Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, niipongeze Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kazi nzuri iliyofanyika leo ambayo Mheshimiwa Rais ameitolea maamuzi pale bandarini. Nawaomba na Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuweze kupongeza hatua hiyo ambayo Mheshimiwa Rais ameionesha pale bandarini leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati Mheshimiwa Rais anafanya kazi leo bandarini ilikuwa live amesema iletwe amendments tuweze kuweka sheria ya kuwabana watu wasilete raw material ya vyakula kutoka nje ili kuwasaidia wakulima wetu wa ndani. Kwa slogan hii, ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, jirani yangu, umesikiliza michango ya Wabunge na mimi tangu nimekuwa Mbunge, lazima niseme wazi kwa kweli leo kimenuka, si cha kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kuhusiana na ununuzi wa pamba, mimi natoka maeneo ya pamba na bahati nzuri Mheshimiwa Tizeba tuko jirani. Ukienda Jimbo la Geita hakuna go-down hata moja la chama cha ushirika, jimbo zima na sisi tumewahamasisha wananchi walime na pamba iko nyingi. Hebu nikuulize Waziri mnapoweka haya masharti ya vyama vya ushirika wanunue wanaiweka wapi hii pamba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati zao hili limeachwa kulimwa tumefanya kazi kubwa sana ya kuwahamasisha wananchi. Naamini hata Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu pengine labda hawakupata taarifa sahihi. Hakuna mtu kwa sasa aliyeupokea huu ushirika, hayupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika ni mzuri tunautaka lakini haujaboreshwa kutoka kule tulikoharibikiwa mpaka tulipo sasa. Ukimwambia leo mwananchi apeleke pamba kwenye ushirika yaani ushirika uwe broker wa wenye pesa? Maana yake mkulima ataenda kuuza siku ya kwanza na kwa hesabu nyepesi tu ni kwamba labda kijiji kimoja kinaweza kuwa na vituo nane mpaka kumi; sasa kituo kimoja kinaweza kununua kilo 200, 500 kwa siku, pamba hiyo haiwezi kuchukuliwa na gari gharama ni kubwa, ili ipatikane tani 10 pengine itachukua siku saba, aliyeuza siku ya kwanza atakuwa na siku saba anasubiri pesa, ni kitu ambacho hakiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wewe mwenyewe ni shahidi, unazunguka kule unaona hali halisi. Ushirika uliopo sasa hivi ni uleule umejibadilisha kwa maneno, kwamba walewale waliotuibia ikafa Nyanza na SHIRECU mmewarudisha tena, yaani mtu akasimamie ushirika amejaa viraka matakoni halafu tukampe kazi ya kusimamia hela za wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unisamehe, lugha yetu Wasukuma Kiswahili kidogo kilitupiga chenga, nafuta maneno hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali na michango ya Waheshimiwa Wabunge mmeiona mliangalie suala hili. Mheshimiwa Waziri kabla hujafika mwisho wa kuhitimisha hoja yako naomba kesho asubuhi uje na kauli ya kuondoa ushirika kwa sasa ili tufanye maandalizi ya kuweka ushirika mwaka ujao. Naamini kila mtu analalamika kwa upande wake, kuna watu wanalalamikia mahindi, mahindi tulishakosea tusiende kukosea na kwenye pamba ambayo sasa iko sokoni. Tusilimbikize tena matatizo ya mahindi tukaweka na pamba tutaua soko hili la wakulima na wakulima hawatakuwa na moyo tena wa kulima kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la bei, tulikubaliana kabisa kwenye kikao kwamba tupunguze hizi kodi na bahati nzuri kwenye ukurasa wa 46, umesema umefuta mfuko wa CDTF, kwa nini tena unaweka Sh.100? Maana yake unatugeuza huku tukiangalia huku unasema tena tulipe Sh.100 ni kwa sababu wakulima wengi hawajui kusoma au hii ni design gani? Kwa hiyo, tunakuomba usimamie suala la bei mkulima afaidike ili mwakani tuwe na pamba nyingi hamtakuwa na shida ya kuagiza mafuta machafu kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine, Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe ni shahidi sisi tunatoka maeneo ya wananchi waliotuleta hapa, kuna tatizo gani la kuwalipa mawakala? Tatizo ni nini? Uhakiki gani usioisha? Kila mtu analalamikia mawakala na kila mwaka tunazungumza tunaambiwa mnafanya uhakiki. Mheshimiwa Waziri kwenye kuhitimisha tueleze kwamba pesa haipo ili kama Bunge linaweza kuamua kukuombea pesa likuombee pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamekufa. Usione watu wamefanya biashara ya kuwakopesha wananchi siyo pesa zao wamekopa kwenye taasisi za benki. Watu wameuziwa nyumba, watu wana matatizo huko, vitu vyao vinapigwa minada Serikali ipo tu inaangalia. Mheshimiwa Waziri, bahati nzuri wewe unatoka sehemu ya wakulima wa pamba, rudisha moyo, kama hii kazi ni ngumu, pia kazi ya kukaa huku kuwasaidia Mawaziri kujibu ni nzuri tu unakuja tunakukaribisha huku nyuma. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekti, suala lingine, nawashangaa sana Waheshimiwa Wabunge, yaani mtu anasimama anasema tumekosea sana kununua ndege. Mimi nikiwaangalia ninyi wote si wa kupanda basi, mbona mnazipanda? Kwa hesabu nyepesi tu ya kibiashara lazima uwe na vitu vya kuingiza. Sasa kuhusu suala la ndege, ndege inasaidia kuleta pesa kwenye utalii. Hii kauli kila siku ya kuponda kununua ndege tunataka tuwaone msiwe mnapanda Bombardier muendeshe magari yenu kwenda Dar es Salaam. Haiwezekani mnaponda humu halafu jioni tunadandia wote Bombardier kwenda Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo teknolojia na nchi inayoendelea lazima iwe na vitu vya kuwawahisha watu wafanye kazi Dar es Salaam, asubuhi tuwe Dodoma kwenye Bunge. Kwa hiyo, mimi nawashangaa sana wote mnaobwabwaja kuzungumzia suala la ndege. Pengine ni suala la wivu ambalo kimsingi Watanzania tunahitaji kulipuuza na tusilisikilize kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuomba Mheshimiwa Waziri, Maafsisa Ugani wawe wanaleta mrejesho kama tulivyomuona Rais anawataka Mabalozi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaunga mkono hoja mpaka atoe majibu ya kueleweka.