Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai ambapo sasa wote tuko hapa tukizungumzia Jeshi letu, lakini zaidi sana nawaombea na naliombea Jeshi hilo lizidi kupata nguvu na kutulinda kama linavyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa na chombo makini kama Jeshi hili. Nampongeza CDF na pia nawapongeza wale wote waliomuunga mkono ambao ni wastaafu akiwemo Major General Mboma, Major General Waitara na Major General Mwamunyange. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri leo ametuletea hapa hotuba ambayo ni fupi, inaeleweka na inakubalika, naomba nimpongeze sana Waziri wetu, nimpongeze Katibu Mkuu na timu yake yote walioandaa kitabu hiki, nimeshakisoma kama mara tatu, pamoja na ile ya Kamati. Niseme wazi kwamba mimi niko kwenye Kamati hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumepata elimu siyo tu kwamba wametoa kuomba fedha lakini tumepata pia kama semina. Sasa ninachoomba hapa, kama walivyosema pia wa upande mwingine hela hizi wapewe zote na hata kama nyingine waliogopa basi waongezewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la kwanza; Serikali iwalipie wanajeshi hawa bili yao ya umeme na maji wanayodaiwa kwenye vyombo vingine kama vile taasisi za maji na umeme, TANESCO. Inakuwa fedheha Jeshi linapodaiwa vitu vidogovidogo ya nini? Kule hawathubutu kuwakatia, ile lugha haitembei pale kwa sababu wao wakitugeuzia kipande raia hatuna hamu. Naomba namna gani ya kulipa hayo madeni ifikiriwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani zangu kwa Jeshi hili kuwa wakarimu kwa ile Hospitali ya Lugalo. Kwa kweli hawatibiwi wenyewe tu hata sisi wananchi ikizidi sana wanatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo halinipi amani ni ajira za Jeshi kwa Jinsia ya Kike ni pungufu. Leo tumewaona walivyopendeza huko nje, walivyo nadhifu, na imara, lakini ukiangalia wanawake ni wangapi, sikuona, nimemwona tu raia mmoja wa Jeshi kule. Naomba wanavyotoa ajira mpya wanawake wafikiriwe, inapendeza. Mbona nchi nyingine zina Wanajeshi wa ngazi ya juu wanawake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT inalitoa Jeshi kimasomaso. Waliwahi kupewa tenda ya kutengeneza madawati, walitengeneza kwa wakati na madawati yakapatikana kwa ile hela iliyokuwa imerejeshwa. Wamepewa kutengeneza ule ukuta wa Mererani, wamefanya kwa wakati. Naomba taasisi zote zitoe kazi kwa JKT, ikianzia Bunge kwa hivi viti tunavyokalia. Wanatumia mbao nzuri, wanatumia mninga na pia wanatumia soft. Pia na ninyi ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, naomba zile furniture zenu mnazoagiza za kuishi Dodoma muwape JKT wawatengenezee na watawaletea kwenye milango yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tunapowafikiria mafao yao wanapata kwa wakati, lakini zile pensheni haziji kwa wakati na pensheni ni kitu ambacho mtu anatakiwa akipate baada ya jasho jingi na kazi ngumu na kukung’uta saluti nyingi sana nao wafurahie sasa. Naomba wafikiriwe sana wale viongozi wapatiwe zile pesheni zao waweze kuzifaidi kabla hawajazeeka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba pia Wanajeshi ambao ni wanamichezo waweze kupatiwa ruhusa kwenda kwenye michezo au kwenda kwenye mashindano kama yale ya Kili Marathon, tumeona mara nyingi wanakuja Wakenya wanachukua zawadi nyingi Kili Marathon ni International Marathon ikikaribia Kili Marathoni ule Mji wa Moshi unakuwa Wazungu tu, watu kutoka nje. Yanapofika yale mashindano hakuna Mtanzania anayesogea hata nafasi ya tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Jeshini tuna vijana ambao wana uwezo, naomba ikiwepo Kilimanjaro Marathon, ikiwepo Tulia Marathon, ikiwepo KIA Marathon Wanajeshi wetu wajiandae kuja kushiriki kwenye marathon hizo wachukue hizo zawadi, sioni kama kuna tatizo, wanajeshi wana uwezo mkubwa sana wamekuwa wakishinda sana wanajeshi kwenye netball najua kabisa kuwa hata hiyo wataweza na watashinda na watachukua zawadi nyingi ambazo zitatupa heshima kila mahali na pia watatutangaza nchi yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Jeshi kwa kutoa demo wakati wa sherehe za Uhuru, wakati wa sherehe za Muungano, tumeona tukioneshwa vyombo vyetu vifaru, tumeona tukioneshwa vyombo vyetu vya vita, tumeona tukionesha makomandoo walivyo na uwezo. Kwa kweli vijana wanasema hakuna Jeshi kama hili, siyo vijana wa nchi hii tu hata nje ya nchi hii tunajua Jeshi hili lina nguvu. Tunaomba waendee na pia waendelee kuwa kivutio kwa vijana kujiunga na Jeshi, vijana wetu wengi wanapenda kuwa Wanajeshi lakini wanakuwa na hofu ila wakiwaona katika kufanya vile vitu vyao vile vizuri zuri vile, wanasema na mimi siku moja nitakuwa Mwanajeshi na nina hakika watafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wanapofanya miradi yao waombe na hela za kukarabati miradi hiyo. Nitatoa mfano wa mradi mmoja, juzi wamejenga ukuta wa Mererani, ukuta ule japo umekabidhiwa lakini watatakiwa wauone kwamba ukuta ule unabakia kuwa imara siku zote. Sioni bajeti yoyote ya kusema kwamba hii ni ya ukarabati wa ukuta wa Mererani hakuna kitu kinachoishi maisha kama hakitunzwi. Kwa hiyo, naomba watakapoleta bajeti yao ya mwakani waombe na hilo fungu la kukarabati lile eneo la Mererani ili sifa zao ziweze kubakia na uimara wake uweze kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijamalizia nisije nikasahau kuunga hii hoja mkono, hii kwangu ni hoja muhimu sana. Niliwahi kupitia huko Jeshini kwa mujibu na nilikuwa kwenye ile operesheni aliyokuwa Almasi, operesheni Kagera na namba yangu ni K7078 mimi Mwanajeshi tukiitwa leo ni vita imetokea mimi Frontier Soldier hata kwa umri huu. Tulikuwa na wimbo mmoja unasema “hilo Jeshi mambo yake, vitendo vyake sawasawa” na leo mmeona nadhani kila mmoja leo alikuwa na amani kuwa na Jeshi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu ndugu zangu huo mshahara wa Waziri yoyote akayesisima nadhani atakuwa yeye anasumbuka sana. Tunaomba tuwapatie na iwe ni ya mfano kwamba hakuna usumbufu. Niishie kwa kuwaomba sana wao Wanajeshi wetu waendelee kutulinda tunawapenda, tunawaheshimu, tunawafurahia na kila wakati tunawaombea kwa Mungu na kila wakati tunaamini kwamba wakiwepo hakuna mtu anayethubutu kuleta usumbufu wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naomba kuwasilisha.