Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba hii ya wananchi wanyonge walioko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitatu mfululizo katika zao la pamba tumekuwa tukipata bei nzuri. Mwaka 2016, 2017 na 2018 na tumevuka kiwango mpaka tumefanikiwa kuzalisha takribani kilo 600,000, haya ni matarajio ambayo tunayatarajia. Hii ni kwa sababu wananchi wamehamasika kwa sababu ya kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uzalishaji wa zao hili la pamba, linaweza likaipatia nchi kipato kikubwa sana. Kwa mwaka huu wa fedha tunatarajia kuwa na Dola za Kimarekani takribani 342 lakini kadri tunavyokwenda na taratibu ambazo Serikali yetu ya Awamu ya Tano ilielekeza, namshukuru Mbunge aliyemaliza kuchangia Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba tuwe na ushirika kwa ajili ya kukomboa wanyonge, nataka nikuhakikishie ushirika unaotengenezwa siyo ushirika ambao tunaufahamu, ni ule ushirika wa miaka yote ya nyuma. Ni watu ambao walishachoka tangu miaka 23 na mwaka huu kama tutawakabidhi huu muziki wakulima wetu wataendelea kupata adha kubwa sana. Ningeiomba Serikali ijaribu kutengeneza upya mfumo wa kuhakikisha kwamba zao hili la pamba linanunuliwa vizuri na kwa umakini mkubwa zaidi. Hata go-down walizonazo zilishauzwa, ushirika uliobaki kule ni ushirika ambao ni hoi bini tabani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unatoka katika Wilaya ya Bariadi unayo majimbo mawili, Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Vijijini, ushirika uliopo katika kijiji chenye watu 2,000 kuna washirika watatu, wanne na leo tunataka kwenda kuwakabidhi fedha za wakulima wetu. Niiombe
Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi, kilio hiki iende ikakifanyie kazi upya kuliko hivi sasa ndiyo wanahangaika kule vijijini wanaunda vikundi na hizi ni fedha za watu na mabenki inabidi benki hizi zirudishe fedha na kipato cha ndani kiendelee kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zima la pembejeo. Tumeshuhudia mwaka huu Mheshimiwa Waziri amefanya kazi nzuri pamoja na watendaji wa Bodi ya Pamba kwa kuhakikisha ametutoa tulipokuwepo na kutufikisha hapa tulikofikia. Matarajio yetu tukiendelea kusimama vizuri na kuimarisha zana zetu katika maeneo yetu ya kilimo cha pamba, katika hotuba yake amesema ifikapo mwaka 2020 tutafikisha tani 1,000,000, naamini bei zikiendelea kuwa nzuri na pembejeo zikiwa za kutosha ifikapo mwaka 2020 tutazalisha tani milioni 2.4. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu mikoa inayolima pamba ni 17, tunazo wilaya 56 utaona tu kwamba hata uzalishaji tulionao kwa mwaka huu tumepiga hatua. Ukigawanya wastani wake ni kama kila wilaya imezalisha tani 10 ambapo tukisisima sasa jukumu hili tukalibeba wote Serikali pamoja na Wabunge kwa kuhamasisha na kuunda AMCOS zilizosajiliwa kwa mwaka huu uzalishaji utaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Waziri Mkuu kutoa agizo Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwenda kuunda vikundi kilichofuatia ni Mrajisi kwenda kutengeneza ushirika wake wa miaka 20 ambao umefilisi wananchi wetu na bado watu wanauchukia hata sasa hivi ukisema ushirika wanakimbia. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliangalia suala hili kwa mapana zaidi, zana ni nzuri lakini si nzuri kwa kipindi ambacho tunakitarajia hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 146, hapa napata kigugumizi kusema, ametuandikia ameamua kufuta Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba lakini kwenye kukotoa huku kuna Sh.100, sasa angetupa majibu tunafanya kitu gani? Hizi fedha zikienda kwa mkulima moja kwa moja bei zinaongezeka. Kwa hiyo, naomba sana hili suala la pembejeo Waziri ahakikishe linakuwa katika mipango mizuri ili wakulima wetu wasiendelee kupata adha ambayo wanaendelea kupata kwa mwaka huu tunaoumaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu tutakapoweka usimamizi na uzalishaji mzuri wakulima wetu wa pamba hawasukumwi kwa sababu ni wajibu wao na ni biashara yao lakini tunavyotaka kwenda tunaweza tukatengeneza mazingira ya kuua zao la pamba na litafia hapa Dodoma. Kwa mwaka 2020 tunarajia kuvuna tani 1,000,000 lakini kwa mfumo ambao ameuleta Mheshimiwa Waziri hatutafikia huko, wakulima wataacha kulima kwa sababu hii miti wanalima kwa mwaka, wanakata wanazalisha tena upya. