Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ukilelewa kwenye vyombo hivi toka udogo wako, unajua nchi ilivyokuwa imara na ilivyokuwa salama. Mimi nilijiunga na Jeshi la Anga wakati nina miaka 18 tu na katika umri wangu mpaka nakuwa mtu mzima nilikuwa katika vyombo hivi. Kwa hiyo, najua umuhimu wa vyombo hivi na ulinzi ambao nchi hii sasa hivi unao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyoweka kipaumbele masuala ya ulinzi wa nchi yetu. Siyo kila kitu Kamati inaweza kuleta kwenye Bunge kuzungumza mambo ya ulinzi, lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, nchi iko salama na kuna mambo makubwa yanafanywa na Serikali kwenye vyombo hivi katika mambo ya kiusalama ambavyo vinafanya Taifa letu kuogopwa katika nchi ambazo zimezunguka. Demarcation za nchi zetu zinalindwa na vyombo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshi letu lina uwezo wa rapid deployment forces, any time any place nchini mwetu, lakini nidhamu ndani ya Jeshi ni kubwa sana. Nampongeza CDF, Chief of Staff na Makamanda wote wa JKT na Makamanda wengine kwa namna wanavyoweza kuhimili na kusimamia ulinzi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshi sasa lina utaratibu wa vifaa kama mavazi, kushonwa nchini Tanzania. Tutaokoa pesa nyingi sana za kigeni badala ya kuagiza uniform ambazo zimeshashonwa nje ya nchi. Napongeza sana utaratibu ambao umewekwa na Serikali, Mheshimiwa Rais, Waziri na Jeshi lenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya Naval Base Kilwa ni kipaumbele kikubwa sana cha Kamati na Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko ndani hapa. Mahsusi kwenye Kamati ya Bajeti nimejenga hoja hii, pesa zinazohitajika ni shilingi bilioni 3.6 tu. Tuchukue kituo hiki licha ya kuwa ni cha ulinzi kitakuwa na uwezo kuwa na commercial activities.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa sana za dry dock, za seaworthiness ambazo meli nyingi zinahitaji Tanzania, zinakwenda kutengezwa nje ya nchi. Tumezungumza na Naval Commander watakuwa na uwezo wa kuweka dry dock katika eneo hili iwe kitega uchumi kikubwa sana cha vyombo hivi vya ulinzi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, aone kuwa anawekeza katika sehemu ambayo watakuwa na own source na uwezo wa kuwa na mahitaji yao kwa siku za mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tamaduni za nchi nyingi; ukienda Pakistan, wana kitega uchumi, kama sisi hapa tunayo hii National Housing Corporation. Ukienda Pakistan, National Housing Corporation ya kwao iko chini ya vyombo vya ulinzi ili waweze kujihimili na mahitaji muhimu. Umeona hapa Majenerali waliostaafu malipo yao yanachelewa. Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone umuhimu wa kuweza kulipa hizi pesa ili kituo hiki kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilibahatika kuwa katika Kamati hii toka Bunge la Tisa, la Kumi na sasa la Kumi na Moja. Kuna issue ya Sera ya Ulinzi, bado inaelekea upande mmoja wa Muungano hawajairidhia na kuipitisha. Tunaomba Serikali zishirikiane, pande zote mbili hizi wakae, wamalize ili sasa National Defence Act iweze kupitishwa na iwe dira ya kuweza kusaidia maslahi na mambo mbalimbali ya ulinzi katika nchi yetu. Mheshimiwa Waziri wa Nchi yuko hapa, ajaribu kuzungumza na upande wa pili waweze kumaliza haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Jeshi kwa mwaka huu ni shilingi trilioni tatu, lakini ceiling waliyopewa iko chini ya hiyo shilingi trilioni tatu. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone umuhimu. Jeshi wakati wa amani linakuwa ni jeshi la uchumi. Chombo hiki, ni jeshi mashine. Kwa hiyo, naomba, najua amenipa dakika tano na sina nia ya kuzungumza mambo mengi sana, nisije nikasema mazuri ya ulinzi ambayo nayajua halafu yakaharibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waziri wa Fedha ashirikiane na chombo hiki kusaidia Jeshi hili liweze kufanikisha mahitaji yake kipesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya machache, naunga mkono hoja.