Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia nami kuchangia katika hoja iliyopo mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona mahali Waheshimiwa Wabunge wanaliongelea eneo hilo basi Serikali ilifanyie kazi. Waheshimiwa Wabunge wengi wanaongelea TRA. Sasa hivi TRA ni eneo ambalo haliko rafiki na wafanyabiashara wadogo wadogo. Wameweka urasimu wa makusudi, siwezi nikasema ni wote, lakini maeneo mengi ya TRA sasa hivi ni eneo ambalo linawakwamisha wafanyabiashara wadogo wadogo, hivyo, siyo eneo rafiki kwao. Hili eneo litawakatisha tamaa wafanyabiashara hawa ili wasiweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosikia, unatakiwa kwanza wakutoze ushuru hata kazi hujafanya. Mama Ntilie anapika wali, hajajua kama anaweza akauza wali wake, umeshamwekea tayari, lipa shilingi milioni moja, anaipata wapi? Huu ni unyanyasaji wa kibiashara kwa wazawa.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kwenda katika Tanzania ya viwanda. Tanzania ya viwanda inahitaji mazingira wezeshi kwa viwanda. Enzi za Mwalimu Nyerere alianzisha maeneo ya viwanda na maeneo yale aliweka mazingira mazuri ya maji, umeme na barabara. Kwa mfano, alianzisha viwanda 14 vya korosho, hili nalirudia tena karibu mara ya tatu, viwanda vile vilikuwa na umeme, maji na ajira ya kutosha. Vilevile walikuwa wana uwezo wa kupata malighafi ya korosho palepale katika mikoa inayozalisha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ametaja mikoa yote ambayo imepewa kipaumbele cha viwanda; Lindi, Mtwara na Ruvuma sijaiona hapa. Kwa maana moja, hata hivi viwanda vya korosho vilivyopo, mategemeo ya kuvifufua hayapo. Ni aibu kiasi gani korosho inalimwa Tanzania inanunuliwa inapelekwa India, wanakwenda ku-process tunaletewa korosho ile iliyobanguliwa kuja kula tena Tanzania. Huu siyo mfumo mzuri wa kibiashara. Tunavyo viwanda vya korosho Tanzania lakini unavikuta vinapeleka korosho nje ya nchi as a raw material. Huu ni uharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda katika semina ya korosho, tunaambiwa Tanzania haionekani kabisa kama ni mzalishaji wa korosho, kwa vile tunaipeleka nje wale ndio wanaonekana wanazalisha na kusafirisha korosho. Je, tutapata lini ajira kama korosho yote tunaipeleka nje? Viwanda vyote vimefungwa. Cha kusikitisha zaidi, Mkoa wa Lindi hatuna kiwanda hata kimoja. Hivyo viwanda vya korosho vilivyokuwepo; vya Mtama na Lindi, vyote vimefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama Mheshimiwa Waziri ameikutia tu hii issue, ni makosa makubwa yalifanyika ya ubinafsishwaji na uwezeshaji. Uwekezaji wa nchi hii haukuweka mazingira mazuri katika mikataba, haukuweka mazingira mazuri kwa kujua nini tufanye katika kubinafsisha. Tumewabinafsishia watu, wamevifunga viwanda, watu walewale ndiyo wanapeleka korosho nje. Haiwezekani kabisa. Nataka utupe taarifa, ni nani wamechukua viwanda? Bado walewale waliochukua viwanda wanapeleka korosho nje, huu ni uhujumu wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na viwanda Tanzania ambavyo vinakamua mafuta. Mwanza tulikuwa tunapata Mafuta ya OKI, SUPA-GHEE, TanBond ya Tanzania ambayo hata Kenya walikuwa wanaipeleka, viwanda vile vyote vimefungwa, kwa nini vimefungwa na nani amevifunga? Kama ni mkataba, mkataba wake ulikuwa wa muda gani? Palikuwa na mikataba mibovu ambayo haikuwa na timeframe. Hivyo mtu amechukua kiwanda, amekifunga, anaagizia mafuta machafu kutoka nje wakati tunaweza kutengeneza