamati yetu ili pengine kwa jinsi itakavyoamua Kamati tunaweza kuja kutoa taarifa katika Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia miradi ya maji mijini tunaendelea kutekeleza. Mfano Jiji la Dar es Salaam na nishukuru sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wangu amezungumzia. Jiji la Dar es Salaam tumetengeneza miradi mikubwa kwenye vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini na maji sasa yanapatikana yapo kwa wingi. Kitu kilichobaki ni kuhakikisha kwamba tunaweka miundombinu ya kutosha ili tuweze kuyasambaza maji kwenda kwa wananchi na tayari tumeshaanza. Serikali imefanya utafiti, imefanya utafiti/study na kuona kwamba tunahitaji dola milioni 100 ili tuweze kukamilisha kusambaza maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kwanza wa dola milioni 32 umeanza na unakaribia kukamilika. Baada ya muda mfupi tumepata tena dola milioni 45 ambayo tunakaribia kutangaza tender ili tuendeleze kusambaza mabomba kwenye maeneo mengine ambayo bado hayajapata huduma ya maji safi na salama katika jiji la Dar es Salaam. Kwa kufanya hivyo Waheshimiwa Wabunge ni kwamba pia tutapunguza na upotevu wa maji na tunaendelea kutafuta teknolojia nzuri na tunafanya trial mbalimbali kama Mji wa Tanga kwa sasa, bomba likivuja ule mtandao wa bomba umeainishwa kwenye simu yako ya mkononi, kwa hiyo itakuwa ni rahisi ku-detect sasa kama maji yanavuja ni rahisi kutuma wataalam waende wakaone hapo kuna nini, kuna wizi na kuziba ili tuendelee kupunguza upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru tena sana Waheshimiwa Wabunge sipendi tena nipigiwe kengele kwa sababu kengele ya kwanza imeshapiga, lakini niwashukuru sana Wabunge kwa michango yao na niseme nitaendelea kama nilivyo tabia yangu napenda kuongea na Mbunge yeyote aniambie hoja moja kwa moja na nilivyo ukiniambia naifuatilia na lazima nitakuja hata kwenye jimbo lako ili tuizungumze ili niweze kuifikisha katika Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Wabunge, Wizara yangu kwa kweli kama mlivyosema ninyi wenyewe ina mapenzi mazuri kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama.

Ninaomba mtupitishie bajeti hii ili tuweze kuendelea kupambana kwa kushirikiana na ninyi na taasisi mlizonazo kwenye majimbo ili tuweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya naomba kutoa hoja.