Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nami pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima na afya kuweza kukutana leo. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri leo asubuhi, lakini nilikuwa nataka nianze tu na ushauri mdogo tu kwake. Hii Wizara haitakiwi kuendeshwa kwa operations. Naomba sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji, wafahamu kabisa kwamba Wizara hii haitakiwi kuendeshwa kwa operesheni kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, operesheni zipo katika vikosi vya jeshi na kwenye theater za mahospitali. Kule ndiyo kuna operesheni. Wamefanya operesheni ya kwanza na ya pili, inatosha. Watoe elimu sasa, wasijikite kwenye operesheni kila siku, itakuwa kila siku kazi yao wanaifanya kama fire brigade sasa. Kazi yao ni kuzima moto tu. Waende wakatoe elimu. Nitatoa mfano mdogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la mitungi ya gesi limezungumzwa sana hapa. Mimi natokea Mafia, mwaka huu peke yake nimeshapoteza wavuvi zaidi ya watatu, wamekufa. Wamepiga marufuku kokoro, wameruhusu ring net ambapo watu wanakwenda katika kina kirefu cha mita 50, wakati huo unatarajia mvuvi aende aka-dive mita 50 chini bila ya kutumia mtungi wa gesi. Maana yake una-condemn to death, hakuna tafsiri nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa upande mwingine wanasababisha vifo kwa hawa wavuvi wetu. Sasa wanapokuja na hoja kama hizi za kusema kwamba wavuvi wasitumie mitungi ya gesi, mita 50 sijui wenzetu waliokuwa kwenye comfort zone, kwenye viti vyenu vya kuzunguka huko na Watendaji Maofisini sijui kama hawa wataalam wanakwenda kwa wavuvi na kuongea nao. Bahati nzuri kuna Chama cha Wavuvi na Wawakilishi wao, wapo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwa Mheshimiwa Waziri hebu wapate nafasi waende wakaongee na hao wavuvi wawaambie anayekwenda kuchukua majongoo kule chini ni nani na anayekwenda kuvua ni nani? Haiwezekani kosa la mmoja wakawahukumu wavuvi wote. Siyo sawa kabisa. Kama kuna dereva ameendesha gari akiwa amelewa, huwezi kufungia leseni za madereva wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inashangaza sana kama kuna wavuvi wanatumia mitungi ya gesi, wanafanya diving, wakifika chini kule wanachukua yale majongoo bahari, wa-deal na hao tu, wasiwazuie wote. Matokeo yake sasa tunapoteza watu na wavuvi wanafariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la hifadhi ya bahari nimekuwa nikilizungumza sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ameanza vizuri sana, ametuletea mtendaji mpya pale, nami natarajia kwamba tutakwenda vizuri, lakini lazima zile changamoto ambazo amezikuta pale azifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu ya Mafia na Mheshimiwa Ulega anafahamu, alikuja Mafia. Tunasisitiza siku zote, kanuni zao zinatuumiza kule Mafia. Leo Mafia, Halmashauri yangu inakufa. Hifadhi ya bahari, taasisi yenye staff wasiozidi 15 wanakusanya zaidi ya shilingi bilioni moja kutokana na maduhuli. Sisi Halmashauri ya Mafia ambao ndiyo Serikali, tunakusanya shilingi milioni 600. Ile Halmashauri inakufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumewaambia siku zote, wabadilishe ile kanuni, sisi tunataka asilimia 10 tu ya maduhuli yale. Nami naamini amekuja mtendaji mpya na pia Waziri mpya pale, wakae wabadilishe hii kanuni. Haiwezekani sisi Halmashauri ambao tunaendesha mambo mengi tupate asilimia 10 tu halafu Hifadhi ya Bahari ambayo staffing yake haizidi watu 15, wanachukua pesa chungu nzima. Kwa hiyo natarajia Mheshimiwa Waziri angalau mara hii kilio hiki watakisikia, wakabadilishe kanuni. Suala ni kanuni tu, wala siyo sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka jana naongea na Mkurugenzi wangu ananiambia mapato ya Halmashauri ya Mafia mwaka wa fedha unaisha mwezi ujao yako chini ya asilimia 47 na Waziri Mkuu bahati mbaya leo hayupo, lakini alishasema Halmashauri yoyote yenye kukusanya chini ya asilimia 80 inafutwa. Kwa hiyo, Halmashauri ya Mafia inakwenda kufutwa kwa sababu tu Hifadhi ya Bahari imechukua vyanzo vyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami katika kuongezea hili, nataka nisisitize, bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha yupo hapa, yale maduhuli yakusanywe na TRA inakuwaje sisi pale tuko watu wawili; kuna Hifadhi ya Bahari na kuna Halmashauri ya Mafia, lakini Hifadhi ya Bahari ndiyo wanakusanya halafu wanatoa gharama. Kwenye gharama mle sijui wanaweka night, safari, wanaweka maposho makali makali, halafu wakija wakitoa sasa wanasema tumepata shilingi milioni 700.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka chanzo hiki Mheshimiwa Waziri wa Fedha akichukue, TRA waende wakasimamie makusanyo ya maduhuli yanatokana na watalii kule Mafia. Hapo ndiyo itakuwa salama. Vinginevyo, tunaibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri leo asubuhi alikuwa akijibu swali hapa akawa anapata taabu kidogo katika kuelezea hawa samaki. Mimi sifahamu sana kuhusu samaki wa maziwani huko; furu, sijui nembe na gogo; sifahamu sana kuhusu hawa samaki. Ila kule baharini kuna misusa, ngawala na kuna samaki wadogo wadogo. Sasa tunaomba watupe tafsiri, tunawavua kwa nyavu zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali asubuhi alisema hapa kwamba hawa samaki wengi; nembe, sijui gogo ni samaki wapya waliokuja ziwani. Kwa hiyo, sheria ilianza halafu baadaye samaki ndiyo wakaja wakahamia. Sasa kama samaki walikutwa na sheria, kwa nini wameanza operesheni wakati wakijua hawa samaki walikuja baada ya sheria?