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atafute mfumo ambao ni mzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo linatuletea masikitiko makubwa sana. Sisi kule kwetu tulikuwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha SHIRECU lakini baada ya Ofisi ya Mrajisi kuingia pale alitengeneza madudu mpaka na go-down zetu kubwa zilizokuwa maeneo ya Dar es Salam ziliuzwa lakini leo Mrajisi huyu amerudi tena na mifumo ambayo badala ya kuishauri Serikali alete utaratibu mpya utakaokuwa na tija kwa wakulima ameleta system ileile ambayo imewatesa wakulima wetu na imewakatisha tamaa. Watu wengine, Mwenyekiti utakuwa shahidi wakati wa kampeni za kuomba kura, watu walikuwa wanakuomba malipo yao ya pili. Kwa hiyo, naomba jambo hili tulichukulie katika misingi mizuri ambayo ina tija lakini kubwa zaidi ni kuweka mifumo itakayokuwa rafiki na wakulima ambao wanazalisha bila kusukumwa na kwa moyo mzuri na ni kwa sababu wanapata pesa nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshauri Waziri aweke mpango mzuri utakaotuwezesha kupata pembejeo na mbegu bora. Niwashukuru sana watafiti wetu wa Ukiliguru kwa sababu kwa mwaka huu fedha tunaenda sasa kuingia kwenye mbegu za asili ambazo wamezizalisha, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nishauri tuendelee kutunza mbegu zetu za asili. Hili jambo tusipoliangalia ni tatizo na janga kubwa. Wakulima wetu wanahamasika sana kulima, nimeona humu ndani kwenye kabrasha hili kuna mikoa mipya imeanzishwa. Mikoa mipya iliyoanzishwa kama mfumo wetu hautakaa vizuri, nataka nikuhakikishie tutapata madhara makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi tunao, mwaka 2008/2009, Serikali ya Awamu ya Nne ilitoa fedha kwa ajili ya kufidia wakulima takribani shilingi bilioni 2 lakini zile fedha zilitumika ndivyo sivyo. Leo hii Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani bei zimeendelea kuongezeka kila siku, sasa kuna mdudu ambaye ameingia huyu sijui katoka wapi. Naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa hili atuwekee utaratibu utakaokuwa rafiki kwa wananchi wetu na tusiwe na maswali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna meseji kibao za wananchi wanalalamika kwamba Bunge lilitangaza tarehe 1 lakini mpaka leo hakuna na wamefungua kijiji kimoja pale Igunga kilo 3,000 zilizonunuliwa, hakuna mtu yeyote aliyeingia mule ndani lakini hata maandalizi hayapo, hata msimamizi wa Bodi anapata wakati mgumu. Mrajisi ana mwongozo wake, Bodi ina mwongozo wake, mwisho wa siku tunashindwa kuwaweka wananchi wetu katika mazingira yenye kuleta kipato kikubwa. Nchi hii tumekubaliana kwamba lazima tuwe na uzalishaji mkubwa ili tukidhi mahitaji ya wananchi wetu. Ukizalisha mbegu nyingi tena tutapata mafuta mengi, tuna alizeti, mawese na vitu vingine lakini wananchi watalima pale ambako hakuna usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba amesema amejipanga kuhakikisha kwamba vyama vya ushirika vinakusanya pamba halafu mnunuzi aende kununua. Ni mwananchi yupi atakayepeleka kwenye vyama vya ushirika ambavyo watu wamekosa imani, hiyo ni kazi ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali jambo hili iliangalie kwa mapana zaidi na tuliwekee utaratibu mzuri utakaokuwa na tija kwa wananchi wetu. Hili jambo wakilipokea itakuwa ni vizuri zaidi kuliko hivi sasa hata ile iliyowekwa kwa mwaka huu Sh.12 inaenda kuimarisha union, kwa hiyo, mwananchi huyu ataendelea kupata shida tu. Pangekuwa na mifumo mizuri kule kijijini kama alivyoelekeza Waziri Mkuu katika kikao chake cha Wakuu wa Mikoa kwamba tunataka hizi AMCOS zimilikiwe na wenyewe lakini mliporudi ninyi kwenye sheria na utaratibu wenu mkasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)