Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REHEMA J. MIGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni katika Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu katika uchumi na maendeleo ya wananchi wake. Tunajua kabisa asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania wamejikita katika kilimo. Hata hivyo, kilimo leo hakipewi kipaumbele hali inayopelekea wananchi waone kilimo si jambo lenye tija kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze zaidi katia zao la tumbaku. Zao la tumbaku ni muhimu sana kwa wakazi wa Tabora na Tanzania kwa ujumla kwani linapelekea nchi yetu na Serikali kwa ujumla lipate pato kubwa hasa katika fedha za kigeni. Hata hivyo, zao hili leo hii limekuwa halina tija kwa mkulima wa Tabora kutokana na changamoto mbalimbali mfano suala la masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi soko la tumbaku si la uhakika, wananchi wanalima mazao kwa shida sana, wanatumia muda mrefu na gharama kubwa lakini hawajui zao lao la tumbaku wataliuza wapi na hata wakija kuliuza bado wanapangiwa bei ndogo sana tofauti na gharama za uzalishaji. Hivyo, naiomba Serikali yetu basi iwahakikishie hawa wakulima wa Tabora soko la uhakika ili kilimo hiki kiwe chenye tija. Serikali ituambie, hivi zao hili ina mpango wa kulifuta kabisa au vipi? Kama ndivyo, kuna zao gani mbadala ambalo Serikali imewaandalia wakulima wa Tabora ili shughuli zao za kiuchumi ziendelee? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia napenda niongelee matumizi ya Tanzania shilling badala ya dola. Kulitolewa tamko la matumizi ya Tanzania shilling badala ya dola kwenye shughuli mbalimbali za ununuaji wa tumbaku na uagizaji wa pembejeo kutoa nje ya nchi. Naomba nijue, je, Serikali ilifanya utafiti kujua ni gharama kiasi gani ambayo inawa-face wakulima wanapotumia shilingi badala ya dola? Nasema hivi nikiwa na sababu kwamba, mkulima anapoingia mkataba na wanunuzi huwa anaingia kwa gharama ya dola lakini inapokuja kwenye suala la manunuzi anaambiwa auze kwa Tanzania shilling.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa kwamba shilingi yetu ya Tanzania inashuka thamani siku baada ya siku, lakini inapokuja kwenye suala la uuzaji anauza kwa dola ambayo kwa wakati huo inaweza kuwa imepanda. Tunaomba Serikali ituambie, je, walifanya tafiti za kutosha kubadilisha matumizi ya dola kwenda kwenye shilingi kwa sababu shilingi inamuumiza mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu pembejeo hususani mbolea. Mbolea imekuwa ni janga kubwa sana kwa wakulima wetu pamoja na kwamba Serikali imekuja na mfumo mzuri wa ununuzi wa pamoja lakini ununuzi huo au mfumo huu kwa sasa inaonekana kama vile umefeli kutokana na ukweli kwamba mbolea haiji kwa wakati. Wakati mkulima anahitaji kupanda mbolea haipo akishapanda ndiyo mbolea inakuja, wakati anapotaka kukuza mazao yake mbolea haipo, anapotaka kuvuna ndiyo mbolea inakuja, sasa tunamsaidia huyu mkulima au tunamchezea makidamakida? Naomba Serikali ije na majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imewekwa bei elekezi lakini haifuatwi. Kwa hiyo, tunataka tujue kwa nini Serikali inatoa maagizo ambayo hayatekelezeki? Kama hayatekelezeki ni hatua gani mnachukua kwa watu hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni utitiri wa kodi. Kumekuwa na tatizo la kodi na tozo nyingi sana kwenye suala la tumbaku na anatozwa mununuzi. Kutokana na kwamba mnunuzi huyu anatozwa kodi na tozo nyingi na yeye sasa anaamua kwenda kumbana huyu mkulima wa chini hali ambayo inamuathiri katika bei ya tumbaku. Tunaomba hizi tozo zipunguzwe au zifutwe kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hivi vyama vya msingi (AMCOS) vimekuwa ni shida. Kwanza, havipewi bajeti ya kutosha kwa ajili ya kujiendeleza lakini pia vimekuwa vinawadhulumu sana hawa wakulima wetu. Tunaomba hili suala liangaliwe hawa wakulima wasiteseke sana, wanalima kwa kuteseka bado waje kudhulumiwa, hapana hili jambo haliwezekani na halikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watendaji wa hivi vyama vya ushirika na hata Bodi za Tumbaku wanateuliwa tofauti na watu wanaojua tumbaku. Mtu hana taaluma ya tumbaku lakini anakwenda kuchaguliwa kufanya kazi kwenye AMCOS na kwenye Bodi la Tumbaku. Kama mtu hana utaalam wa tumbaku unafikiria ataifanya kazi hii effectively? Tunaomba kabisa Serikali iwaaangalie hawa watendaji wa kwenye hivi vyama vya ushirika pia hawa watu wanaoteuliwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)