mafuta masafi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni nini? Nafika mahali sielewi kama najielewa au pengine mimi niko nyuma ya wakati. Viwanda vya mafuta tunavyo. Nachingwea tulikuwa na viwanda vya mafuta, Mafuta Ilulu, ufuta wetu wote ulikuwa unakamuliwa Nachingwea. Leo ufuta wote wa Tanzania tunaupeleka nje, halafu hapa tunalalamika tuna uhaba wa mafuta wakati mafuta yetu mnapeleka mbegu nje, mnapeleka ajira nje na raw material inabakia kule na makapi yanatengeneza feed cake za wanyama. Huu ni uhuni wa kibiashara ambao umechezwa kwa muda mrefu, tunafanya biashara kwa mazoea, matokeo yake tunaiweka nchi katika crisis. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila inapofika karibu na Ramadhani wafanyabiashara wanaanza uhuni wao; mara hakuna mafuta, sukari, hii ni crisis ya makusudi wanataka kupandisha bei ili wananchi wapate ghadhabu na Ramadhani. Mfanyabiashara kupata pepo ni ngumu sana. Wanaangalia ni eneo gani nitafanya fujo yangu halafu watu watahamasika ili angalau hili litakuwa ni chachu kwa wananchi kulalamika hakuna sukari na mafuta. Nina imani sukari ipo, mafuta yapo, yatafutwe na wananchi wapate sukari na mafuta. Tumechoka kusikiliza uhuni wa kibiashara wa muda mrefu. Nchi haiendeshwi kwa uhuni wa kibiashara, nchi inaendeshwa kwa taratibu zilizopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii alizeti inapelekwa nje, magazi kutoka Kigoma yanapelekwa nje, wanachuja wanatuletea tena, ooh, tuna mafuta yako nje yamenasanasa. Kwa nini mmefunga viwanda vyetu vya mafuta na mmevizuia hamkamui mafuta, mnatuletea matatizo kibiashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kusema ubinafsishaji ndiyo donda ndugu la nchi hii. Tumefunga viwanda vyote. Tulikuwa na viwanda vya kusokota nyuzi. Kamati ya PIC tulikwenda Ubungo, eti hata nyuzi tunaagiza kutoka China. Tulikuwa na viwanda vya kusokota nyuzi Tanzania, pamba inatoka Mwanza na Shinyanga. Wenzetu, ndugu zetu, watani zangu Wasukuma wanalima pamba, ile pamba inabidi ipelekwe nje ikatengenezwe nyuzi tuletewe Tanzania wakati tulikuwa na viwanda vya nyuzi, tulikuwa na Kiwanda cha Mwatex na Kiwanda cha Kilitex. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, yeye ni mbuzi wa kafara, haya mambo ameyakuta. Naomba timu nzima ya Mawaziri irudi ikakae ituambie viwanda hivi viko wapi, vinafanya nini? Tupate database, nani wamechukua na kwa nini wanatuletea crisis ya mambo ya viwanda? Haiwezekani kila siku tunachukua khanga mbovu kutoka nje, madira mabovu kutoka nje, wakati Tanzania tulikuwa tunatoa khanga nzuri; Kenya na Uganda soko kubwa lilikuwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kusema sana lakini najiuliza, kulikoni Tanzania? Tumekuwa katika zigizaga, nenda mbele rudi nyuma, nenda mbele rudi nyuma. Viwanda hivi kwanza vingefanya kazi, basi hivyo vingine vingekuwa vya ziada kwa vile tayari ajira na uchumi ungekuwa mkubwa, lakini vile viwanda vikubwa vyote vimefungwa, kwa nini? Nani amevifunga, ni hao hao wafanyabiashara. Nataka utakapokuja kesho, uniorodheshee majina yote ya waliochukua viwanda na mpaka leo wamevifungia. Kwa nini wamevifungia na kwa nini nguo hazitengenezwi Tanzania? Kwa nini nyuzi hatusokoti Tanzania? Kwa nini korosho tunapeleka nje, tunaletewa tena zile zile hapa Tanzania? Kwa nini ufuta mnapeleka nje na tunakosa mafuta Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengine ya kusema, nataka jibu hilo kesho. Ahsanteni sana.