Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, naomba leo nianze kwa kutoa tafsiri fupi ya nini maana ya viwanda. Kiwanda ni mahali ambapo malighafi inachakatwa kuwa bidhaa iliyokamilika kwa ajili ya mtuamiaji au bidhaa kwa ajili ya viwanda vingine viweze kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa tafsiri hiyo fupi ya viwanda, sasa tutaona Tanzania tutaweza kuelekea katika nchi ya viwanda. Historia ya viwanda duniani kote ukiangalia kwa mfano Britain, America, India, France, China walianza kwa kuwa na viwanda vya nguo na ndipo wakaweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto ameeleza kwa kifupi mimi nitaenda kwa undani zaidi. Inasikitisha sana ni kwa namna gani sisi kama Tanzania tunaweza kuwa ni nchi ya viwanda kama hatutaongelea viwanda vya nguo. Leo katika kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri sijaona ni namna gani ameongelea viwanda vya nguo nchini Tanzania. Hii inasikitisha sana kwa sababu inaonesha ni kwa namna gani hatuwezi kuwa na nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kuwa na nchi ya viwanda nchini Tanzania halijaanza leo, lilianzishwa na Mheshimiwa Rais wetu Mtukufu, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1970 hadi mwaka 1992 viwanda vikabinafsishwa. Inasikitisha Serikali haijaweza kuvichukulia hatua yoyote viwanda 156 vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niko katika Kamati ya Viwanda na biashara. Kamati ilitisha list ya viwanda 156 ambavyo vilibinafsishwa mwaka 1992. Taarifa ambayo ililetwa mbele ya Kamati na ninayo hapa, Serikali inajaribu kueleza ni kwa namna gani inachukua hatua lakini ukiangalia maelezo yanayotolewa ni kwamba ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali unachukuliwa na wanasema mashauri mengi yako mahakamani.

Mheshimiwa Spika, taarifa hii kusema ukweli hata Kamati ilisoma na ikaona na haikuweza kuridhika na majibu ya Serikali. Nilitegemea leo hii katika kitabu hiki ambacho ni cha Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Waziri angeweza kuelezea na kufafanua ni kwa namna gani Serikali imejipanga kuwachukulia hatua watu ambao walibinafishiwa viwanda
156. Watu hawa ni wezi, ingekuwa ni nchi nyingine kama China wangenyongwa kwa sababu ndiyo wametufikisha hapa sisi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umasikini tulio nao Tanzania leo ni kwa sababu ya viwanda vilivyobinafishwa. Viwanda hivyo 156 vingi ambavyo ni vikubwa vilikuwa ni vya nguo. Sasa ukiangalia kama nilivyoanza kusema viwanda vya nguo vilisababisha nchi za Marekani, Britain, France na China kuweza kufanikiwa kuwa nchi za viwanda lakini leo hii sasa sisi Tanzania tuko wapi, tunaenda wapi? Naitaka Serikali kuchukua hatua kwa hivi viwanda ambavyo vilibinafsishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutangulia kusema hayo, naomba sasa tuangalie katika Mkoa wa Mwanza. Mwanza tuna Kiwanda cha MWATEX. Kiwanda cha MWATEX kilikuwa kina wafanyakazi zaidi ya 3,500 miaka ya nyuma kikashusha wafanyakazi hadi kufikia 1,500. Leo hii tunaongelea wafanyakazi si zaidi ya 150 katika Kiwanda cha MWATEX. Suala hili linasikitisha sana. Siku moja nilisikia Mheshimiwa Rais akisifia kwamba Kiwanda cha MWATEX kinafanya vizuri, yawezekana Mheshimiwa Rais hajapata ukweli kutoka kwa watendaji juu ya Kiwanda cha MWATEX. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana sana, watendaji wa Wizara hii ya Viwanda wamsaidie Mheshimiwa Rais, kwa kumueleza ukweli na si kwa kuja hapa kwa kujitamba kwamba tuna viwanda vingi, viwanda vingi wakati impact kwa Watanzania haionekani? Mtu anakuja hapa anaongelea suala la viwanda vya cherehani, hivi unataka kusema leo hii mimi nikimuita Waziri wa Viwanda na Biashara kwamba twende naye Mwanza tukazindue viwanda watu wana vyerehani vinne, atakuja kweli? Je, inaleta impact? Mimi hainiingii akilini, sahamahi sana kwa kusema hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna Kiwanda cha MUTEX ambacho kiko Musoma kimekufa. Pamoja na viwanda vingine ambavyo vimekufa Kiwanda hiki cha MUTEX kinanisikitisha kwani kilikuwa kinatoa vitenge na kanga nzuri, vitenge vilikuwa vinauzwa mpaka nje ya nchi Swaziland. Leo hii kiwanda kimekufa lakini katika kitabu kiwanda hiki hakionekani kuongelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naitaka Serikali kuangalia ni kwa namna gani inachukua hatua madhubuti za mikakati kuweza kuviinua viwanda ambavyo vilikuwa vimekufa ambavyo ni viwanda vya nguo ili nasi tuweze kuitumia pamba yetu. Katika Mkoa wa Mwanza na mikoa mingine kama Simiyu na Shinyanga wanalima pamba kwa wingi lakini unapoangalia kwenye taarifa ya Waziri ni asilimia 30 tu ya pamba ndiyo ambayo inatumika, pamba nyingine yote inaenda nje.

TAARIFA . . .

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunisaidia kujibu taarifa ile isiyokuwa na maana yoyote. Kwa sababu mimi sijasema viwanda ameviua Mheshimiwa Mwaijage ndiyo maana naona kwamba taarifa ya kaka yangu pale haijakaa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niendelee kwa kusema kwamba viwanda hivi vinapaswa kufufuliwa kwa ari kubwa sana ili pamba iweze kutumika kwa asilimia walau 70 ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Urafiki kinasikitisha. Leo hii ukienda kwenye kiwanda kile kuna show room ya magari ya Wachina iko pale. Ni kwa sababu gani Kiwanda hiki cha Urafiki hakifanyi kazi? Tunakuomba Mheshimiwa Mwaijage pamoja na watendaji wote katika Wizara hii muangalie viwanda hivi ambavyo ndivyo vinaweza kutusaidia Watanzania kujivunia na kuwa nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii ukiangalia Kiwanda cha Kiltex, Mbeya Textile, Sungura Textile, Tabora Textile vyote havipo. Katika taarifa tunaambiwa kuna viwanda 11 vya nguo, sijui ni viwanda gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote hayo niliyoyaongea, naomba nitumie dakika mbili kutoa ushauri kwa Serikali. Hatuwezi kuwa na viwanda vya uhakika kama hatuwezi kusaidia upatikanaji wa uhakika wa umeme katika viwanda vyetu. Mashine nyingi zinakufa katika viwanda kwa sababu umeme upatikanaji wake siyo effective. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali iweze kujitahidi kuangalia viwanda vyetu vinapata umeme wa uhakika lakini pia vinapata maji ya uhakika na pia barabara za kutoa malighafi sehemu moja kupeleka katika viwanda na kutoa bidhaa viwandani kwenda sehemu za masoko ili kuweza kusaidia viwanda vyetu kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba kutoa ushauri, kama inawezekana Serikali ichukue ushauri huu, kwamba viwanda vya nguo vitolewe ile asilimia 18 ya kodi ili kuweza kuvi- motivate kuweza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja lakini yale niliyoyasema yaweze kuzingatiwa na Serikali na hatimaye yaweze kufanyiwa kazi. Nashukuru sana.