Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Salum Mwinyi Rehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa kwa mara ya kwanza leo hii kuweza kuchangia katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ninalotaka kuchangia ni suala zima la fidia katika maeneo yetu mbalimbali ya Jeshi la Ulinzi Tanzania. Kwa kweli hili limekuwa dondandugu na nimwombe sana Waziri wa Fedha, Jeshi limeshaomba bilioni 20.9 zaidi ya miaka mitatu hazijapatikana. Kuna mizozo mikubwa inaanzishwa na inakuzwa kutokana na kutokulipwa fidia katika maeneo mbalimbali ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata kuzunguka katika kila eneo unapouliza juu ya fidia unaambiwa, tulipokwenda Mtwara tumeambiwa, Songea kuna madai mengi tu ya maeneo ya wananchi, Bukoba, Mbeya, Zanzibar, kila eneo kuna madai haya. Kwa hiyo, niombe Waziri wa Fedha hili liwe moja kati ya vipaumbele vya kumaliza migogoro baina ya wananchi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nataka kuzungumza suala la Jeshi kuongeza maeneo ya shughuli zao. Niwaambie tu kwamba kwa hali ilivyo sasa hivi, it’s too late. Kwa sababu maeneo ambayo wanataka kuyaongeza tayari wananchi wameshakaa na wananchi walikaa zamani sana wao wanalijua hilo. Sasa leo kitendo cha kwenda kuwaondoa wananchi wakasema tunaongeza sehemu hii wakati eneo lile hata kama wataongeza itakuwa wao wenyewe wameshajiingiza ndani ya wananchi ni kujitengenezea migogoro isiyokwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawasihi sana, yale maeneo ambayo tunataka kuyachukua ambayo yalishachanganyika na wananchi kwa kiasi kikubwa sana, ni bora kuyasamehe na kuweka uzio katika eneo ambalo litakuwa salama zaidi kufanya shughuli zao kuliko kujichanganya na wananchi ambapo matatizo mengi baadaye yanaweza kuzuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linanasibishwa na mfano wa eneo ambalo liko katika Jimbo langu la Uzini, eneo la Kambi ya Ubago, eneo la Kidimni, eneo ambalo wananchi wamekaa toka miaka ya sitini wako pale, lakini juzi wanakuja kuibuka viongozi wa Jeshi na kupiga X kuanza kuwatisha wananchi na kuwaambia kwamba wahame katika eneo lile wakati eneo lile lilikuwa la Wizara ya Kilimo, nami najua mpaka makubaliano waliyopewa wananchi na Wizara ya Kilimo kukaa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naliomba Jeshi sana na nalisihi sana, kwa eneo lile it is very sorry kwa sababu wamechelewa, wananchi wameshakaa pale na kwenda kuwahamisha wananchi wale ni kuongeza fidia nyingine wakati hizi za nyuma bado hazijalipwa. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri katika majibu yake tupate kauli ya Serikali na ya Wizara juu ya eneo ambalo linataka kuchukuliwa na Jeshi wakati wananchi wameshakaa katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa hakuna uendelezaji wowote unaofanywa katika eneo lile kwa sababu kumepigwa X na Wanajeshi wale ambao wanapita kila siku kuwatisha wananchi, wengine wanapigwa, wengine wanazuiliwa kufanya shughuli zao, naomba wapate uhuru wa kufanya shughuli zao na Jeshi mipaka waliyokuwa wameiweka toka miaka ya 1975 na 1980 na mwisho 2005 iheshimiwe na waweze kufuata ile mipaka ya zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumza ni suala zima la Jeshi kuanza uwekezaji sasa hivi. Tuondokane na mawazo ya zamani kwamba Jeshi kazi yake ni kushika bunduki, kulinda mipaka na shughuli nyingine za Kijeshi. Majeshi mengi sasa hivi duniani yanakwenda kwenye mtindo wa kisasa kuweka uwekezaji na kujiendesha yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahali pekee Jeshi linaweza kufanya uwekezaji ni suala la kuweka dry dock ile ambayo iko kule Mtwara, eneo lile litaweza kufungua pato kubwa ndani ya Jeshi la Wananchi kwa sababu