Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza naomba niliambie Bunge na Watanzania kwa ujumla kwamba kwa mujibu wa maandiko matakatifu, samaki hazijaweza kutosha Ziwa Victoria wala baharini. Kwa sababu Yesu alipokuwa akitembea kule Galilaya, aliwakuta akina Petro na ndugu zake wametupa jarife, wamechoka, wamekosa samaki, akawauliza, kwa nini mmechoka? Wakasema, tumekesha tunavuta, lakini hatujapata samaki. Akafanya miujiza yeye mwenyewe, ndipo wakavuta wakapata samaki. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Biblia, samaki baharini, samaki ziwani hawajawahi kutosha. Hilo lazima Bunge lijue na Taifa kwa ujumla lijue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nzuri iliyokuwa imeanzishwa na Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni nzuri sana kwa sababu uchafu ulikuwa umeshakithiri katika maziwa yetu. Tatizo ni moja tu kwamba badala ya kudhibiti uvuvi haramu, watu wanaonewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani leo tunazungumza uvuvi haramu, mtu unamkuta ana sangara mmoja wa sentimita 52 au wa sentimita 86 ambaye amempata tu kwa sababu nyavu hizi zinanasa samaki yeyote bila kubagua wakati mwingine. Huyu samaki wa sentimita 86, ukimkuta naye mmoja, unamkamata, unamwambia uhujumu uchumi, faini yake shilingi milioni 10, faini yake ni shilingi milioni 20, unategemea kwamba tunawasaidia wavuvi? Hatuwasaidii hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana Wizara hii haijapewa fedha za maendeleo miaka mingi, ndiyo maana sasa inatafuta fedha za faini ziwe fedha za maendeleo. Haiwezekani jambo hili brother, haiwezekani. Ni vizuri Serikali tukaiwezesha Wizara hii ikapata fedha za kutosha kuendesha Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusema kwamba ni Serikali hii ndiyo itakayomaliza uvuvi haramu, lakini siyo kwa staili hii. Kwanza wamefanya kazi kubwa. Wavuvi wale wakubwa sasa hivi hakuna anayevua haramu, yaliyobaki ni makokoro ambayo wameshindwa kuyadhibiti kwisha. Hata hivyo, najiuliza sana kwamba tukienda kwa style hii tutamaliza uvuvi haramu?

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Dau kwamba ni muda muafaka wa kutoa elimu sasa kwa wavuvi ili tuwe na uvuvi endelevu. La sivyo, tutamaliza gharama bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi task force ambazo ziko kule zinaendesha operesheni, ofisi zao ni Guest House. Hivi hakuna Ofisi za Serikali? Majengo ya Wakuu wa Wilaya yana nini? Wao ofisi zao zimegeuka kuwa Guest House, ni sawa sawa? Watueleze! Kwa sababu hata Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya hatambuliki na operesheni hizi, ni sawasawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hata faini hizi wanakataa kuingiziwa benki, wanataka uwapelekee cash, wakati mwingine unalipa kwa M-Pesa, ni sahihi? Ushahidi tunao. Yawezekana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu hamjui, lakini Watendaji wenu wanaofanya operesheni kule wana-sabotage Serikali. Haiwezekani hii brother! Lazima tukubaliane kwamba operesheni hii siyo msaada sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti umefanyika TAFIRI na wavuvi, ripoti ipo ya madhara ya macho 26 na madhara ya macho 78. Kuna madhara gani? Mapendeklezo ambayo tunajua sisi ni kwamba macho 78 hayana madhara yoyote kwa uvuvi wa Ziwa Victoria. Tunawasitisha wavuvi wetu wa nchi hii, Kenya inavua macho 78, Uganda inavua macho 78, hivi tunawasaidia Watanzania? Yawezekana Mheshimiwa Waziri hajui vizuri, kazi yake inaweza kuharibiwa na watu wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi nchi jirani tunaamini kwamba kuna sheria ambazo zinashabihiana: Je, tumeshindwa kuwa na sheria moja ambayo inaweza kuwezesha uvuvi endelevu kwa nchi zote hizi tatu ambazo tunatumia ziwa letu na bahari nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kiwanda cha Nyavu cha Arusha. Kiwanda hiki kilikuwa kinatengeza vyandarua, lakini kiwanda hiki kimegeuzwa kuwa kinatengeza nyavu. Wavuvi hawa wanasema, material yale ya vyandarua hayadumu kwenye maji kwa muda mrefu. Kwa hiyo, wanachukua miezi sita nyavu hizo zote zinaisha, tunawatia umaskini. Naomba wataalam wawashauri vizuri Mawaziri, ni material yapi yanayofaa kutengenezwa nyavu za kuvua katika Ziwa Victoria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la mifugo. Mifugo inakamatwa kwenye hifadhi. Inapokamatwa inapelekwa Mahakamani, wafugaji wakishinda kesi, hawarudishiwi mifugo yao. Tunawasaidia? Kama Mahakama imesema mifugo hii irudishwe kwa wenyewe, hairudishwi tunawasaidia? Itafutwe njia ya kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wengine mtu alikuwa amekamatiwa ng’ombe zake 260, anarudishiwa 76, wengine wamekufa. Ni sahihi? Tunataka wanapokamatwa ng’ombe wa wafugaji wetu, watunzwe, walishwe mpaka ambapo kesi itafikia muda wake wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la ufugaji, kuna na viwanda. Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga ni kiwanda ambacho kiko eneo zuri na kubwa, lina uwezo kabisa la kufugwa ng’ombe na kuchakata ng’ombe, lakini kiwanda hiki kimesimama. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, ifanye mkakati wa haraka kuweza kufufua kiwanda hiki pamoja na kiwanda cha maziwa kilichopo Utegi na kiwanda cha ngozi kilichopo Mwanza ili kusaidia mazao haya ya mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuniruhusu dakika moja, kuna mifugo inakamatwa inapotoka Minadani, wanataka ipakiliwe kwenye malori; ng’ombe watatu au wanne, hata mahali pa kupakia huko kwenye Minada ya Serikali hatujatengeneza. Tunawapiga faini bure hawa wafugaji. Hata wanapopeleka maeneo ya kwenda kupakilia, wamekaribia na gari wanaliona, ile task force. Wanawakamata wanawatoza faini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hili namwomba sana Mheshimiwa Waziri hata kama alikuwa halijui, alifuatilie watamharibia sifa na heshima ambayo alikuwa ameanza nayo vizuri. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.