Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii, kwa sababu ya muda nitaenda haraka haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya kilimo inaajiri asilimia 65 ya nguvu kazi ya Taifa; inachangia asilimia 9.9 ya pato la Taifa; inachangia asilimia 65 ya malighafi viwandani na inachangia asilimia 100 ya chakula kinachopatikana hapa nchini. Sekta hii ya kilimo kama ikiwekezwa vizuri itatoa ajira ya kutosha; itaondoa umaskini; tutafikia hicho mnachokitaka kinaitwa Serikali ya viwanda na tutaweza kufikia uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sekta hii imekuwa haipewi fedha kama inavyotakiwa. Fedha tunazozitenga hapa Bungeni hazifiki kwenye Wizara na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa miaka 10 fedha ambayo imepitishwa na Bunge lako ambayo imefika kwenye Wizara hiyo ni asilimia 2 tu. Mwaka huu fedha hizo za miradi ya maendeleo ambazo zinaombwa imekuwa ni pungufu ya asilimia 23 ya bajeti ambayo tulipitisha mwaka 2017/2018. Maana yake ni kwamba sekta hii ya kilimo imeendelea kupuuzwa, kuachwa nyuma na haipewi msisitizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa sekta ya kilimo kwa mujibu wa Ripoti ya Benki Kuu ni kama ifuatavyo: Mwaka 2011 ilikua kwa asilimia 1.9; 2012 ilikua kwa asilimia 3.2; 2013 ilikua kwa asilimia 4; 2014 ilikua kwa asilimia 3.4; 2015 ilikua kwa asilimia 3.2; 2016 ilikua kwa asilimia 1.9; 2017 ilikua kwa asilimia 1.3. Serikali ya Awamu ya Nne wakati inaondoka madarakani iliacha sekta ya kilimo ikikua kwa asilimia 3.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano mmejiita Serikali ya Hapa Kazi, Serikali ya Viwanda, mmeweka mikakati ya kufikia uchumi wa kati lakini sekta ya kilimo ambayo inategemewa na asilimia 65 ya Watanzania, ambayo inachangia pato la Taifa imeendelea kushuka na kufikia kiasi cha asilimia 1.3. Kwa wastani maana yake ni kwamba sekta ya kilimo imekua asilimia 1.9 tu. Kila siku mnatuambia uchumi unakua kwa asilimia 7, Watanzania asilimia 65 wanategemea kilimo, halafu uchumi huu wa sekta ya kilimo tu unakua kwa asilimia 1.9 halafu mnataka miujiza mfikie kitu kinachoitwa uchumi wa kati? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa nchi hii ni lazima wajue adui yao ni Serikali hii ambayo ina mipango mibovu ya kutoweza kuiwezesha sekta ya kilimo. Asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo lakini uwekezaji unaofanywa kwenye sekta hii ni kiasi cha asilimia 0.52 ya bajeti kuu ya Taifa lakini asilimia 5 ya Watanzania ambao wanategemea usafiri wa ndege inapewa kipaumbele ndege unawaacha asilimia 65 ya Watanzania ambao wanategemea kilimo. Huku ni kuwahadaa Watanzania, ni kuwahadaa wakulima, ni kuwadanganya wakulima wa Tanzania. Wakulima wa nchi hii adui yenu ni Serikali hii ya CCM iliyoko madarakani. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hapa michango ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakilalamikia suala la mahindi kutokuuzwa. Nimeona leo mzigo anashushiwa Mheshimiwa Tizeba pale, hivi tumesahau ni nani alikataza mahindi yasiuzwe. Kauli zikatolewa hapa kwamba mahindi yasiuzwe na Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama hapa akasema hakuna kuuza mazao nje ya nchi. Sasa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanasimama wanampongeza Waziri Mkuu, wanampongeza Rais, wanamshushia mzigo Mheshimiwa Tizeba pale na Mheshimiwa Tizeba ataubeba tu mzigo huu kwa sababu kama huwashauri tunafanyaje.