Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote kwa kuandaa hotuba na kuleta hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni ya tumbaku Mkoa wa Tabora yanaendelea kupunguza makadirio/makisio ya tumbaku kila mwaka. Msimu wa mwaka 2017/2018 makisio yalishuka kutoka tani 13 hadi tani 10, na msimu huu wa mwaka 2018/2019 zipo dalili za makisio kushuka zaidi wakati wakulima wameshakopa benki, wakapata pembejeo na sasa wanakosa soko kwa kukosa makisio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali/Waziri inasaidiaje wakulima wa tumbaku inayoendelea kuvunwa wakati hawana uhakika wa soko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeelezea juu ya kununua mbolea kwa pamoja na kusambaza kwa bei ya ruzuku. Pamoja na kuja na mfumo huu, bado tatizo la upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei elekezi na ya kutosha ni tatizo kubwa sana. Serikali itueleze ni mfumo gani umewekwa kwenye Wilaya zetu wa kuhakikisha mbolea hii ya ruzuku inawafikia wakulima na kwa wakati kwa bei elekezi na ya kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018, tumbaku ya Kaliua zaidi ya tani milioni tano zimeuzwa kwa bei ya makinikia, USD 0.073 hadi 0.070 baada ya bei elekezi ya USD 2 hadi 2.5. Wakulima wengi wamebakiwa na madeni makubwa ya benki na taasisi za fedha. Wengi wao wameshindwa kuingia kwenye kilimo cha tumbaku na wana hali mbaya. Tunaiomba Serikali iwasaidie wakulima hawa ili waweze kunyanyuka tena na kuingia kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mwaka jana iliruhusu chini ya tani wanunuzi wa mazao chini ya tani moja wasilipe kodi, hili limekuwa ni tatizo na pia kunyima mapato Halmashauri za Wilaya zinazotegemea kilimo na mazao kama chanzo cha mapato. Wanunuzi wanasafirisha gunia 10 mpaka 15 bila kulipa ushuru hivyo wanabeba kidogo kidogo ili wasilipe ushuru. Serikali mnasaidiaje Halmashauri za Wilaya kupata mapato kupitia ushuru wa mazao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kila Mkoa kuna mazao ya kimkakati ya biashara ambayo ndiyo yaliyosaidia kuinua uchumi wa mikoa hiyo. Mazao mengi yaliyotegemewa yamedorora na mengine hayalimwi kabisa kwa kukosa msukumo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa-Kilimanjaro, kokoa- Mbeya, minazi-Pwani, korosho-Kusini, ndizi-Bukoba, zabibu- Dodoma, tumbaku-Tabora, mawese-Kigoma na kadhalika. Serikali itupe maelezo ni mikakati gani ya uhakika kuhakikisha maeneo haya yanayotegemewa kuinua uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo kandarasi waliongia mkataba na Serikali kwa ajili ya kujenga ma-godown kwa ajili ya mazao, wengine hawajalipwa tangu mwaka 2016. Wapo waliojenga ma-godown saba tangu mwaka 2016 mpaka leo hawajalipwa na wanadai kwa miaka yote bila kulipwa. Pia mawakala wa kusambaza pembejeo za kilimo hawalipwi kwa wakati. Serikali ilieleze Bunge mpango wa kulipa madeni yote ya kandarasi waliokopwa miaka mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kilimo cha uhakika bila ushirika wenye nguvu. Serikali iweke utaratibu endelevu wa kukagua Vyama vya Ushirika (AMCOS) mara kwa mara ikiwezekana kila robo ya mwaka. Waziri apewe taarifa za ukaguzi wa ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mafunzo yatolewe kwa uongozi wa ushirika ili waongoze AMCOS/ushirika kwa ufanisi na uaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipangaje kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuhakikisha tunaongeza hekta za umwagiliaji kufikia hata hekta milioni moja kwa mwaka 2020? Tangu mwaka 2013 mpaka leo hata nusu hatujafika. Kilimo chetu kwa asilimia zaidi ya 80 tunategemea mvua. Kuna mabadiliko ya tabianchi, mvua hazieleweki. Serikali itueleze inajipangaje kwenye sekta ya umwagiliaji na kuwasaidia wakulima kuelekea uchumi wa viwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko, Serikali inahamasisha wananchi walime, wanaingia benki wanachukua mikopo, wanaweka nyumba zao bond, wakizalisha hakuna masoko. Ili kupata masoko ya uhakika, tunahitaji wataalam ambao watatembea duniani kuangalia fursa za masoko kwa mazao ya aina mbalimbali. Kuna mpango gani wa haraka kuhakikisha mazao ya mahindi, karanga pamoja na mbaazi ambayo yamekosa soko yanapata masoko.