Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze mdogo wangu kwa kazi nzuri anayofanya japokuwa ni kazi ngumu sana, kuna wakati anakimbia badala ya kutembea anawahi kusikoeleweka. Kuna siku nikamwambia mdogo wangu hebu rudi nyuma kidogo, namshukuru alinisikiliza na namuomba aendelee na kazi vizuri sisi tuko nyuma yake tutamsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizungumzie mambo mawili tu. Jambo la kwanza ni mbuga ya Wembere ambayo ni hifadhi iliyokuwa imeanzishwa na wakoloni mwaka 1940 kwa ajili ya kutunza wanyama lakini pia ilikuwa ni kwa ajili ya mapito ya wanyama kwa sababu inaunganika na Serengeti. Baada ya uhuru, Serikali iliisahau kidogo hii mbuga, mbuga hii inaanzia Mkoa wa Shinyanga, inapita Mkoa wa Tabora lakini pia iko Mkoa wa Singida, ni bonde la ufa linaloelekea Lake Eyasi. Ilivyotelekezwa wanyama wengi walimalizika kwa sababu waliwindwa bila utaratibu, lakini pia mabadiliko ya tabianchi bonde hili lilikauka mwaka 1974 na wanyama wakaisha kabisa. Lilikuwa pia ni mazalia ya ndege wanaotoka Ulaya, walikuwa wanakuja kuzaa wakati wa kiangazi huku na sasa hivi kwa sababu mazingira yameharibika, hawaji tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mbuga hii imekosa sifa ya kuitwa hifadhi kama ilivyokuwa zamani. Kwa sababu hiyo, wananchi wengi walihamia, hiyo miaka ya 70 mpaka 80 na Serikali ikapima vijiji na kata kwenye mbuga hii. Kwenye mbuga hii kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, kuna kata zaidi ya saba lakini kule Singida na kwenyewe ziko kata nyingi kweli kweli sikumbuki ni ngapi. Ukienda Shinyanga kuna kata kama tatu hivi, kule Meatu, wananchi wako mle ndani. Kutokana na kukosa sifa na watu kukaa mle ndani, shughuli za kilimo zimeongezeka sana. Ndiyo tunapozalisha mpunga, mkipita Igunga mnakuta mpunga mzuri unaonukia au mchele unaonukia, unatoka kwenye mbuga ya Wembere. Pia ufugaji umeendelea kupanuka kwa sababu watu ni wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo sasa, ugomvi kati ya wafugaji na wakulima umekuwa mkubwa sana na miaka kadhaa watu wamegombana kama kule Isakamaliwa mpaka wengine wakauawa. Pia, pale Makomelo ukiwa unakaribia Igunga, kulikuwa na ugomvi mwaka jana, watu walijeruhiwa sana. Ukienda Itumba nakotoka mimi kama unaelekea Loya kule kwa ndugu yangu Mheshimiwa Musa Ntimizi na kwenyewe watu walipigana sana kwa sababu watu ni wengi, maeneo ya kuchunga na kulima ni machache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwaka 2014, tuliandika barua Wizara ya Maliasili na Utalii ili wabadilishe matumizi ya mbuga hii, waiangalie, wabakize eneo dogo lakini lingine wawaachie wananchi. Mwaka 2012 Serikali iliunda kamati ya wataalam wakapitia mbuga na hifadhi nyingi kuangalia ipi imekosa sifa. Moja ya mbuga ambayo imekosa sifa ilikuwa ni mbuga ya Wembere. Namuomba Mheshimiwa Waziri, nimemwandikia barua tena, naomba akaitazame mbuga hii, karibu Igunga Waziri, tukaitembelee, aje na wataalam wake tuone ni jinsi gani tunaweza tukabadilisha mipaka ili wananchi wetu waweze kupata mahali pa kulima pamoja na kuchunga ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nilitaka kuzungumzia ni ukurasa wa 90 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri, kuhusu Idara ya Mambo ya Kale na anazungumzia majengo ya kihistoria kama ya Dar es Salaam na maeneo ya kihistoria kama Engaruka na kadhalika. Sisi tulikuwa na utawala wa Kitemi na wewe Mwenyekiti ni Mtemi na hata mimi natoka kwenye utawala wa Kitemi wa Usongo. Tuna maeneo ambayo Watemi sasa hivi wameyaacha, ukienda kule Meatu, Igunga, kwa mfano, Igunga kuna Mtemi Shomari Ng’wanaasali nyumba yake bado ipo pale Igurubi. Kuna Mtemi mwingine anaitwa Kasanda wa Unambiu na yeye nyumba yake bado ipo. Kuna Mtemi Ntinginya na akina Humbiziota nyumba zao bado zipo. Ukienda Urambo au tuseme Tabora yuko Mtemi Mirambo na yeye nyumba yake bado ipo na Watemi wengi sana masalia yao bado yapo. Isike pale kuna masalia na sehemu nyingine nyingi lakini Wizara haichukui tahadhari yoyote, haiweki programu yoyote kuyahifadhi maeneo haya. