Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa fursa hii na nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa mabadiliko makubwa aliyoyafanya kwenye uongozi wa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari (MPRU) kwa kuteua mtendaji mpya na kuvunja bodi ya taasisi. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aharakishe kuunda bodi kwani pesa za maduhuli kwa Halmashauri ya Mafia zimekwama kutolewa kwa sababu MPRU haina bodi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni uwekezaji uliofanywa na MPRU kwenye Kisiwa cha Shungimbili na Hoteli ya Thanda. Mwekezaji anatakiwa alipe service levy ya 0.3 kwenye Halmashauri ya Mafia lakini wawekezaji hawa wamegoma kulipa ada hii kwa maelezo kuwa wanalipa moja kwa moja kwenye MPRU. Hii ni kinyume na sheria kwani ada hii ni haki ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwekezaji huyu Thanda Hotel mwaka jana wakati nachangia nilimuomba Waziri awaagize wafute jina la Thanda Island kwani Kisiwa kile kinaitwa Shungimbili na siyo Kisiwa cha Thanda. Waziri aliahidi kuwa maelekezo yameshatolewa kwa mwekezaji kufuta jina la Thanda Island lakini mpaka hivi sasa tovuti rasmi ya hoteli hiyo inasomeka kwa jina hilohilo la Thanda Island. Nimuombe Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi jambo hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mipaka ya Hifadhi ya Bahari katika Kisiwa cha Mafia, ,mwaka 1994 wakati Hifadhi ya Bahari inaanza ilianza na vijiji vitatu tu yaani Jibondu, Chule na Juani, hivi sasa hifadhi ipo katika vijiji 13. Cha kushangaza zaidi uongezaji wa vijiji vya hifadhi umefanyika kinyume na matakwa ya kisheria na wananchi wa vijiji husika hawakushirikishwa na wameingizwa kwenye hifadhi bila ya kupewa fursa ya kuulizwa na wao kutoa ridhaa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni maduhuli yatokanayo na watalii kuingia katika maeneo ya hifadhi. Kanuni ya Hifadhi inayopanga mgao wa asilimia 70 kwa Hifadhi, asilimia 10 Halmashauri na asilimia 20 vijiji husika haipo sawa hasa kwa kuzingatia Halmashauri ya Mafia ina majukumu makubwa katika jamii kama elimu, afya, barabara na maji. Tunaomba Mheshimiwa Waziri abadilishe kanuni na mgao uwe 50/50 baina ya Halmashauri na MPRU.

Mheshimiwa Spika, suala la ubinafsishaji wa Visiwa vya Nyororo na Mbarakuni, namuomba sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe MPRU inashirikisha Halmashauri kwenye uwekezaji wowote katika Kisiwa cha Mafia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.