Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala, lakini niwashukuru vile vile wananchi wangu wa Mtwara ambao leo hii wameniagiza kwa mara nyingine tena nimweleze Mheshimiwa Mpina kwamba kijana aliyeuawa na kikosi kazi chake ambacho alikiunda yeye cha kushughulikia uvuvi haramu katika Operesheni ya MATT ambayo inafanyika kwenye Bahari ya Hindi kuanzia kule Mtwara mpaka kule Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha salamu hizi kwa niaba ya wananchi wa Mtwara, wameniagiza nimweleze Mheshimiwa Waziri ile roho iliyoondoka, iliyopotea, kijana Abdillah Abdulrahman ambaye alipigwa risasi kisogoni kwake akiwa anatafuta kitoweo. Tunaomba kauli ya Serikali kwa sababu mpaka leo Serikali iko kimya na Wizara hii ndiyo iliyounda ile Tume ya Kushughulikia Uvuvi Haramu na huyu kijana alikuwa hafanyi uvuvi haramu. Tunaomba tamko na kauli ya Serikali kutoka Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nikiwa nasoma, nilisoma jiografia na historia, niliweza kusoma kwamba maelezo ya zamani ya vitabu vyote vimeandika kwamba Miji ya zamani Miji yote Tanzania na duniani kote ilikuwa inaanzishwa kutokana na mambo kadhaa. Jambo la kwanza, ni uwepo wa water bodies yaani vile vyanzo vya maji. Kwa hiyo, wananchi wengi wamejenga katika maeneo mbalimbali ambako maji yanapatikana kwa lengo kuu moja au mawili:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kutumia yale maji kwa ajili ya kuweza kujipatia chakula chao kwa kufanya uvuvi ambao tunasema subsistence kind of fishing ili waweze kuvua, waweze kutumia wale samaki kwa ajili ya kula. Hawa wananchi wamejenga kwenye vyanzo hivi vya maji waweze kupata wale samaki wanapokwenda kuvua mwisho wa siku waweze kupata pesa, wakiuza waweze kuendesha maisha yao, waweze kujenga nyumba, waweze kusomesha, waweze kufanya mambo mengi ya maendeleo. Nilikuwa nasoma mambo haya wakati nasoma historia wakati nikiwa sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, watu wengine wamejenga maeneo mbalimbali kwa sababu tu ya kufuata barabara. Sasa mimi na wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini ni miongoni mwa wananchi ambao tulijenga Mtwara, tuliamua kuishi Mtwara tangu mababu na mababu kwa sababu ya kufuata bahari ambayo ndiyo ilikuwa inatunufaisha kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunasikitika sana kwamba oparesheni hizi zinazoendesha (Operesheni MATT) na Operesheni Jodari) ambazo zinafanyika kwenye bahari kuu kwamba wananchi wanakatazwa kuvua samaki, wananchi wanakatazwa kwa maana nyingine wasile samaki wao ambao Mwenyezi Mungu amewapa na wao wameenda kujenga kwenye maeneo yale ili waweze kunufaika na samaki kwa kisingizo kwamba ni uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote na Wabunge wengine wamezungumza hapa kwamba hakuna anayetaka wanachi wafanye uvuvi haramu, la hasha, hata pale Mtwara mwaka 2008 wananchi walikamatwa wengi sana ambao walikuwa wanatumia uvuvi wa mabomu na sisi tulifurahia sana kwa sababu samaki waliendelea kupatikana na wananchi tulikuwa tuna-enjoy samaki, tuna-enjoy matunda aliyotupa Mwenyezi Mungu. Sasa wanavyosema kwamba eti kila nyavu ni nyavu haramu, hawa wananchi wa kawaida ambao Serikali hii haijawapa vifaa maalum vya kuvulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka 2008 tukiwa Chuo Kikuu pale tuliweza kuletewa samaki wa Magufuli wakati ule, tuliweza kula wale samaki zaidi ya mwezi mzima pale Chuo Kikuu kwa sababu walikamata meli moja tu ya Wachina waliokuwa wanavua wale samaki, wakaikamata, wale samaki tuligawiwa Vyuo vyote Dar es Salaam pale. Tuliweza kula mwezi mzima mpaka tukawachoka, hiyo ni meli moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wetu Serikali haijawapa vifaa, wanavua kwa nyavu za kawaida halafu wanakwenda kuwakamata, wanawaambia mnavua uvuvi haramu, wakale wapi? Waishi vipi? Wananchi hawa wanaishi kwenye maeneo ya bahari, wafanye kazi gani? Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Serikali ihakikishe ya kwamba inaleta vifaa vya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mtwara nimeshaandika sana, nimezungumza sana ndani ya Bunge hili kwamba wananchi wangu wamejiunga katika vikundi vidogo vidogo wanahitaji boti, wanahitaji zana za kisasa za kuvulia Serikali ituletee waweze kukopa wale wavuvi mwisho wa siku waweze kufanya uvuvi ambao hawaitwi uvuvi haramu, kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itekeleze hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, pale Mtwara kuna Chuo cha Uvuvi ambacho kimejengwa, huu ni zaidi ya mwaka wa saba hakijaanza kutumika, wanafunzi hawajaanza kusoma, zaidi ya miaka saba lile jengo lipo tu, lipo baharini kabisa pale Mikindani, ninapoishi mimi, bahari iko hapa kile Chuo kipo pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji sasa hiki Chuo kianze kufanya kazi, wanafunzi wafundishwe, waweze kusoma, mwisho wa siku tusifanye uvuvi haramu lakini Serikali haitekelezi, haitupi haya, mwisho wa siku wanakuja kutukamata kwa yale ambayo tunafanya, wanasema kwamba eti hatuvui sawasawa.