Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii. Kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbilinyi (Mheshimiwa Sugu) kwa kutoka siku ya leo. Namshukuru sana Mungu aliyemwezesha kukaa gerezani kwa muda wote bila kutetereka na sasa ametoka anakuja kutekeleza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia hotuba hii na nataka kumaanisha ili ushauri wetu ambao tumekuwa tukiutoa kila wakati katika Bunge Serikali iweze kuufanyia kazi Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namkumbuka sana Mheshimiwa Mbilinyi alijaribu kuzungumzia sana kuhusiana na jambo ambalo lilikuwa linafanywa na Serikali ya kuikusanyia nchi ya Kongo mapato. Baada ya ushauri ule nafikiri Serikali ilikubali na sasa ilishaondoa na sasa hivi naona Wakongo wanatumia Bandari ya Dar es Salaam vizuri na mambo yanakwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba siasa safi ni uchumi. Tusije tukajidanganya hata siku moja tukafikiri siasa za kibabe, siasa za kutenganatengana zinaweza zikasababisha nchi ikawa na uchumi bora. Siasa ni uchumi lakini pia uchumi ni sayansi. Kwa hiyo, sisi ni lazima tujue kabisa kwamba umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, bila kujua hili tukaendeleza ubabe tunakoelekea siko kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kuhusiana na wafanyabiashara wengi Tanzania wanaohama nchi. Liko kundi kubwa sana la wafanyabiashara ambao wanahama katika nchi yetu na wanakwenda kufanya biashara kwenye nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo liko wazi na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara wajibu wake mkubwa ni kuhakikisha kwamba ustawi wa wafanyabiashara na biashara zao katika nchi hii ya Tanzania ni kipaumbele kikubwa kabisa. Huwezi kuamini wafanyabiashara wengi sasa hivi, ukienda Malawi wengi wamehamia kule. Ukienda Zambia maeneo yote kuna wafanyabiashara wametoka Tanzania wamehamia Zambia. Pia ukienda Kongo ambako hali kwa kweli ya usalama si nzuri lakini wafanyabiashara wako tayari kuondoka Tanzania waende wakafanye biashara Kongo, kwa sababu ya mazingira mabaya ambayo yapo kwa wafanyabiashara wetu ambao wanajitahidi kuwekeza kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu jambo moja kwamba leo Mtanzania akitoka na mzigo wake Dubai, akifika kwenye Bandari ya Dar es Salaam amekuja na invoice yake ya kiwandani kabisa alikonunua mzigo kinachotokea watu wa TRA wanamwambia kwamba hii wamekukadiria vibaya umetengeneza invoice, anaanza kukadiriwa upya akiwa bandarini Dar es Salaam. Amenunua mzigo wa Dola milioni 10 anaambiwa huu mzigo bwana ni milioni 20, mfanyabiashara anakimbia, anaacha mzigo, mizigo inakaa pale kwa muda mrefu na biashara baadaye zinakufa na huyo mfanyabiashara anapoteza fedha zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nakumbuka wakati tunajadili hapa, juzi nilikuwa nasikiliza Radio Clouds wanasema tumeshangaa sana Wabunge wetu, wanasema wakati Mbunge anaomba mwongozo watu walishangilia sana, wakati Mwijage anajibu watu wakashangilia sana lakini wakati Mheshimiwa Spika anatoa ufafanuzi na kutoa maelekezo kwa Serikali watu wakashangilia tena. Sasa wanasema Wabunge wetu hawa tatizo ni nini hapa yaani kipi ambacho walikuwa wakikishangilia, ni ule mwongozo uliotolewa na yale majibu ya Waziri au kilichokuwa kinashangiliwa ni yale maamuzi ambayo Mheshimiwa Spika aliiagiza Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tumesikia hapa wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu akitoa maelekezo kuhusiana na tatizo la mafuta ambayo yako bandarini. Ametoa maelezo hapa na akasema kwamba anatoa siku tatu. Tunaomba sana uchumi hauhitaji nguvu, unahitaji kukaa na kuzungumza. Hawa wafanyabiashara ambao wamekaa kule na mizigo yao nia yao kubwa ni kuja kuuza na kuhakikisha kwamba wanalipa kodi kwenye Taifa hili lakini kitendo cha kuendelea kutumia nguvu kwa kuwalazimisha haitaweza kutusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ikubali kukaa na wafanyabiashara. Hata mwanzo tuliwaambia kukaa na wafanyabiashara na kuzungumza nao ni jambo kubwa katika nchi hii. Hawa ndiyo watu wanaoweza kulipa kodi na ndiyo ambao wanaweza wakaendesha Taifa hili, lakini bila wafanyabiashara kukubali kufanya biashara katika nchi hii na kuwekewa mazingira mazuri nchi hii haitakusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekiri hapa ndani, amesema tatizo kubwa kwa nini mnasema fedha hazijaenda huku, kwa sababu makusanyo yamekuwa madogo, fedha hakuna. Tafsiri yake ni kwamba wafanyabiashara hawalipi kodi kwa sababu biashara zao zimeshadhoofi lakini wengine wamefunga biashara, wengine wamehama na biashara zao, sasa anataka kodi kutoka kwa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kuangalia ni namna gani wanaweza wakatengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya wafanyabiashara wetu ili waweze kufanya biashara vizuri. Ukienda Tunduma pale mpakani tumepakana na eneo la Nakonde Zambia. Sasa hivi nyumba ambazo walikuwa wanaishi Wazambia zimeshafumuliwa Watanzania wameingia mikataba wameamua kuhamisha biashara zao na sasa wamefungua maduka makubwa upande wa Zambia kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza sana, nimesema ndani ya Bunge lakini pia nimewashauri Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya hawawezi kusikiliza wanaendelea kukomaa wanasema hapana tunataka tufunge barabara. Wamefunga njia ambazo watu walikuwa wanapita, wafanyabiashara wa Zambia na Kongo wakitoka wamenunua mizigo wanapita katika njia ambazo walikuwa wanazipita siku zote. Wamefunga wameweka mataruma wafanyabiashara wa Kongo na wa Zambia wamesema hatuji tena Tanzania tunakwenda kununua maeneo mengine. Kwa hiyo, walichokifanya wafanyabiashara wameamua kutumia akili zao za haraka haraka na kwenda kuhamia upande wa Zambia na leo Zambia maduka ni mengi. Wafanyabiashara walioko pale sasa hivi ni karibuni wafanyabiashara 3,000 waliohama kutoka Tunduma wanafanya biashara Zambia lakini wanalala Tanzania. Kwa hiyo, tunachokizungumza hapa tunakuwa tunamaanisha katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni lazima pia afike mahali aangalie kodi kwenye Taifa hili limekuwa ni tatizo. Kila mwaka wanaleta taarifa hapa kwamba wanakwenda kuzifanyia kazi hizi kero za kodi ili wafanyabiashara wetu waweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuamini, wafanyabiashara wengi sasa hivi wanakadiriwa kodi, mtu anakadiriwa shilingi milioni 300, shilingi milioni 400, mwingine anakadiriwa shilingi bilioni 1, shilingi bilioni 2 bila sababu za msingi na kuelezwa kwa nini anatakiwa kulipa kodi hiyo. Wafanyabiashara sasa hivi wamekuwa kama wakimbizi, Serikali haiwaamini wafanyabiashara wa Tanzania. Serikali inawaona ni wezi wafanyabiashara wa Tanzania na Serikali inawaona wafanyabiashara wa Tanzania ni watu ambao wanakwepa kodi wakati si kweli. Kazi ya Serikali ni kuweka mazingira bora na safi ya kufanyia biashara na siyo kuwayumbisha wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema ni lazima tukubaliane ukienda TRA sasa hivi wanakukadiria fedha wanayotaka na ukiwaambia sina fedha wanakwambia nenda halafu baadaye wanakwambia bwana ili tukufanyie vizuri tunaomba utupe labda shilingi milioni 10 au shilingi milioni 5 au shilingi milioni 6 na kwa sababu Serikali imewatia woga wafanyabiashara wanakwenda kutoa rushwa badala ya kuingizia mapato Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wanatumia msemo mmoja wanasema wewe hujui kama ni Serikali ya Awamu ya Tano ya Magufuli hii, ni hapa kazi tu, hakuna namna yoyote utatoa na usipotoa tunakufilisi. Ndicho wanachowaambia wafanyabiashara, imefika mahala wafanyabiashara wameamua kusema sasa ngoja na sisi tuache. Wengine wanafunga biashara wanaona afadhali waende maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nirudi kwenye vitabu vya bajeti vya Waziri. Nakumbuka kwenye bajeti ya mwaka 2016/ 2017 fedha iliyokuwa imetengwa kwenye viwanda ilikuwa shilingi bilioni 45 lakini fedha iliyokwenda kwenye viwanda kutekeleza majukumu ya maendeleo ni shilingi bilioni 6.7 ambayo ni sawa na asilimia 8 ya bajeti yote. Hii inaonyesha ni jinsi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi inazungumza ndani ya Bunge lakini haijajiandaa kutengeneza viwanda na kuleta viwanda katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ni jinsi gani ambavyo utekelezaji wa bajeti umeendelea kuwa chini mwaka hadi mwaka na hatujui tatizo ni nini. Leo mnasema viwanda, viwanda haviji kwa maneno, viwanda haviji kama alivyokuja Mwijage na Kitabu kikubwa hapa. Viwanda vinakuja kwa kutenga fedha na fedha hizo kuzipeleka katika maeneo husika ili zikafanye kazi. Kwa hiyo, yote haya ni lazima yaeleweke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya 2017/2018 walikuwa wamepangilia kukusanya shilingi bilioni 28 kwenye Wizara lakini wamekusanya shilingi bilioni 6.6 peke yake. Hii inaonyesha hata uwezo wa kukusanya mapato kwenye Wizara yenyewe imekuwa ni chini kabisa. Yote haya yanafanyika kwa sababu ya kutokuwa na maandalizi ambayo yako sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.