Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi angalau dakika tano hizi niweze kuchangia kwa haraka haraka tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeamka tofauti kabisa, mara nyingi sana nilikuwa nafikiri Mheshimiwa Tizeba ni tatizo. Naomba nikiri leo ndani ya Bunge kwamba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo hana tatizo lolote. Tatizo ninaloliona hapa ni Waziri wetu wa Fedha ndiyo kikwazo kwa kila jambo tunaloliongelea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukilalamika sana kuhusiana na Wizara ya Kilimo, lakini leo naomba niseme kwamba kwa 18% iliyotengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwenye kilimo tumefanya makosa makubwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri na Bunge lituunge mkono kwamba bajeti hii ikapitiwe upya ili tuje tuijadili kwa sababu muda bado tunao, lakini kwa asilimia 18 kwenye suala la maendeleo naomba niseme kimsingi tumeshindwa kutekeleza yale ambayo tulikuwa tumekubaliana toka mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa harakaharaka tu, nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutoa kikwazo cha vibali kusafirisha mahindi yetu kwenda nje. Nikuombe tusifanye tena makosa haya. Kosa hili limetugharimu sana hasa sisi wakulima wa mahindi na mpunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivyo kwa sababu, maeneo tunayotoka sisi ndiyo zao letu kubwa kama zao la chakula lakini ndiyo zao la biashara. Mnapofunga mipaka hii matokeo yake mnatufanya sisi tunaathirika zaidi. Sisi Wabunge wa maeneo hayo tuna kila sababu ya kuwatetea wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Sumbawanga gunia moja la mahindi ni shilingi 15,000 mpaka shilingi 20,000. Hebu niambie huyu mkulima leo hii unamwambia akalime tena mahindi ataweza kweli kulima? Kwa bahati mbaya mnambana kila kona na mkulima huyu hatumsaidii chochote. Narudia, hatumsaidii chochote. Nikuombe, kosa tumeshalifanya tusirudie tena kufanya kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi vibali unavyovisema Mheshimiwa Waziri vitatoka mikoani unaenda kukaribisha rushwa kule, kwa nini msifute moja kwa moja? Uwezo wa kununua hatuna, uwezo wa kuwasaidia wakulima hatuna, waachieni wafanye wanavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la kusema mkulima ndiyo wajibu wake kuhakikisha mwananchi hafi na njaa, tunakosea. Kama hoja ni hiyo, basi hata sisi watumishi na Wabunge, ikitokea kuna suala la njaa tuwe tunakatwa na sisi mishahara yetu ili tukafidie kule ambako kuna tatizo la njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wakulima wetu hawa wanaonewa sana, ifike wakati sasa tuagalie jinsi gani ya kuwasaidia tuwaache wawe huru, walime wenyewe, wavune wenyewe na vilevile wakatafute masoko wakauze kokote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda haraka haraka, leo tuna mawakala wamekuja kututembelea hapa, mawakala hawa huu mwaka wa nne hawajawahi kulipwa hata senti moja. Tunaamini mmefanya uhakiki, mnaangalia madeni, mmechunguza, lakini Waziri wa Fedha aje atujibu hapa nini dhamira ya dhati ya hawa ambao walitusaidia wakati wa dhiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano, juzi kule kwetu kuna mfanyabiashara mmoja ambaye ni wakala alikuwa anaitwa Mohamed, kwa jina maarufu alikuwa anaitwa Mohamed Msomali, kauziwa nyumba yake kapata pressure amefariki. Basi kama mmehakiki madeni yale ambayo ni halali walipeni kwanza wapunguze machungu wakati mengine mnayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, najua tatizo haliko kwako, Waziri wa Fedha akija hapa aje atujibu, lile ambalo mmeona ninyi ndiyo halali yao wapeni mengine wataendelea kudai baadaye ili wakapunguze machungu waliyokuwanayo. Leo hii hapo walipo wana wiki moja wako hapa Bungeni, kulala kwa shida, kula kwa shida, matokeo yake wamekuwa ombaomba hapa ndani ya Bunge, nafikiri na leo wapo hapa. Hebu angalieni jinsi gani ya kuwasaidia, kuweni binadamu, Waziri wa Fedha liangalieni hili, walipeni hawa watu kwa sababu walitusaidia wakati wa shida, tena wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015. Kama hawadai, semeni hawadai ili wakaanzishe kazi nyingine waridhike kwamba sasa hivi hatudai, wasamehe hayo madeni. Mheshimiwa Waziri, hili sio la kwako, naomba Waziri wa Fedha aje atujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea kuhusu mbolea. Kila Mbunge ana haki ya kuchangia lolote lile ndani ya Bunge hili. Kila Mbunge ana wajibu wa kuchangia na wengine wachangie, siyo tusipingane, tupingane kwa hoja, sisi siyo wataalam lakini wataalam wanatuambia mbolea ya Minjingu inafaa. Mimi naona kuna shida hapa, shida ni jina, brand ile, wangeongeza neno moja ‘s’ pale Minjingus ikawa la kizungu hapa tusingepiga kelele. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninavyojua kwa sababu kuna DAP, wameshazoea DAP kwa sababu ni la kiingereza. Leo hii hata shati…

T A A R I F A . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongelea kuhusu wataalam, sijui dada yangu kama ni mtaalam. Sasa hapa ndiyo kuna shida hapa, Mheshimiwa Waziri mje mtujibu wataalam wanasema nini, research yao inasema nini na kama inafaa watuambie inafaa na kama haifai tuambiwe haifai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka niseme ndani ya Bunge hili, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa mzalendo kwa kutaka kufufua viwanda vya nchi yetu lakini kuongeza viwanda...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)