naamini wazi kama tutaweza kujenga ile bandari, niiombe Serikali, tutafute fedha tulipe fidia, bilioni 3.6, lakini isitoshe, tutafute fedha tukope tuwekeze pale. Tukiweza kuweka dry dock pale ya samaki, kwa mfano bandari ya uvuvi ikiwekwa pale, meli zote zinazotaka kufanyiwa fishing inspection zitakwenda pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, meli moja kuifanyia inspection ni dola 6,800, lakini meli moja ikija pale kuchukua mzigo tu wa kuweza ku-feed wavuvi ambao watakaa ndani ya bahari kwa muda wa miezi mitatu, ni zaidi ya milioni 45 hadi milioni 60, hicho ni kipato kikubwa! Kwa nini, tukatafute fedha nyingine, kwingine za Serikali wakati vyanzo vya kupata pesa vipo?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pale panahitajika pawekwe karakana ambapo kama kuna kifaa kinahitajika kuchongwa kichongwe na Wanajeshi wetu, JKT watapata nafasi. Pia kiwanda cha chumvi katika eneo lile ndiyo penyewe, kwa hiyo fursa zipo nyingi. Niwaombe sasa hivi waanze kubadilika na wawe na mtazamo chanya wa maendeleo zaidi wa kujiwekeza kwenye uzalishaji pamoja na shughuli za ulinzi zikiwa zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuchangia katika eneo hili, ni suala zima la makazi ya Wanajeshi wetu. Bado kuna tatizo kubwa katika maeneo yetu, Wanajeshi kweli wanakaa katika nyumba ambazo bado hali zake ni mbaya na nyingine zimejengwa toka miaka
ya sabini, hazina ukarabati, hazina miundombinu yoyote, zimechoka. Kwa hiyo, niombe kwa kweli Kitengo hiki cha JKT kisiwe tu kinajenga katika maeneo mengine lakini kiwezeshwe fedha za kujenga au kufanya ukarabati katika maeneo ambayo wanakaa Wanajeshi wetu ili na wao waishi kama maafisa wengine wa ngazi mbalimbali wanavyoweza kufanya shughuli zao kwa raha na wajisikie kama kweli wako kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Waziri hili nalo alitilie mkazo na atoe kauli kwamba sasa hivi mwelekeo wao ukoje katika ukarabati na ujenzi wa nyumba za Wanajeshi wetu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala zima la muda wa kuondoka kazini Wanajeshi wetu. Suala hili kuna manung’uniko mengi ya Wanajeshi wetu, muda wanaoondoka ni mwingi na wanataka kujua sheria gani ya utumishi inawafanya kuingia kazini saa 12 asubuhi na wakatoka saa 12 jioni. Kwa hiyo, hili lazima Mheshimiwa Waziri atupe maelezo ili na wao waweze kuridhika, kwa sababu wao hawana mahali pa kusemea, wanatuma wawakilishi wao waweze kuwasemea, katika hili tupate maelezo kitu gani kipo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nataka kuzungumzia juu ya maendeleo ya SUMA JKT na shughuli wanazozifanya na vijana ambao wanakwenda katika maeneo yale. Wenzetu wengine wamelidokeza kwamba bado vijana ambao wanatoka katika maeneo yetu ni wachache, vilevile ile recruitment inayofanyika kwa kweli inakuwa ina figisufigisu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza vijana hawa kuweza kupatiwa skills maalum za kuweza kujiendeleza kule wanakokwenda. Hii ni kwa sababu siyo wote wanaokwenda kule wanafaa kuwa Askari, wengine wana vipaji mbalimbali na kazi mbalimbali za mikono, wanaweza kwenda kuwekeza. Kwa hiyo, wazo langu ni kwamba, JKT iweze kuwa na skills maalum kwa vijana ambao wanakwenda kule wakitoka pale waweze kwenda kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba ikiwezekana watoke pale basi wengine wapewe kits za kuweza kwenda kuanza maisha katika maeneo yao na siyo kwenda pale kila mmoja kutegemea kwamba apate ajira ya Jeshi au Polisi au Magereza au kazi nyingine. Wale vijana kule wakikusanyika mambo mengi wanaweza kuyabuni, wakaweza kuyafanyia kazi na wakaweza kutoka pale na ujuzi wa aina yake wakalisaidia Taifa hili kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante.