Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada zake za dhati za kutatua mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo. Mgogoro huu ulikuwa ni wa muda mrefu sana, wananchi walikuwa wanachomewa maboma yao, mifugo ilikuwa inateketezwa, lakini sasa wananchi wa Loliondo wanaishi kwa amani. Hii ni kwa sababu tunaona jitihada kubwa sana ya Serikali na najua kabisa kwamba vijiji vitarudi kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Arusha tuna wajasiliamali wadogo wadogo katika soko linaloitwa Masai Market lililopo karibu na CCM Wilaya ya Arusha Mjini. Soko hili lina wajasiliamali wanaofanya biashara za utalii hasa akina mama ndio wengi na tunajua mama ndiyo msingi wa familia. Wafanyabiashara hawa wamekuwa wanapata changamoto kwa sababu baadhi ya watalii wakija wakinunua vitu vyao hususani vinyago wanapata shida kupita airport, wanazuiliwa. Hali hii inaleta mkanganyiko kwa akina mama na tunajua kabisa wanatafuta vipato vyao kihalali kabisa. Naomba Serikali ijaribu kuangalia ni jinsi gani itawasaidia akina mama ili watalii hao wakinunua vinyago hivyo waweze kupita airport bila tatizo lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Arusha tumejengewa Kituo cha Polisi cha Kitalii cha Kidiplomasia. Kituo hiki kimejengwa kwa jitihada kubwa za Mkuu wetu wa Mkoa Ndugu Mrisho Gambo na wadau wa utalii (TATO). Hata Mheshimiwa Rais alipokuja alifurahishwa sana na ubunifu huu. Hata hivyo, kituo hiki pamoja na kwamba wadau wamejitahidi lakini tulikuwa tunaomba Serikali japo ituletee hata gari kwa sababu kituo hiki kimeleta heshima kubwa katika Mkoa wetu wa Arusha. Kituo hiki ni kwa ajili ya kutatua changamoto za watalii na wageni wanapopata matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mhifadhi wa Ngorongoro, Ndugu Manongi. Wanasema kwenye ukweli tuongee na mimi naongea ukweli. Ndugu Manongi aliajiriwa tarehe 30/10/2013 akaanza kazi Januari, 2014 alikuta mapato ya Ngorongoro yalikuwa shilingi bilioni 59. Kufikia Juni, 2017 alifikisha mapato shilingi bilioni 104 na Juni mwaka huu anategemea kufikisha mapato ya shilingi bilioni 122, ina maana atakuwa ameongeza mara mbili ya kiasi alichokikuta. Hadi sasa ameshakusanya zaidi za shilingi bilioni 110. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ngorongoro lilikuwa shamba la kuiba yaani watu walikuwa wanaiba, kulikuwa hamna chochote. Huyu Ndugu Manongi nakumbuka alipigwa vita sana, sasa nimegundua kumbe vita ilikuwa kwa sababu ya kubana matumizi kama hivi. Kwa hiyo, naomba sana nichukue nafasi hii kumpongeza Bwana Manongi na naomba aendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu huyu Ndugu Manongi kajitahidi kuongeza aina mpya ya utalii, utalii wa miamba ya mabadiliko ya sura ya nchi (Geotourism). Naomba nimpongeze sana. Vilevile ameboresha mapango ya Olduvai Gorge sasa yamekuwa katika mazingira mazuri sana, hata Makamu wa Rais alikuja akazindua. Kama watendaji wengine wangekuwa kweli wanamsaidia Mheshimiwa Rais hivi, kwa kweli Rais wetu angekuwa hana kazi kubwa sana, hongera sana Bwana Manongi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wa hoteli za middle class wamekuwa wakipata shida sana kwa sababu ya tozo nyingi. Wafanyabiashara hawa wamekuwa wakitoza watu Sh.25,000 hadi Sh.45,000, lakini wanatozwa TALA license USD 4,500, ambayo ni kama milioni 6, hapohapo kuna property tax. Tunajua sasa hivi biashara ni mbaya na ukijumlisha kodi na tozo, wana kodi 56. Wafanyabiashara hawa Waziri alikuja tukakaa kikao, Waziri aliondoa TALA licence, lakini aliondoa kwa kuongea tu hakuweka in writing, kwa hiyo hawa wafanyabiashara wamekuwa wakisumbuliwa sana. Huku wenyewe wanasema Waziri ameiondoa, huko wanapotakiwa watoe wanaambiwa hatuna barua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mheshimiwa Waziri namwamini na naamini utendaji wake, naomba sana aweke kwa maandishi ili hawa wafanyabiashara wa middle class hotel waache kusumbuliwa na kama alitoa agizo naomba aliandike. Mheshimiwa Waziri kwa sababu namwamini najua hata hii lunch break anaweza kuandika hiyo barua, kwa sababu wafanyabiashara hawa wamekuwa wakisumbuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wafanyabiashara wa utalii wamekuwa na changamoto kubwa sana, wana kodi nyingi sana ambazo wanatakiwa watoe lakini kodi hizi zinapitia sehemu nyingi sana, wenyewe wako tayari kutoa lakini wanaomba liwekwe dirisha moja. Kwa sababu zimekuwa zinawapotezea muda wao mwingi kutembea huku na huku ili kulipa kodi hizo. Tatizo hili lingeweza kutatuliwa kwa dirisha moja tu. Hii inasaidia pia kuokoa muda na pia usumbufu kwa hawa watu unakuwa umemalizika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nashauri, Arusha kingejengwa Kituo cha Kuvutia Watalii (Theme Park).
Hii park itasaidia sana kwa sababu tumeona watalii wanakuja Arusha wanaenda mbugani lakini tukiweka kivutio kama hiki, tuweke kumbi za starehe, tuweke hata zoo wale watalii wakija watakuwa wanapata muda wa kukaa Arusha na vilevile na sisi tutachukua hizo dola zao. Kwa sababu watalii wakija wanaenda mbugani, wakitoka mbugani wanaondoka. Tukiwawekea kitu ambacho kitasababisha wale watalii waendelee kukaa pale Arusha itatusaidia sana kuingiza pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla na Naibu wake na uongozi mzima wa Wizara. Tumeona tangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla amechagulia jamani yuko field muda wote anafanya kazi. Tukubali, tukatae wanamsaidia Rais, wanafanya kazi nzuri sana. Hongera Mheshimiwa Waziri, tuko na wewe na tunakuunga mkono. Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla amekuwa msikivu hata ukimwambia issue yoyote anaitatua kwa haraka. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri, endelea kuwa na moyo huo huo, endelea kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atakapokuja kujibu, anijibu kuhusu hii barua ambayo aliongea kwa maneno, anatakiwa aweke kwa maandishi na vilevile hizi tozo za hawa wadau wa utalii ambao wanataka liwe dirisha moja. Nakuamini sana Mheshimiwa Waziri najua hii utalitendea haki kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Tumeona alivyokuja Arusha, alijumuika na wadau wengi wa utalii. Vilevile pongezi zangu ziende kwa Mkuu wangu wa Mkoa wa Arusha, tumeona anavyojitahidi kukuza utalii wetu kwa kukutana na wadau mbalimbali na wadau wa utalii sasa hivi wamekuwa wanaongea kitu kimoja hata wakileta tatizo wanalileta kwa umoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.