Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. ZAINABU M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuumba sisi kuwa wanadamu kisha akatupa akili na ufahamu ili kuweza kujadili mambo mbalimbali kuhusu Taifa letu. Pili, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ni kitovu cha biashara katika nchi yetu na wafanyabiashara wa Dar es Salaam huchangia pato kubwa katika Taifa hili lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi sana. Ili uanzishe biashara kuna taratibu za kufuata hadi biashara yako ifunguliwe, kwanza lazima upate leseni, lakini kinachotokea kwa wafanyabiashara hao wanaanza kulipa mapato kabla ya kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawaumiza sana wafanyabiashara. TRA wanakadiria watu mapato kulingana na eneo analilopo na siyo biashara wanayoifanya. Wanapoenda kudai leseni wanaambiwa kwanza waende TRA wakakadiriwe mapato, nauliza inawezekanaje mtu hajaanza kufanya biashara anakadiriwa mapato, kauza nini huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali Taasisi ya Mamlaka ya TRA itoe grace period kwa wafanyabiashara. Wakati wanataka kuanzisha biashara zao kwanza wapewe leseni, pia wapewe muda wa kufanya biashara hiyo angalau miezi mitatu wakati wanatumia mashine za EFD kisha ndiyo wakadiriwe. Kitendo kinachofanywa na TRA kuwakadiria watu mapato kabla ya biashara kwa kweli, kinawaumiza sana wafanyabiashara, hususan wa Jiji hili la Dar-es-Salaam. Naomba sana Serikali ilichukue hili na ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishauri Serikali wale ndugu zetu wafanyabiashara ndogondogo Wamachinga ni wafanyabiashara pia lakini watengewe maeneo maalum. Sasa hivi ukifika katikati ya Kariakoo maeneo ya Narung’ombe, Kongo, Mchikichi, wafanyabiashara ndogondogo wameweka bidhaa zao mbele ya maduka ya wafanyabiashara ambao wanalipa kodi kihalali. Kutokana na buyer behavior ya watu wetu wa Tanzania wenye kipato cha chini kuona kwamba biashara zilizokuwa barabarani ni rahisi kuliko za ndani hupelekea watu wenye maduka kushindwa kufanya biashara zao vizuri na Taifa kukosa mapato kutokana na kwamba wafanyabiashara wale wanaosambaza barabarani kutolipa mapato ya aina yoyote.

Kwa hiyo, naishauri Serikali itenge maeneo maalum kwa ajili ya Wamachinga ili nao waweze kufanya biashara pia walipe kodi kwa Taifa letu. Najua kwamba Machinga ni wapiga kura pia wafanyabiashara wa madukani ni wapiga kura wa Taifa hili, kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine sasa hivi kumetokea mtindo kwa Kikosi cha Zimamoto kupita katika maduka ya wafanyabiashara Kariakoo kuwalazimisha waweke fire extinguisher ndani ya maduka. Fire extinguisher ina kilo 5 na kila mtungi mmoja ni Sh.200,000 na kila mwisho wa mwaka ulipe Sh.40,000 unaweka ndani ya duka, je, moto ukitokea saa 8.00 za usiku wakati mfanyabiashara huyo yuko nyumbani kwake ile fire extinguisher itamsaidia nini kuokoa mali zake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni dhahiri kwamba Kikosi cha Zimamoto kimeanzisha mradi mwingine kwa wafanyabiashara ili kuwakandamiza. Naishauri Serikali ikutane na Kikosi cha Zimamoto, iwashauri wale wamiliki wa majengo waweke fire extinguisher kwenye corridors za nyumba na siyo ndani ya maduka ya wafanyabiashara, kwa sababu huwezi kujua moto utatokea wakati gani. Ni bora fire extinguisher ziwekwe kwenye corridor kuliko ndani ya maduka ya wafanyabiashara, hii itasaidia moto ukitokea wakati wowote aidha, asubuhi, mchana hata usiku kuweza kutumia fire extinguisher kuzima moto ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuelekea Tanzania ya Viwanda kuna viwanda vingi ambavyo vimepewa wawekezaji. Nitatolea mfano Kiwanda cha Nguo cha Karibu Textiles Mills ambacho kiko Wilaya ya Temeke. Kwa sasa hivi kiwanda kile kimefungwa na kimegeuzwa kuwa ghala la kuhifadhia soda. Nimetembelea mwezi uliopita pale wameweka soda na kiwanda kile kilikuwa kinazalisha nguo, vitenge, khanga pia mashuka na kilikuwa kinaleta ajira kwa zaidi ya watu 1,000. Kwa sasa hivi Mheshimiwa Waziri kimegeuka kuwa ghala la kuhifadhia soda na hakuna kiwanda tena pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, wakati tunaelekea Tanzania ya Viwanda badala ya kutafuta maeneo ya kuanzisha viwanda vingine ni bora kwanza tuvifufue vile viwanda ambavyo vimepewa wawekezaji. Maeneo mengi yalikuwa na viwanda, nitakutolea mfano Mkoa wa Morogoro, mwaka wa 1980 ulikuwa ukifika Morogoro unaweza kupata ajira mapema kuliko kupata chumba cha kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna Kiwanda cha Canvas Mill, Ceramics, Polyester, Moro Shoe, Tanneries, Magunia, Kiwanda cha Tumbaku, Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Kiwanda cha Sukari Kilombero, vyote hivi vilikuwa Mkoa wa Morogoro, lakini kwa sasa hivi viwanda vile wamepewa wawekezaji na haviendelezwi. Morogoro ni katikati ya Dar es Salaam na Dodoma, viwanda vile vifufuliwe na kupewa wawekezaji na kusimamiwa vizuri, iwe ni sampling area. Sasa hivi tunajenga treni ya mwendokasi ambayo itarahisisha watu kufika kwa urahisi Morogoro, italeta ajira kwa watu wa Morogoro, Mkoa wa Pwani pia wa Dodoma wanaweza kupata ajira katika Mkoa wa Morogoro. Badala ya kutafuta maeneo ya kwenda kuanzisha viwanda vingine ni bora tuvifufue viwanda vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona viwanda vingi pia Mkoa wa Tanga. Kilikuwepo Kiwanda cha Mbolea, Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Amboni, Kiwanda cha Gardenia na Mbuni, viwanda vile vyote vifufuliwe kuliko kwenda kuanzisha maeneo mengine mapya, ili viweze kutoa ajira kwa watu wetu. Mkoa wa Tanga unazalisha matunda mbalimbali lakini katika hotuba ya Mheshimiwa tunashauri, kuanzishwe Kiwanda cha Juice ambapo itasaidia wakulima kwenda kuuza matunda yao katika kiwanda kile, kuliko sasa hivi matunda ikifika msimu yanaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushauri Mheshimiwa sana wakati unaelekea kuanzisha viwanda vipya vile vya zamani visimamiwe kwa uhakika ili kuleta ajira na pato la Taifa letu. Naomba haya yazingatiwe kwani yatasaidia sana kuliendeleza Taifa letu kuliko kuanza kukata misitu huko na
kutafuta mashine za kufunga, tuboreshe mashine katika viwanda vya zamani ambavyo vitasaidia kuleta ajira kwa kwa wananchi wetu na pia kuchangia katika pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naomba maoni ya Kamati yazingatiwe ili kuelekea Tanzania ya Viwanda. Ahsante.