Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu ahsante sana kwa kunipa hii nafasi adimu ili na mimi nichangie kwa dakika tano katika Wizara hii ya Kilimo ukizingatia mimi ni mtoto wa mkulima na hapa nilipo nimekulia kwenye kilimo na maisha yangu yote yapo kwenye kilimo. Uzuri zaidi katika Wilaya yangu ya Kilombero, Jimbo ambalo naliongoza mimi la Mlimba karibu asilimia 99 sisi ni wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kuna haja ya kusema kwamba kilimo hiki ambacho sisi tunahangaika kwa majembe ya mkono, wengine power tiller, kwenye matope, barabara hamna, mbegu, panya tunapambana nao viwavijeshi na Maafisa wa Ugani hakuna yaani tunahangaika tu kama kuku wa kienyeji. Serikali imeshindwa kabisa angalau kuonyesha kumkomboa huyu mkulima siyo kwa maneno tu kwa vitendo kwa kutoa ajira nyingi kwa Maafisa Ugani hasa kwenye maeneo ambayo tunalima. Unaposema tu kilimo ndiyo uti wa mgongo karibu asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima lakini asilimia 100 ya Watanzania tunatumia mazao ya kilimo halafu kilimo chenyewe kinakuwa alfu lela ulela kwa kweli inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema inasikitisha? Pamoja na kilimo hiki kuachwa kinahangaika chenyewe lakini katika pato la Taifa kinachangia asilimia 31 lakini leo katika bajeti ya kilimo haki ya Mungu inatia huruma, hivi kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika kipindi hiki cha kupanda nilihangaika sana kwenye Wizara ya Kilimo, kwa Waziri kwa Naibu Waziri, panya walivyovamia kwenye mazao, watu wamepanda mara ya kwanza panya wamekula, mara ya pili wamekula, mbegu wanahangaika lakini kwenda Wizarani hawana bajeti. Nilitegemea kwenye bajeti hii kuwepo na bajeti kabisa ya dharura kwa sababu wadudu wengine waharibifu wanatokea bila taarifa. (Makofi)

Kwa hiyo, tunaomba bajeti ya dharura au maalum kwa ajili ya majanga kama haya katika suala la kilimo, hapo ndio mtakuwa mmeenzi kilimo kuliko kuacha watu wanahangaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi sisi kule tunalima mpunga, kokoa, ufuta, mbaazi kule kila kitu kinakubali hata binadamu ukimpanda kule anaota Mlimba, Wilaya ya Kilombero. Cha kushangaza pamoja na mambo yote haya kwamba tunalima wenyewe mpunga mwaka jana soko likawa kubwa kweli kweli, Tanzania nzima wakaja Ifakara. Bei ya mchele na mpunga ikapanda kwa sababu pumba ni mali chakula cha mifugo, pumba tunachomea matofali yaani hakuna kitu kinachotupwa katika mpunga, lakini ikafikia mahali bei ilivyopanda tukaambiwa soko limefungwa hakuna tena kupeleka mazao nje, ninyi vipi kwani mlitugea ninyi mitaji? Kwa nini mnatuonea wenzenu? Barabara mbovu, tunahangaika tunalima wenyewe halafu mnafunga masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba mipango hii ya Serikali ya kufunga masoko ya nje au kufunga mipaka naomba msitufanyie tu sisi wakulima. Mtuone kwamba na sisi tunastahili kuuza mazao yetu nje, siyo lazima tuuze hapa hapa Tanzania. Kwa sababu sisi Wilaya ya Kilombero hitaji letu sisi ni tani 130, tunazalisha tani 530 ziada ni tani 400 sasa mnataka tuzipeleke wapi? Kwa hiyo, ni vema sasa mkatuona kwamba na sisi tunastahili kupata maisha, kusomesha watoto, kujenga nyumba bora, kuchangia shule, elimu, hospitali tunajenga wenyewe majengo. Kwa hiyo, tunategemea tukilima, tukipata pesa ndiyo tunaenda kuchangia hizo huduma za jamii. Sasa mnavyotuacha hivi tunahangaika wenyewe huduma za jamii tutachangiaje na Serikali imesema wazi wananchi watajenga maboma Serikali ndiyo itakuja kumalizia. Sasa tunajengaje maboma kama hatuna kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushirika, hili nalo ni janga la Taifa kwa sababu hawa viongozi waliopo katika ushirika ndiyo walioua ushirika, leo zinaundwa timu kwenda kuhangaika na madeni halafu wanashirikisha viongozi hao hao. Mimi nataka nijue Serikali imechukua hatua gani kabla hatujaenda kwenye ushirika kwa wale viongozi walioua ushirika ambao wapo. Siyo mnakimbilia tu kuunda ushirika wakati wale walioharibu ushirika hamuwachukulii hatua.

Hiyo itakuwa ngumu sana mtu kujiunga katika ushirika na mtagombana na mtawafunga wengi kama mnapitisha maagizo ya namna hiyo huko chini, hayatatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiomba bajeti ya kilimo iongezeke na ishuke chini watu waajiriwe, tupate wataalam watusaidie katika masuala ya kilimo na masoko yawe wazi mkulima awe na uwezo wa kuuza mahali popote. Kama mnataka kudhibiti masoko basi muwe na kilimo maalum, Serikali itoe hela kwa wakulima mseme mazao haya tumetoa pesa na mbolea bure kwa wakulima kwa hiyo hayo lazima tuyauze ndani lakini aliyehangaika mwenyewe, muacheni akauze mahali popote, tutakuwa tumemstawisha huyo mkulima.