Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ambayo nitapata taabu kidogo kulingana na mazingira yenyewe ya sekta kwa sababu nina maslahi nayo mapana kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitapata taabu kwa sababu Mawaziri wlaiopo katika Wizara hii wote ni vijana na ni marafiki zangu ambao tunafahamiana kwa muda mrefu lakini ambao kwa kweli katika Wizara hii wameshindwa kabisa kabisa kuonesha ujana wao katika Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu kuna makundi makubwa manne; kuna kundi la wafanyakazi, wakulima, wafugaji na kuna wavuvi. Kama Serikali inatafuta ugomvi kwa makundi haya yote manne hii Serikali inategemea ku-survive kwa mazingira gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka mitatu mfululizo hawajapandisha mishahara ya watumishi, miaka mitatu mfululizo wameshindwa kupeleka mbolea kwa wakulima, miaka mitatu mfululizo wameshindwa kutuletea hata shilingi ya wafugaji. Mheshimiwa Waziri, wanategemea nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Serikali ni kwenda kuomba ridhaa kwa wananchi wakipewa wanakusanya kodi kwa niaba ya wananchi, wanapeleka huduma. Wao wanakusanya, hawatuletei huduma. Mkataba wetu kwa maana ya wananchi na Serikali tunakutana wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana wakaona ng’ombe kama chakula, wakaona kama kitoweo wanavyoenda kunywa maziwa pale, wakala nyama, wakala samaki, wakala kuku, wakala mayai, wakashiba mkaja hapa wakaendelea. Sisi ni uchumi! Sisi ni maisha yetu! Mheshimiwa Waziri anakubalije kumeza dhambi hii? Anakusanya bilioni ishirini na sita kutoka kwetu halafu anaandika kwenye bajeti yake hajapeleka hata shilingi. Kama binadamu, yeye anajisikiaje? Huu ni unyang’anyi uliohalalishwa na sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Mheshimiwa Waziri, anatuletea bajeti, ndugu yangu, rafiki yangu kweli? Halafu amekusanya bilioni ishirini na sita, wameshindwa hata kutupa shilingi 100, kweli Mheshimiwa Waziri? Wafugaji wa nchi hii tumewakosea nini Serikali? Wizara zote wamepelekewa kidogo, sisi hata shilingi hawajatuletea, fadhila wanazotupa ni kutunyang’anya ng’ombe, fadhila wanazotupa ni kutunyang’anya samaki, nyavu, kutufilisi halafu kweli? Hata basi wangekuwa wanatunyang’anya, lakini wangeturudishia hata sehemu basi, kwa nini Wizara hii inyimwe fedha kuliko Wizara zote katika nchi yetu? Tumewakosea nini tuwaombe radhi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka yote ya nchi hii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Serikali haijawahi kupeleka ruzuku; kilimo ina ruzuku, sisi hatuna! Sisi tunataka watutengenezee mazingira tufuge, lakini kweli wanakusanya hela, wanatunyang’anya hela kwa nguvu halafu hawaturudishii hata kidogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Mifugo ya Mwaka 2006 na Mheshimiwa Waziri anajua ambayo imefanyiwa marekebisho ya tatu mwaka 1983 na 1997, imeeleza changamoto nne za wafugaji. Moja, ilizungumza habari ya ukosefu wa mikopo na mitaji ikazungumza habari ya magonjwa, ikazungumza habari ya ardhi, malisho ya maji na maeneo mengine ya wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 13 baadaye serikali hii imeshindwa kutatua hata tatizo moja ambalo sera hii imeainisha kwenye kitabu cha Serikali. Wanahitaji miaka mingapi kutusaidia malisho na wanahitaji miaka mingapi kutusaidia majosho? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri anasema amepeleka zero, kwetu sisi, tunataka watuwezeshe tu. Hii sera wametunga wenyewe, maeneo mengine inasema kabisa kwamba, matatizo haya yametokea kwa sabahu maeneo ya wafugaji yamevamiwa na wakulima na maeneo mengine yamevamiwa na uwekezaji wa National Parks, lakini ranch za Taifa wamewapa watu hawataki kuwarejesha wala hawataki kuendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana katika nchi yetu kwa mujibu wa takwimu 60 hectors million ni kwa sababu maeneo yanafaa kwa ajili ya nyanda za malisho ya mifugo. Mpaka leo kwenye ramani ya nchi hii miaka 50 ya uhuru hakuna mahali hata pamoja kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2010 iliyotangaza rasmi maeneo ya nyanda za malisho ya wafugaji, lakini wanayo sheria, hawatekelezi sheria wanatunyanyasa, hawatutengei maeneo ya malisho ya mifugo, tukiingia kwenye hifadhi wanatuuwa, tukiingia kwenye parks wanatuuwa, tukiingia kwenye maeneo ya mapori wanatuuwa, wanatunyang’anya ng’ombe wetu wanauza, sisi twende wapi? Watueleze leo? Tumepata soko Kenya, juzi wameenda wamezuia tusiuze, hawana masoko tupeleke wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mahali pa kulisha, hakuna maji, hakuna dawa, hakuna ruzuku wanayotuletea. Tunataka kuuza, tumekosa masoko ndani tumepata masoko nje wanataka kutu-charge kodi kwa lipi walilowekeza? Kwa nini wanataka kuvuna pasipo kupanda? Kwa nini wao wanataka kuvuna pasipo kupanda? Wamewekeza nini kwenye mifugo wanatukamata kila siku? Wametuletea nini? Wanasema wasipeleke nje, tupe masoko basi; hakuna haki pasipo wajibu. Wizara wajibu wao ni nini katika hili wanalotu- charge kila siku? