Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu hatimaye nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu sana ya kilimo. Tukiamini kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifikapo mwaka 2025 tunategemea kwamba nchi yetu ya Tanzania itakuwa ni nchi ya kipato cha kati ikiongozwa na kaulimbiu yetu ya Tanzania ya viwanda. Hili ni jambo jema sana kwa ustawi wa Taifa letu la Tanzania. Pamoja na hayo ili tuweze kufikia azma yetu ya 2025 kuwa Tanzania ya viwanda ni lazima kama nchi tuwekeze sana kwenye kilimo na hasa kilimo cha umwagiliaji ambacho kinatupa uhakika wa kile ambacho tunatarajia kukifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi duniani zilianzia kwenye kilimo hatimaye kukaja na mapinduzi ya viwanda, kwa mantiki hiyo tukiwekeza kwenye kilimo tutakuwa na uhakika wa kupata malighafi zitakazotusaidia kwenye viwanda vyetu hatimaye tutaweza kukua kwa kadri tulivyokuwa tunatarajia. Ushauri wangu kwenye jambo hili ni lazima tupange mikakati yetu vizuri ili azma yetu hii tunayoitarajia iweze kutekelezeka kama tulivyojipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia kwenye eneo la ufuta. Ufuta ni zao kubwa na ni zao muhimu. Sisi kama Tanzania tunalima ufuta lakini kama Afrika vilevile nchi yetu ni nchi ya pili ikiongozwa na Ethiopia, pia hatuko nyuma kwenye dunia. Katika nafasi ya dunia sisi Tanzania tuko kwenye kumi bora. Kwa mantiki hiyo ina maana kwamba tukiwekeza vizuri kwenye ufuta, nini kitakachoweza kujitokeza, tunaweza kuzalisha wenyewe mafuta ambayo sasa hivi ni changamoto kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia ufuta wakulima wetu tuliwahamasisha sana juu ya kilimo cha ufuta na mazao mengine mbalimbali. Tatizo linakuja baada ya wakulima kuweza kulima vizuri lakini hata hiyo pesa yenyewe waliyotumia kulima wamekopa kwenye mabenki, inafikia hatua uuzaji inakuwa ni changamoto kubwa kwao. Kwenye eneo hili vilevile ninafarijika. Nimesikia kwenye taarifa hapa
kwamba, kuanzia sasa kuelekea siku zijazo ufuta nao utakuwa ni kati ya mazao ambayo yatauzwa kwa stakabidhi ghalani, ninaipongeza sana Serikali kwa kuweka ufuta kwenye stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu korosho. Korosho tunaamini na zao kubwa na ni zao ambalo linachangia uchumi wa Taifa letu la Tanzania. Lakini sasa korosho hii imeingiliwa na mdudu na mdudu huyu ni unyaufu wa korosho. Katika taarifa sikusikia eneo lolote, ni mkakati gani wameupanga juu ya kuondoa tatizo hili la unyaufu wa korosho. Korosho hizi zinalimwa Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani na Mikoa mingi ambayo iko kwenye Ukanda wa Pwani na sasa hivi korosho litakuwa ni zao la Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi hakuna kiwanda hata kimoja, ina maana kwamba suala la korosho lisipowekewe mkakati wa kudumu wananchi wa Lindi watazidi kuwa maskini kwa sababu hawatakuwa na kipato chochote kile, kwa kuwa hakuna kiwanda hata kimoja.

Mheshimimwa Mwenyekiti, naomba nielekee kwenye zao la mbaazi. Mbaazi tuliwahamisha wakulima walime, wengi sana walilima kweli kweli. Lakini ikafikia wakati mbaazi zikakosa soko, Mkoa wa Lindi ni asilimia 20 tu kati ya mbaazi zote ambazo zimeweza kuuzwa nyingi zimeharibika na wananchi hawa ni maskini. Serikali tunaomba iwasaidie chochote ili waweze kuendelea na kilimo waweze kujipatia maslahi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nakushukuru sana kwa kunipa fursa, lakini jambo lolote ni mchakato, naamini matatizo haya tukijipanga yataisha. Ahsante sana.