Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na ningependa kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ndani ya Bunge lako tukufu na niseme tu kwanza awali niwapongeze Waheshimiwa Madiwani wote kwa ujumla wao bila kujali itikadi zao wa Manispaa ya Bukoba kwa kufanya jambo la kihistoria siku ya juzi kwa kupitisha kwa kauli moja, wakapingana na kauli na njama ambazo zimekuwa zinafanywa na Mwenyekiti wa chama tawala, wa CCM kwa kutaka kudumaza mradi kujenga stand ya Bukoba kwa sababu ambazo hazina msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo ambalo ni la kihistoria kwamba sisi Bukoba kwa awamu hii tuliamua kwamba tunaweka siasa pembeni, tunapiga mzigo, wananchi wa Bukoba wanatoka katika historia za malumbano, wanataka mabadiliko ya Bukoba Town. Kwa hiyo, nawapongeza kabisa, kabisa na hususana Mwenyekiti wa caucas ya Madiwani wa CCM Mheshimiwa Richard, Mungu ambariki kwa kuonyesha kwamba sasa Bukoba imebadilika. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nitoe pole kwa vijana wa bodaboda wawili wa Kata ya Kashai ambao wanatokea maeneo ya Kisindi na Kashenye ambao wameuawa kinyama kwa kupigwa visu na mapanga na hivi sasa tunapozungumza hata wahusika hawajakamatwa, suala hili limewarejesha katika kumbukumbu za watu kutolewa koromeo kwa sababu vijana hao wameuawa, pikipiki haikuchukuliwa, pesa hazikuchukuliwa, helmet haikuchukuliwa. Ni jambo ambalo hivi sasa limewafanya vijana kuanza kulala saa mbili na kwamba hivi sasa ikifika saa mbili usiku Bukoba hakuna usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitoe pole kwa familia ya Mzee Kahigi ambaye ameondokewa na mtoto wake ambaye amepigwa risasi na watu wanaojidai kwamba wanaendesha programu au shughuli ya operesheni ya uvuvi haramu, yaani amepigwa risasi na matukio hayo mpaka sasa hivi polisi hawataki kutoa statement rasmi. Sasa masuala kama haya nakumbuka kwa Wizara zilizopita, watu wamezungumzia suala la amani na utulivu lakini Serikali imekuwa inapata kigugumizi kutaka kukubali hata kuleta Scotland squad waje watuambie tatizo liko wapi kwa sababu vyombo vyetu inaonekana vimeshindwa kung’amua matatizo yako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mheshimiwa Mwijage nimelizungumza hili ili na Mheshimiwa Mwigulu alijue, mazingira ambayo ni mema ya kuwekeza yanategemea amani ya mazingira yenyewe, sio kukata leseni peke yake. Pale ambapo Maafisa wa Ubalozi wanatekwa na kunyang’anywa kile walichonacho na kuumizwa ujue taswira mbaya inakwenda kwenye nchi za wenzetu na kwa wawekezaji kwa ujumla wao kiasi kwamba hata wawekezaji wataogopa kuwekeza Tanzania kwa sababu hakuna amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nataka kuzungumzia senene. Senene ni watamu kuliko nyama na ni kitoweo ambacho hivi sasa ni international, ukienda Dubai, London na Washington, sasa hivi senene zinakatiza, wanaliwa na watu wengi, ukienda Tanzania hii kila Mji Mkuu wa Wilaya wa Mkoa machinga hawezi kutengeneza hela kama hajafanya biashara ya senene. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwijage, nimetumwa na wanaumoja wa wauza senene Bukoba Mjini, wanasema hivi; wao hii biashara walianza tangu mwaka 2000 nilipokuwa Mbunge ya kuanza kuuza senene kwamba ni zao, niliwaelekeza kama ni fursa. Ikaanza kuuza Dar es Salaam kwenye mataa na nini sasa imevuka mipaka. Sasa wanasema, wanaomba uwaunganishe na TBS, TFDA, Sokoine University hata na wenzetu wa Ubalozi wa Canada ambao tumeona katika kitabu chako umesema kuna taasisi zinasaidia wajasiriamali wachanga, ili senene sasa kwanza zitangazwe kama ni zao ambalo lina ladha inayolika Tanzania nzima na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili wanataka sasa kuwa na senene ambazo ni standardized ambao wana ladha inayofanana ambayo mtu wa Washington akiwala basi wanafanana na yule aliyeila South Africa.

Kwa hiyo, kwa maneno mengine hizo Taasisi zilizoombwa tunaomba ziende ziwasaidie hawa wajasiriamali wa senene kwamba sasa hili zao wafundishwe namna ya processing, wasaidiwe namna ya packaging kimataifa ili zao hili liendelee kuwa fursa kwa wananchi wa Bukoba na wengine kwenye mikoa ambao wanakuja hawajui namna ya kuwakamata basi watu wa Bukoba watakwenda na kufunga mitambo ya kienyeji iliyoko Bukoba hivi sasa. Sasa viwanda vile vilivyoko Bukoba tunataka mwekezaji apatikane kwa njia yoyote ili aende kwa local industry ambayo imeanzishwa na iboreshwe tuweze kupata viwanda vya kisasa, vya ku-process, ku-pack senene vizuri ili tuanze ku-export kwenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi, watu wanaofanya biashara ya senene, wanajenga, wanasomesha, yaani senene ni product ambayo ni bora kuliko hata kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwijage umekuwa maarufu sana kwa hapa ndani ya Bunge kwa kauli zako kwamba mtu yeyote anayehitaji mwekezaji muonane nje ya Bunge umkabidhi mwekezaji aondoke naye kwenda jimboni. Sasa mimi siondoki kwenye Bunge hili, nitakuomba unipe mwekezaji, awe wa Kichina, wa Kijapani, mimi niende naye tuangalie mikakati ya kukamata senene. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa pointi hiyo usemi wa Kireno unaosema batakusiima kwiluka ukalabauliembo mwanyu. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo maana yake ni kwamba usisifiwe kufanya kazi sana kabla hujaangalia mazingira ambayo yanakuzunguka. Hiyo ndiyo tafsiri, nafikiri ameelewa.