Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. AIDA J. KHENAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa aliyemaliza amesema anaunga mkono hoja lakini amezungumzia suala la mahindi, mimi nasema mapema kwamba siwezi kuunga mkono hoja wakati wananchi wangu mahindi yanaoza yako nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbolea, tumezungumza suala la Mfumo wa Pamoja wa Kununua Mbolea, nataka nimwaambie Waziri na Wizara kwa ujumla kwamba, mfumo huu ume-fail, haujafanikiwa hata kidogo. Mkafanye tathmini upya juu ya ugawaji wa mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa Mkoa wangu wa Rukwa, juzi tulikuwa kwenye semina mkazungumzia Minjingu, yaani kwetu Minjingu tunaichukia kama ugonjwa wa UKIMWI. Imeleta umaskini kwa wakulima na imeleta shida kwa wakulima wetu. Kwa hiyo, kama lengo la Serikali ni kujenga viwanda, waiteni wawekezaji waje kuzalisha urea, waiteni wawekezaji ambao watakuja kuangalia hitaji la wakulima wanataka nini, Minjingu Mkoa wa Rukwa hatuihitaji, labda kama mtarudi kufanya maboresho ya mbolea hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la bei elekezi. Bei elekezi ni kizungumkuti tu. Mkoa wetu wa Rukwa mbolea imekuja kwa bei tofauti na ile ambayo ilikuwa imepangwa. Kwa hiyo, niseme tu kabla hamjatoa tamko lolote au kuzungumzia bei elekezi kama hamna uhakika muache kwanza mkafanye tafiti badala ya kuwaletea ugomvi wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi tamko la Serikali linatoka hapa la kuzuia kuuza mazao nje ya nchi, Sumbawanga Mjini bei ya gunia ilikuwa Sh.70,000, hivi ninavyozungumza leo gunia la mahindi Mkoa wa Rukwa ni Sh.18,000 mpaka Sh.24,000. Naomba niwaambie tu Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama mmeamua kwamba zao la mahindi halifai njooni na zao mbadala badala ya kuwafanya wakulima wawe maskini. Kama hamna zao mbadala muwaambie kwamba wao ni Watanzania au wanatoka nchi gani? Mbolea mnaleta kwa kuchelewa, yaani wakati tunahitaji mbolea za kupandia hamleti, wakati tunahitaji mazao yakue ndiyo mnaleta mbolea ya kupandia kwa hiyo mnakwenda vice versa tena kwa bei tofauti na ile ambayo mlikuwa mmepanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niiambie Serikali, kama nia yetu ni kujenga viwanda, kama mnavyosema kauli mbiu ni kujenga viwanda, mambo yanayotendeka na Wizara ya Kilimo ni tofauti na kauli mbiu. Huwezi kujenga viwanda umeshindwa kutengeneza mazao ambayo unajua ndiyo ambayo yanakwenda kuzalisha hivyo viwanda vyenu mnavyovizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo yanasikitisha sana. Leo unapozungumzia kilimo ambacho kinaajiri watu wengi kwenye Taifa hili ndiyo mmepeleka asilimia 18. Tunaomba Waziri utakapokuja hapa utuambie nini kilitokea mpaka mkapewa asilimia 18. Mkumbuke kwa kuwa, ninyi ndio mlizuia wananchi wasiuze mazao yao nje ya nchi yale mazao yao ya mwaka jana kwa sababu tunaenda kwenye msimu mwingine wa mavuno, ambayo ninyi ndio mlisababisha wao wakashindwa kuuza, mnayafanyaje? Mnayanunua au mnawaruhusu wapeleke sehemu nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kizungumkuti kidogo kwenye suala la mawakala. Bajeti ya 2015/2016 ilikuwa ni shilingi bilioni 35, kwenye chombo chao cha mawakala wanazungumza kwamba hilo ndiyo deni, lakini watu wenu kwenye Wizara wanasema ni shilingi bilioni 67 na ndiyo maana mpaka sasa hivi hamjawalipa mnaendelea kuhakiki. Sasa tunata Waziri atakapokuja atuambie ipi ni sahihi? Kwa sababu, kama bajeti ilikuwa shilingi bilioni 35 hiyo shilingi bilioni 67 imetoka wapi na hizo vocha zilitengenezwa kwa pesa gani? Zile vocha zilizorudi zimerudi kwa nani na kwa utaratibu gani? Waziri atakapokuja hapa atuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kutengeneza vocha zaidi ya bajeti ilivyotengwa, lazima uendane na bajeti. Kwa hiyo, kama kweli mna hakika mnashughulikia mafisadi tunataka uwazi wa jambo hili, ni kipi kati ya shilingi bilioni 35 na shilingi bilioni 67?