Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kupata nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Kwa sababu ya muda, nianze moja kwa moja na hotel levy pamoja na bed night levy kwa maana ya tozo zinazotozwa na hotel za kitalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Serikali yetu kupitia Mamlaka ya Serikali za Mitaa imejiwekea utaratibu wa kukusanya mapato kwa namna tofauti kwa misingi ya sheria. Katikati hapa kumekuwa na sintofahamu ya mwingiliano baina ya tozo ambazo zinatokana na bed night levy ambayo inatozwa na Bodi ya Hoteli za Kitalii ambayo imekasimiwa kwa TRA lakini halmashauri zinatoza hotel levy. Kumekuwepo na mkanganyiko ambao kwa muda fulani hivi umepelekea halmashauri hizi kupoteza mapato yake kwa namna fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Makatibu Wakuu wa Wizara hii ya Maliasili na Utalii lakini pia Katibu wa TAMISEMI. Nimezungumza nao na wamelichukulia suala hili serious na hivi navyoongea niwakumbushe na niwasisitize juu ya kuleta mabadiliko ya sheria hapa ndani ili kila mamlaka isimamie ukusanyaji sehemu inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ni juu ya matumizi ya nishati ya mkaa na kuni. Imekuwepo kasumba au tabia kila hoja inayoibuka watendaji wanakwenda kutekeleza kwa namna wanayofikiri wao inafaa kuliko sheria inavyotaka. Hili limewakumba watu wengi sana, siyo tu Waheshimiwa Wabunge wanaotoka kwenye maeneo ya mijini lakini hata huko kwenye majimbo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Bunge hili halijawahi kutunga sheria ya kuzuia matumizi ya mkaa. Pia ni ukweli usiofichika, nimshukuru Waziri na Naibu wake, ukisoma katika ukurasa wa 37 wamesema vizuri kwamba zaidi ya asilimia 85 ya nishati yote nchini inatokanana na kuni na mkaa. Zaidi ya yote wamesisitiza wakasema takribani asilimia 90 ya wananchi wote hutegemea nishati hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sote tunafahamu wananchi zaidi ya asilimia 90 wanategemea nishati ya mkaa na kuni, inakuwaje leo mwananchi anayekutwa na baiskeli na pikipiki amebeba gunia moja, mawili anakuwa ni haramu katika nchi hii? Sote tunafahamu umuhimu wa matumizi ya mkaa na changamoto iliyopo. Mambo ya mabadiliko ya tabianchi ni lazima yaendane na muda huku tukimthamini mwananchi ambaye anawajibika kwenye hii asilimia 90. Mwananchi wetu wa leo asilimia 90 tunayoizungumza ni mwananchi ambaye anaijua leo yake na kesho yake haitambiui. Wananchi wengi kule tunapotoka, napotoka Nyamagana wapo wananchi wana uwezo wa kununua kifuko au kitini cha Sh.500 akatumia matumizi ya siku hiyo ili kesho yake ifike ajue kesho itakuwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi navyozungumza na wewe tarehe 16 kwenye Kata ya Buhongwa kwenye maeneo ya Nyanembe, Nyangwi kwenda Bulola kule chini mpaka kwenye mpaka wa Misungwi mambo haya yanafanyika. Mambo haya yanatokea hata kwenye Wilaya nyingine za jirani za Magu na Kwimba. Waziri wananchi wananyanyasika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Mwanza leo liko kundi kubwa la wafanyabiashara wanaouza kahawa, wako wa mama ntilie wanaotumia mikaa hii ili shughuli yao iende. Zaidi ya yote wako watu wanapika vitumbua. Sasa leo mtu anapika vitumbua akatumie gesi anaipata wapi? Mtungi mdogo wa gesi ni Sh.18,000, hiyo ni kujaziwa tu, ukienda kununua mtungi na gesi yake ni zaidi ya Sh.36,00. Gesi kilo 15 ni Sh.52,000 mpaka Sh.54,000, hiyo ni kujaza tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza vizuri, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwenye hotuba amesema sawasawa muendelee kufikiria umuhimu wa kutengeneza mkaa mbadala. Wako wataalam wanasema kupitia taka zinazozalishwa majumbani unaweza ukatengeneza mkaa mbadala na ukasaidia. Mwanza peke yake Nyamagana kwa siku tunazalisha tani 350 za taka. Sasa ukienda pale dampo kwa mwezi tuna tani ngani, ni mkaa mbadala kiasi gani unaweza ukazalishwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha watujibu sawasawa matumizi ya mkaa yanaruhusiwa au hayaruhusiwi? Kama hauhusiwi mbadala wake ni upi ili wananchi wajue. Kama hatuna mbadala wa namna ya asilimia 90 ambao ni watumiaji wa mkaa na kuni wananchi wataendelea kunyanyasika na kukosa amani maana sasa baiskeli na pikipiki nyingi zimekamatwa. Hatujafika kwenye kiwango cha kuzuia matumizi ya mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku amesema vizuri, ninukuu kidogo, Mheshimiwa Waziri amesema, wanaangalia namna bora ya kufundisha wananchi juu ya kutengeneza majiko banifu. Pia wamesema wanaangalia namna bora ya utaratibu wa kutengeneza au wa ulinzi wa misitu ya miti ya mkaa. Ulinzi huu lazima uanzie kule inakozalishwa mikaa. Juzi ameenda mtu mmoja pale kakuta mtu katandika mkaa wake, kaweka kwenye vitini kafunga na mikaa, hajakaa sawa anaingia ndani anatafuta mkaa ulipo anakamata, anatoka kwenye mkaa anatafuta na stoo anachukua mpaka uliopo stoo. Hii siyo sawa! Sijui mnanielewa maskini ya Mungu? (Makofi)

Hii siyo sawa Mheshimiwa Waziri. Ni lazima tuhakikishe watendaji tunaowatuma kufanya kazi hii wanaifanya kwa weledi na ubora tukihakikisha maisha ya Watanzania tunaendelea kuyalea ili waendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine amesema watahakikisha wanafundisha mbinu mbadala lakini kuangalia maeneo maalum yatakayokuwa yanauziwa mikaa hii. Hili jambo lifanyike mapema na ijulikane mikaa yote itakuwa inanunuliwa sehemu fulani. Mwanza tuna Kata 18 tuambiwe kata zipi na zipi, kama ni za mipakani, kama ni za katikati ili mikaa hii ipatikane na mwananchi anayekutwa na gunia moja asiwe haramu au haramia, tukifanya hivyo itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima tuseme, Waziri ametuambia yuko tayari kutambua wauzaji wa mikaa, inachukua muda gani kutambua wauzaji wa mikaa, wako wengi, wako wakubwa, wa kati na wadogo. Wale wakubwa ndiyo wanagawa kwa wadogo huku. Mama mwenye maisha yake ya kawaida mjane ana uwezo wa kuuza gunia moja likiisha anaongeza lingine. Lazima tuwaonee huruma watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho amesema wataangalia namna bora ya kuhamasisha ili taasisi nyingi zinazotumia mkaa zielimishwe juu ya matumizi haya. Nishauri siyo tu kuelimishwa, waelimishwe zaidi taasisi hizi juu ya kupanda miti kabla ya kuikata itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka leo nijikite sana kwenye mkaa kwa sababu napotoka ndipo kuna wauza kahawa wengi, wapika vitumbua wengi na mama lishe wengi, wote hawa wanatumia nishati ya mkaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini sio mwisho kwa umuhimu, niwapongeze sana watendaji wote wa Kituo cha Saanane. Mheshimiwa Waziri nimkushukuru sana, leo tunazungumzia watalii wanaokwenda kwenye kituo Saanane wapatao 12,600, hii siyo idadi ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya kazi kubwa, wameboresha njia na wameboresha kila namna ya kuvutia watalii. Naomba watuimarishie uwanja wetu wa Mwanza ili kwenda sambamba na utalii huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.