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu wanzishe mkakati maalum wa kuyatambua maeneo ya Watemi wetu hawa, wayapandishe hadhi, wayahifadhi, Wazungu ambao ni watawala wetu kwa hakika wakisikia kwamba maeneo haya yako tayari na hasa Wajerumani, watakuja kuyatembelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maeneo hayo pia yaendane na ngoma zetu za jadi. Mheshimiwa Waziri, mkishirikiana na Wizara ya Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, mnaweza mkaanzisha taratibu hizi kwenye utemi huo, watu wanacheza ngoma, embinabhabha, tunazihitaji ngoma zirudi ili wananchi wetu waendelee kucheza. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri anisikilize, nilishawahi kusema last time juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kusema ni ng’ombe ambazo zinakamatwa kwenye hifadhi. Kwa kweli tunatambua umuhimu wa kutunza maeneo. Tunatambua na tunataka hifadhi itunzwe lakini namna ambavyo hatua zinachukuliwa kuwafanya hawa watu wasipeleke ng’ombe haziendi vizuri na actually zinafanywa na wale wadogo Mheshimiwa Waziri anaweza asijue. Wale vijana waliomaliza kidato cha nne na kupata hizo kazi wanavaa nguo za kijana, nadhani hata leo wapo wanafanya kazi vibaya. Wengi ni matajiri hao vijana, wamejenga majumba kwa sababu ya hizo ng’ombe na wana magari kwa sababu ya hizo ng’ombe. Kwa hiyo, kuna tatizo katika utekelezaji wa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri waangalie namna ya kutekeleza jambo hili kama wanataka kulifanya vizuri. Wakilifanya hivi wanavyolifanya kwa kweli wananchi wanajisikia vibaya, wanajisikia wameachwa katika nchi yao. Wako wananchi wengi sana ambao wamechukuliwa ng’ombe wao. Kuna mtu namfahamu yuko hapa, nilikuwa naongea naye, ng’ombe wake 4,000 walichukuliwa na wakauzwa, mzee wa watu ana hali mbaya sana. kuna mwingine ana kesi mpaka mahakamani lakini wakati kesi inaendelea, zikauzwa, wala hawajali kwamba kuna kesi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, itazameni upya tena hii program ya kukamata hawa ng’ombe kwenye hifadhi ili muweze kufanya hii kazi vizuri, hatukatai, ni lazima tuhifadhi maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapori mengi sana ambayo yamepitwa na wakati kama mbuga ya Wembere nilivyosema yagawiwe kwa watu waweze kuchunga. Sehemu nyingi sana maeneo yamepitwa na wakati. Kule Nzega kuna sehemu moja inaitwa Ipala na kwenyewe watu wanafukuzwa kwenye hifadhi, kuna mjomba wangu kule mzee Charles alichomewa nyumba zake zote. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, tambueni maeneo haya ambayo yamepitwa na wakati muwape wananchi waweze kuchunga na hiyo changamoto ya kuingiza ng’ombe kwenye hifadhi inaweza ikapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona nimefika mwisho, nashukuru sana. Narudia tena, mbuga ya Wembere Mheshimiwa Waziri, tafadhali tupeni mbuga tuweze kuitumia kadiri ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya makazi, hifadhi, kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja.