Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimewahi kuhoji kwenye Bunge hili kwamba ni nani kati yetu atapewa mtaji wa shilingi milioni 250 a-raise mpaka shilingi bilioni 2 ndani ya miaka mitano? Hoja yangu ni kwamba mabenki mengi yamefungiwa baada ya kukosa vigezo vya kutimiza mtaji wa shilingi bilioni 2. Athari yake ni nini kwa uchumi wa nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi walikuwa wamewekeza pesa kwenye mabenki hayo na wakati wakisubiri process za insolvency maana yake watachukua muda mrefu sana ili waweze kuletewa fedha zao. Waliahidiwa kwamba kwa awali watalipwa Sh.1,500,000 kila mmoja halafu watasubiri process ya mfilisi mpaka itakapofikia mwishoni ndiyo waweze kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi iweze kuhakikisha kwamba inashusha riba ili watu wetu waweze kuwa na uwezo wa kurudisha mikopo katika mabenki yetu. Ukiangalia ripoti ya CAG inaonesha mikopo isiyolipika ilipanda kutoka shilingi bilioni 9.1 mpaka shilingi bilioni 2.5. Watu wengi kushindwa kulipa mikopo kwa sababu mbalimbali. Wapo ambao wanashindwa kulipa mikopo kwa sababu kodi za TRA zimezidi lakini wapo ambao wanashindwa kulipa mikopo kwa sababu sekta ya biashara na uchumi imezidi kudorora katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka napenda nizungumzie Special Economic Zone. Kuna suala zima la fidia ambalo limezungumziwa katika Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia hata kwenye sheria zetu, mfano Sheria ya Land Acquisition Act, section 15 inaelezea kwamba maeneo ambayo yamefanyiwa tathmini kwa ajili ya kulipwa fidia ya Special Economic Zone (SEZ) na Export Processing Zone (EPZ) yaweze kulipwa takriban shilingi bilioni 60 kwa mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi fidia zile zimefikia shilingi bilioni 190. Hiyo ni kwa sababu kila mwaka kwa mtu ambaye alithaminiwa na alitakiwa alipwe fidia ukipita mwaka mmoja kuna 6% kama nyongeza ambayo anatakiwa aongezewe. Kwa hiyo, kwa wananchi wote wa maeneo ya Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Kigamboni kwa maana ya Kurasini (Tanzania-China Logistic Center), Mara, Ruvuma na maeneo mengine yote, fidia imeongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu Serikali imeshindwa kulipa fidia kwa wakati na hivyo kuliingizia Taifa hasara na mzigo mkubwa kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka napenda kuitaka Wizara iwasaidie wawekezaji wetu kutoka nje. Kuna Tanzania Diaspora, tumeona hapa wenzetu Wachina na India, juzi hapa waliitishwa Wahindi wote waliopo duniani warudi India kwa ajili ya kwenda kufanya uwekezaji ambao utakaokuwa na tija. Wahindi waliopo Tanzania na wengine walitoka kwenye Bunge letu hili walienda India kuwekeza. Kwa nini Diaspora wetu ambao wapo nje ya nchi wenye uwezo mzuri, ambao wangeweza kuchangia uchumi wa nchi hii, hawawi included katika kuendeleza uchumi wa nchi hii?
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Nne iliweka Desk la Diaspora pale na walikuwa wameshaanza process hizi lakini mpaka sasa bado kimya. Ukiangalia katika Katiba pendekezwa ya Ndugu Warioba, Ibara ya 72, iliweka kipengele kwamba Watanzania ambao walibadili uraia kwa ajili ya kutafuta maisha wapewe special priority au hadhi maalum ili waweze kutambulika katika uchumi wa nchi yetu, waweze kumiliki ardhi, kuwekeza katika hisa na waweze kumiliki mali katika nchi yetu. Kwa hiyo, tunaomba tuweke desk maalum kwa ajili ya Diaspora ili waweze kujiunga vikundi kwa vikundi, waweze kuwekeza kwenye sekta za maji, kilimo, viwanda na kadhalika kwa sababu kuna Watanzania wenye fedha na wenye uwezo mzuri katika nchi za Arabuni, America na Ulaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni kabisa napenda nimalizie kwa kuzungumzia hali ya uchumi katika Mkoa wa Kigoma. Ukitaka kuhakikisha kwamba hali ya uchumi imekuwa mbaya, mwaka uliopita Mkoa wa Kigoma takriban miezi sita au mpaka saba wafanyakazi na wafanyabiashara wa maduka mbalimbali katika Mji wa Kigoma waligoma kufungua maduka kwa sababu walipandikiziwa tozo kutoka Sh.15,000 mpaka Sh.50,000 na Chama cha ACT Wazalendo. Hiyo inaonesha kabisa kwamba uchumi unayumba ndiyo maana watu waliamua kufunga maduka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Chama cha ACT Wazalendo walilikoroga akaja Ndugu Polepole akalinywa, alipoingia pale aliambia wananchi wanatakiwa wafungue maduka na kodi ile inashushwa. Kupandisha kodi ni mchakato wa sheria na ulifanywa kwa mujibu wa sheria na Baraza la Madiwani ndiyo lililopandisha na ikaenda Mkoani, TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri akaweka saini ikashuka, inakuwaje anakuja Mwenezi na kukataza kodi ile isilipwe?