Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa JKT, Makamanda wote wa vikosi, Maofisa, Askari, Taasisi zote zilizo chini ya Jeshi na Watendaji wote walioshiriki na kufanikisha kazi nzuri katika jeshi la letu. Nichukue fursa hii kuwapa pole kwa vifo vya wanajeshi wetu waliopoteza maisha wakiwa katika ulinzi wa amani nchini DRC, Mwenyezi Mungu awape pumziko la amani na milele. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limekuwa ni msaada mkubwa na tegemeo la Watanzania, jeshi letu limeshiriki katika ukombozi wa Kusini mwa Bara la Afrika, (Zimbabwe, Msumbiji, Angola, Namibia), Afrika Kusini na kadhalika. JWTZ limeshiriki kumpiga Nduli Idd Amin Dada aliyevamia nchi yetu Mkoani Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo ya ulinzi wa nchi yetu JWTZ limeshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na hata kusaidia kuwaokoa wananchi pale wanapopatwa na majanga mbalimbali kama, matukio ya Lindi na Mtwara mwaka 1990, kuzama kwa meli ya MV Bukoba, kuzama kwa meli ya MV Spice Island 1-Zanzibar, ajali ya Treni-Dodoma, mafuriko ya Kilombero, madaktari wa kijeshi kutibu raia (dharura), mlipuko wa mabomu ya Mbagala na Gongo la Mboto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshi limetumika kufanya kazi kwa ufanisi na uadilifu mkubwa na kwa wakati. JWTZ limeshiriki kusomba mbolea kupeleka mikoani, JWTZ limeshiriki pia kusomba vitabu kuvigawa mikoani. Jeshi limeshiriki kusaidia kuokoa wananchi pale wanapopatwa na ajali za barabarani , majanga ya moto na mafuriko mbalimbali. JWTZ limekuwa ni tegemezi la Watanzania na hata nchi za Bara la Afrika lina heshima na kuthamini mchango wa jeshi letu, kwa sababu zote hizo na nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itenge fedha nyingi zaidi kwa majeshi yetu ili waweze kukidhi mahitaji yanayoendana na hali ya sasa na matishio ya kigaidi kwa kutenga fedha za mafunzo yanayoendana na teknolojia za kisasa kwa kuwapelekea vijana wetu nje ya nchi kupatiwa mafunzo na mbinu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kununua vifaa na mitambo ambayo inaweza kung’amua au kutambua viashiria vya hatari kabla ya mashambulizi (mfano DRC) ugaidi. Ziara za Kimataifa kwa makamanda za mara kwa mara ili kujifunza mambo mapya ya kiulinzi, kujenga makazi ya Askari wote kwa kuomba mkopo wa nyumba wa muda mrefu na kwa riba nafuu ili kukidhi mahitaji ya Askari wetu, ambao ndiyo tegemeo la Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT ipewe fedha kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa kwa kilimo cha alizeti, ufuta, mchikichi na mazao ambayo yanatoa mafuta na kufanya hivyo kutasaidia kuondoa tatizo la upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini. JKT ina rasilimali ardhi kubwa, watu na uongozi imara utakaoweza kufanikisha kilimo hicho. Kwa kufanya hivyo kutasaidia JKT kuingiza fedha zitakazotokana na mauzo ya mbegu za mafuta au kuanzisha viwanda vya kusindika mafuta ya kula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.