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upelekaji wa fedha. Mwaka 2015/2016, walitenga shilingi bilioni nne hawakupeleka hata shilingi moja. Mwaka 2016/2017 walitenga bilioni nne hawakupeleka hata shilingi, mwaka jana bilioni nne hawakupeleka hata shilingi, miaka mitatu mfululizo, hivi wanafikiri sisi tunaishije? Wanatutaka nini wafugaji wa nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wao wamebaki kukusanya kodi na kutupiga na kutunyang’anya ng’ombe, lakini wao hawatuchangii chochote. Natamani wafugaji wa nchi hii siku moja, wiki moja tu wawanyime maziwa, wawanyime nyama, mayai, samaki, kama hawajafa humu ndani, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utitiri wa kodi katika sekta ya mifugo. Hii Mheshimiwa Waziri naomba atuambie leo, mtu akitaka kuwa na Export License ya Mifugo anatakiwa kulipa Sh.2,500,000/=, lakini wakati huo huo anatakiwa kujisajili kwenye Bodi ya Nyama Sh.100,000/=,
lakini wakati huo huo anatakiwa alipe Movement Permit Sh.2,500/= kwa kila ng’ombe. Akipeleka pale Namanga anatakiwa kulipa Sh.20,000/= kwa kila ng’ombe, anatakiwa kulipa Market Fee Sh.5,000/= kwa kila ng’ombe, anatakiwa kulipa Sh.2,000/= mpaka Sh.3,000/= ya hela za Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ng’ombe mmoja tu akisimama wao wanachukua Sh.50,000/= hawajachangia chochote, hawajafanya chochote, wanadai hizo fedha. Kama mtu ana Transport License ya Mifugo anapeleka Kenya kwa nini wana-charge ng’ombe mmoja mmoja tena fedha? Kama sio wizi ni nini huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtu ana Permit ya kusafirisha mifugo kwa nini wanatu-charge Sh.20,000/= kule Namanga? Tumewakosea nini sisi wafugaji wa nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunafuga kwa tabu, sisi tunachunga, sisi tunaondoka asubuhi umekunywa uji unarudi saa 12.00 jioni. Tunateseka sisi kutafuta malisho, tunateseka kutafuta maji, badala ya kutuonea huruma wanatu-charge hata kile kidogo tunachotafuta. Hii sio fair, linaniumiza kwa sababu linanigusa. Kwa nini wanatuwekea tozo hizi? Kwa nini wameondoa tozo nyingine kwenye mazao mengine yote mifugo wameacha? Kwa nini watu-charge mara kumi kumi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina leseni ya kupeleka ng’ombe Nairobi nimepata soko, unaenda kunizuia tena pale unani-charge Sh.20,000/= kila ng’ombe, nimekukosea nini? Kwa nini unatu-charge hiyo 20,000/=? Atuambie Waziri hizi tozo atapunguza lini, mbona kwingine wanapunguza? Au wana lengo la kuua mifugo? Waue basi tubaki hatuna, kwa sababu, huu ni unyang’anyi wa makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapata hasara katika sekta ya mifugo; nchi yetu ni nchi ya tatu Afrika kwa upatikanaji wa ng’ombe, lakini Mheshimiwa Waziri anajua tunapoteza zaidi ya bilioni mia moja ishirini kwa sababu ya uingizaji wa maziwa nchini, tunapoteza zaidi ya shilingi bilioni saba kwa sababu ya uingizaji wa nyama nchini. Tunapoteza zaidi ya bilioni hamsini na saba kwa sababu ya upelekaji wa ngozi nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni aibu gani Taifa linaloongoza kwa mifugo tunaongoza kuingiza nyama na maziwa na hii mifugo yote tunapeleka sisi Kenya wana- process wanatuletea sisi, kwa nini? Hivi hawajisikii aibu tunapoteza rasilimali za Taifa kwa mazingira ambayo Serikali inapaswa tu kuweka viwanda ili tuuze ndani humu? (Makofi) (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wameshindwa kujenga viwanda, hakuna muunganiko kati ya viwanda na mifugo, tukipeleka nje wanatu-charge wanasema tusitoroshe, tutatorosha tu. Tutatorosha tu na naamini mpaka watengeneze barabara ya kuzunguka mipaka hii, ili wazuie ng’ombe tumeshauza wengi sana. Watutengenezee mazingira rafiki ndani ya nchi ili wafugaji wapate masoko wauze nchini. Wasitembelee migongo yetu kwa sababu wao wameshindwa kutimiza majukumu yenu, wajenge mazingira rafiki. Tunaomba watuambie hizo tozo wataziondoa wakati gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu. Naomba nitoe ushauri kwa Serikali, moja, wafugaji watengewe maeneo yao na yalindwe kisheria; Ranch za Taifa ambazo wawekezaji wameshindwa kuendeleza watupatie tuendeleze sisi, hata tukilipia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, watuondolee tu kodi kwenye dawa za uogeshaji wa mifugo na chanjo za mifugo, sisi tutanunua, lakini waondoe kodi ili na sisi tuweze kuendesha wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, mapori ya akiba yatolewe yarejeshwe kwa wananchi.