Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua za kwanza ndiyo za kupandia. Kwa masikitiko makubwa sana mvua za kwanza za kupandia mbolea na mbegu hazipatikani, hili limekuwa ni tatizo sugu sana katika Taifa letu. Tunaposema kilimo ni uti wa mgongo kwa Taifa letu la Tanzania ukizingatia asilimia 75 ni wakulima, kati yao asilimia 65 ni wanawake na wanawake ndiyo nguzo kuu katika familia zetu. Ni kwa nini basi Serikali kwa kutumia wataalam tulio nao wasiwe na mpango mkakati kuanzia sasa wajue ni wakati gani mbegu na mbolea zifike kwa wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tafiti imeonekana asilimia 25 ya wakulima hutumia mbegu bora. Katika kutumia mbegu bora asilimia 40 huchangia kupatikana kwa mavuno. Kwa maana hiyo, huyu mkulima atakavyokuwa amepewa mbegu bora mavuno yake yanapatikana kwa asilimia kubwa hivyo kipato chake kinamkwamua kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye kundi la kati. Kwa ujumla wake Watanzania tulio wengi watoto wetu tunawasomesha kwa njia ya kilimo, hii haipingiki. Naomba Waziri wa Kilimo anapokuja kuhitimisha hoja yake hii atuambie ni lini sasa Serikali imejipanga kuhakikisha mbegu na mbolea zinaenda kwa wakati muafaka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inasikitisha, wamekiri kuwa asilimia 36 ndiyo sasa mbegu bora zinapatikana, asilimia 64 tunaagiza. Hebu fikiria, tuna vyuo vyetu vya kilimo, ni tatizo lipi linalotukumba sisi Watanzania tusitumie hivi vyuo vyetu kuweza kuwa na wataalam wanaoweza kuzalisha hizi mbegu bora zikapatikana Tanzania tukaepusha gharama ya kutumia kuagiza mbegu katika Taifa lingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukulia mfano Mkoa wa Iringa kuna Kiwanda cha Dash ambacho ni cha kusakata nyanya, hadi navyozungumza kimeshindwa kufanya kazi hiyo kutokana na kwamba wakulima wanaolima zao la nyanya hawatumii mbegu bora hivyo wameshindwa kuzalisha nyanya ambazo zinaweza zikaenda kwenye kiwanda hicho hatimaye na kiwanda kuendelea kufanya kazi. Tuna Maafisa Ugani katika nchi yetu wamebaki maofisini na ndiyo maana wakulima wanalima kwa kubahatisha hatimaye mazao hayapatikani ya kutosha, kama hili zao la nyanya nililotolea mfano la Kiwanda cha Dash. Naomba Serikali basi ifikie wakati wa hawa maafisa wetu kwenda kule kwenye vijiji wakashirikiane na wakulima wetu ili waweze kuwapa elimu ya kutumia mbegu bora na mbolea ili waweze kupata mazao yanayoendana na hitaji ambalo tunataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge jioni ya leo katika Wizara hii wanachangia Wizara hii kwa machungu makubwa sana hasa watani wetu wa jadi. Nachosikitika tutakapokuja kushika shilingi hiyo ya Waziri yatatoka maelekezo, tutaachia shilingi Wizara hii itabaki kama ilivyo. Nawashauri Waheshimiwa Wabunge kwa vile imeonekena wote tunataka katika Taifa letu la Tanzania kilimo kipewe kipaumbele hii shilingi ya Waziri wa Kilimo ishikiliwe mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia mustakabali wa nchi ya viwanda, viwanda hivi vinategemea mazao na mazao haya ndiyo tunayosema mbegu bora. Ukitaka mahindi mbegu bora na mbolea, ukitaka pamba mbegu na mbolea na dawa. Kama Wizara hii inakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kuwa bajeti inayotengwa na kupitishwa kwenye Bunge hili Serikali haitaki kutoa basi na wenyewe watuonyeshe kutuunga mkono kwamba Serikali imekaa kimya kwa kutokutoa fedha kwa wakati ili kilimo hiki tunachosema tunataka nchi ya viwanda kiweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitarudi kwenye zao la mahindi kwenye Mkoa wangu wa Iringa. Tunapozungumzia zao la mahindi Mkoa wa Iringa ndilo zao la …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)